Katika makala niliyotoa ambayo yana kichwa Ndugu Waislamu Nisaidieni, wapo
ndugu zangu Waislamu ambao wamejibu. Mmojawapo ni Maalim Moses – Mzizimkavu. Nakushukuru
Maalim Moses kwa yale uliyosema. Basi na mimi nimeona niseme kuhusiana na kile
ambacho amekisema Maalim Moses huku nikiamini kuwa huu utakuwa ni mwanzo na
mwendelezo wa mjadala wenye manufaa kwetu sote.
Niwie radhi kwa kuwa sikuweza kukujibu mara moja. Hii ni kwa sababu
niliibiwa laptop yangu, hivyo nikawa sina uwezo wa kufanya kazi hii. Hata hivyo,
namshukuru Bwana wangu Yesu kwa kuwa amenipatia laptop nyingine na sasa naweza
kuendelea tena.
Pamoja na kwamba yapo mambo mengi ambayo nina mtazamo tofauti na wa kwako,
lakini kati ya mambo mazuri, jambo mojawapo jema sana ndani yako Maalim Moses –
Mzizimkavu ambalo siwezi kulipita bila kulitaja ni nia yako ya dhati ya kutaka
kuishi kwa ajili ya Mungu wa kweli. Katika hilo nakupongeza na unanipa
changamoto kubwa. Si wewe tu, bali pia Waislamu wengi ambao tangu alfajiri na
mapema sana huenda msikitini kuswali na kufanya hivyo mara 5 kwa siku kwa moyo
wa dhati. Nia hiyo na moyo huo si jambo dogo hata kidogo. Kuhusu kwamba kile
kinachofanyika huko ni sahihi au si sahihi, hilo ni suala jingine.
Hata hivyo, kama ulivyonipa changamoto ukiniambia (nikikunukuu), "Hebu
kaa pembeni acha kila kitu uwe huru wa mawazo tuanze kujadili." Changamoto
hiyo mimi naikubali, lakini nami pia nakuomba ufanye hivyo hivyo. Fungua
ufahamu wako. Usiogope kuhoji mambo – maana nimeona katika majibu yako kwangu
umeanza kuwaomba msamaha Waislamu wenzako kwenye sehemu kadhaa.
Kama ukifungua moyo na ufahamu wako, hakika mwisho wa safari, utakutana na
Mungu wa kweli; pia na kweli ya Mungu – iwe imo katika Uislamu au katika
Ukristo; moyo wako utakwambia tu kwamba ‘Maalim, kweli uliyokuwa unaitafuta
maisha yako yote ni hii hapa!’
Pamoja na kwamba hujanijibu hoja yangu hata moja (yaani hoja zile 7 ambazo
nilizitoa kwenye makala yangu uliyoinukuu) zaidi tu ya kusema kwamba kile
nilichofanya ni kunyofoa, kubinya na kukata aya ‘out of context’ [na hii
hainishangazi kwa kuwa ni namna moja ya kujibu hoja ambayo imezoeleka sana
miongoni mwa wajibu hoja Waislamu wengi pale wanapokabiliwa na hoja kama hizi.
Namna nyingine wanayotumia sana ni kusema kuwa sisi Wakristo ni ‘brainwashed’
kwa hiyo hatuko tayari kukubali ukweli hata kama umewekwa mbele yetu].
Inawezekana nikawa nimefanya hivyo kama usemavyo, lakini nadhani jambo la
msingi usiishie kwenye kusema tu kwamba mimi nimepotosha au niko ‘brainwashed’,
bali unionyesha kabisa nilikokosea; na
ikiwezekana uniongoze kwenye njia ambayo wewe unaamini kuwa ni sahihi kwa kutumia
maandiko yako na hoja zenye mantiki.
Hata hivyo, umesema kuwa unatosheka na majibu niliyopewa na Mahmuud na
Hamudi, ambayo yako kwenye blog hii yangu lakini pia yako kwenye blog tofauti
aliyoifungua ambayo iko HAPA. Huenda
umesoma mwitikio wangu kwa majibu yao hayo.
Mwitikio wangu huo nimeuweka katika sehemu nne – yaani Majibu ya Hamudi
Sehemu ya KWANZA,
sehemu ya PILI,
sehemu ya TATU
na sehemu ya NNE.
Nikirudi kwako Maalim Moses – Mzizimkavu, umetoa changamoto nyingi kama
alivyofanya Hamudi. Basi nitajaribu kuzivunjavunja ili iwe rahisi kuzijibu. Pia
nimezifupisha ili nisilazimike kuandika tena kila kitu ulichosema. Lakini kama
mtu anataka kuzisoma kwa urefu na ukamilifu wake, basi ziko kwenye sehemu ya
maoni na msomaji anaweza kuanzia HAPA.
**********
1. Maalim Moses anasema: Hukumbuki
kongamano la Nicea ambalo liliingiza itikadi ambayo mnaamini hadi leo, yaani
itikadi ya TRINITY au UTATU?
Jibu langu:
Unaposoma katika Matendo ya Mitume 15 unakutana na Kongamano la Kwanza
kujadili mambo ambayo yalikuwa yanawatatiza Wakristo katika nyakati za mitume.
Katika kipindi hicho, Injili (au Ukristo) ndio kwanza ulikuwa unatoka
Uyahudi na kuingia kwenye sehemu nyingine duniani; yaani kwa watu wasio
Wayahudi ambao wanaitwa watu wa Mataifa. Sasa, Wayahudi washika torati walikuwa
wanawafundisha watu wasio Wayahudi kwamba kama wanataka kwenda mbinguni ni
lazima wafuate mambo ya sheria au Torati (kama unavyofanya wewe Maalim Moses).
Kwa mfano walisema kwamba, “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi
kuokoka.” (Mdo 15:1).
Hali hii ilileta mkanganyiko mkubwa na matokeo yake, ilibidi mitume
wakutane Yerusalemu katika kongamano ambalo lilikuwa la kwanza kabisa ili
kujadiliana. Imeandikwa: Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno
hilo. Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama … (Matendo 15:6-7).
Hatimaye walipitisha uamuzi kwamba mambo hayo hayana nafasi katika wokovu
wa mwanadamu. Kati ya yale ambayo Petro alisema ni haya: Basi sasa mbona
mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu
wala sisi hatukuweza kulichukua. (Matendo 15:10).
Ninachotaka kusema ni kuwa, mabishano kuhusu mambo ya Mungu si jambo geni.
Yalikuwapo na yataendelea kuwapo hadi mwisho wa safari yetu ya maisha hapa
duniani.
Nilimwuliza Hamudi swali hili: Kama ninyi Waislamu mnasema kuwa kitabu
chenu ni kimoja na hakijabadilika, kwa nini mna madhehebu mbalimbali? Kwa nini
kuna Waislamu wa itikadi kali (kwa mfano Wahabi) na wale wa itikadi za wastani?
Jibu ni rahisi tu – ni tofauti za tafsiri za maandiko. Maandiko ni yaleyale
lakini tafsiri zinakuwa tofauti kutegemea na mtu na mtu. Na katika tofauti
hizo, ni wazi kuwa wapo ambao wanatoka nje kabisa ya kile kilichoandikwa.
Sasa hebu turudi Nicea. Rafiki yangu Maalim Mzizimkavu, najua kuwa hoja hii
kuhusu utatu kuingizwa na kongamano la Nicea si yako bali ni hoja ya Waislamu
wengi ambao wanajaribu kupinga Biblia. Ni hoja ambayo imeenezwa na watu kama
vile hayati Ahmed Didat wa Afrika Kusini.
Napenda nikufahamishe wewe na wengine kwamba, hoja hii haina nguvu zozote
kwa sababu si ya kweli hata kidogo. Unachojaribu kusema hapa ni kuwa itikadi ya
Utatu iliingizwa kwenye Biblia na kongamano hili.
Ndugu yangu, baada ya Yesu na mitume kuondoka, kulikuwa na mambo mengi
ambayo watu walibishania. Mambo hayo ni pamoja na yafuatayo:
- Yesu ni Mungu au ni mwanadamu?
- Yesu aliumbwa au hakuumbwa?
- Yesu na Baba ni wamoja au ni wawili tofauti?
- Je, Baba ndiye Mungu mmoja wa kweli au Mungu mmoja wa kweli ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu?, n.k.
Kongamano la Nicea lilifanyika miaka 320 baada ya Kristo, na miaka zaidi ya
mia mbili baada ya Paulo. Mambo haya ya Utatu TAYARI yalikumo ndani ya Biblia.
Suala la Uungu wa Yesu na Utatu ni mambo ambayo tayari yalishakuwako tangu
karne mbili au tatu kabla ya kongamano hilo. Shida ilikuwa kwenye TAFSIRI.
Baadhi, kama ilivyo hata leo, walikuwa wanahoji mambo kama nilivyokuwekea hapo juu.
Kwa hiyo, kwa sababu mambo haya yalianza kuleta mgawanyiko kwenye Kanisa na
hata kwenye dola ya Roma, ndipo mtawala wa Roma, Mfalme Constantine, akasema
mtabishana hadi lini? Ninyi wakuu wa dini hebu kaeni chini mtoe maamuzi ambayo
yatafuatwa na kila Mkristo, yaani na kanisa lote, kuliko ilivyo sasa ni vurugu
tu. Kumbuka kuwa wakati huo dola ya Rumi ambayo ilikuwa chini ya mfalme huyo
ilishakubali Ukristo kama dini rasmi ya dola nzima baada ya miaka mingi ya
mateso makubwa kwa Wakristo wa nyakati zile chini ya watawala wa Roma
waliotangulia.
Ndipo walikutana maaskofu takribani 300 kwenye mji wa Nicea kule Uturuki.
Mwisho wa majadiliano yao, WALIAFIKI kile ambacho Biblia inasema tangu karne
nyingi nyuma; kile ambacho kilikuwa ni mafundisho ya mitume – kwamba Mungu Baba
na Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu yuleyule mmoja katika nafsi tatu.
Kongamano la Nicea HALIKUTUNGA wala KUANZISHA Utatu kamwe!
Hebu ona maandiko haya machache tu ya Biblia:
- Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi... Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. (Mwanzo 1:1-3) - Maneno haya yaliandikwa na Musa takribani miaka 1600 KK, yaani ni miaka karibia 2000 kabla ya kongamano la Nicea. Katika andiko hili, Mungu maana yake ni Baba, Roho maana yake ni Roho Mtakatifu, na neno 'akasema' linamwongelea Neno la Mungu, yaani Yesu, maana Yesu anaitwa Neno la Mungu kama utakavyoona kwenye andiko linalofuata.
- Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye huyo alikuwa Mungu. (Yohana 1:1) – haya nayo yaliandikwa na Yohana kwenye mwaka 30 BK, yaani miaka 290 kabla ya kongamano la Nicea. Neno maana yake ni Yesu.
- Basi Bwana ndiye Roho (2 Wakorintho 3:17) - haya maneno yaliandikwa na Paulo kwenye mwaka 60 BK, na miaka 260 kabla ya kongamano la Nicea. Maana yake ni kusema Yesu ndiye Roho Mtakatifu.
- … na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili, ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele. (Warumi 10:5) – haya pia ni maneno ya Paulo ambayo yaliandikwa kwenye mwaka 60 BK, yaani miaka 260 kabla ya kongamano la Nicea.
Maandiko haya manne kati ya mengi kwenye Biblia yanatuonyesha wazi kuwa
Mungu Baba ndiye Neno (Yesu); Bwana Yesu ndiye Roho Mtakatifu; kwa hiyo Mungu
Baba ndiye Roho Mtakatifu. Hawa watatu ambao ni mmoja. Maandiko au maneno haya
yalikuwapo ndani ya Biblia kwa maelfu ya miaka kabla ya kongamano la Nicea
ambalo watoa hoja wa Kiislamu wanajaribu kuwadanganya watu kwamba eti suala la
Utatu Mtakatifu liliingizwa kwenye Biblia wakati wa kongamano hilo.
Kwa hiyo, Maalim Mzizimkavu, hoja hii haina mashiko KABISA wala sehemu ya
kuegemea kwa kuwa msingi wake hauko sahihi. Kile ambacho kinatumiwa kuijenga
hakina ukweli wowote. Ni hoja iliyojengwa kwenye msingi wa uongo. Na uongo SIKU
ZOTE hatima yake ni anguko, hata kama mwanzoni utajiinua hadi kupita vimo vya
mawingu.
Kongamano la Nicea KAMWE HALIKUINGIZA itikadi ya Utatu kwenye Biblia.
Badala yake, kongamano hilo lilifanya
kazi ya kukataa tafsiri potofu juu ya Yesu na Utatu ambazo zilikuwa zinaenezwa
na wapotoshaji kama vile Arius aliyekuwa mhubiri kutoka Libya na kukubaliana na
mafundisho sahihi ya Biblia ambayo yalikuwapo tangu maelfu ya miaka kabla ya
kongamano lenyewe.
2. Maalim Moses anasema: Mama wa mtoto
wa Mungu (Maria) naye ni Mungu.
Jibu langu:
Kimsingi rafiki yangu Maalim Moses, hapa hakuna hoja yoyote. Hakuna sehemu
yoyote katika Biblia inayosema kuwa Maria mama wa Yesu ni Mungu. Ukinionyesha
sehemu hiyo, ndipo nitaweza kujibu suala hili. Lakini kwa hivi lilivyo hata
halina haja ya maneno mengi zaidi tu ya kusema Maria si Mungu bali ni mwanadamu
kama mimi na wewe na hili ni jambo ulilotunga wewe na watoa hoja wengine kama
wewe. Nipe andiko ndipo tuanze kujadili hoja hii.
Kama kuna kitu kinachonishangaza katika hoja za Waislamu zinazopinga
mafundisho ya Biblia ni juhudi yao kubwa inayotumika kufundisha mambo ya uongo.
Na hili ni jambo la faida kwa kuwa linauchimbia kaburi Uislamu. Ni suala la
muda tu kisha Uislamu utakuwa ni historia kabisa! Nirudie kusema tena kuwa,
kitu chochote ambacho hakina msingi katika kweli mwisho wake ni anguko
tu! Sababu yake ni kuwa kila anayewaunga mkono anafanya hivyo SI KUTOKANA NA
USAHIHI WA HOJA, BALI KUTOKANA NA KUTOJUA KWAKE. Ile gundi inayowashikilia
pamoja waungaji mkono wa hoja kama hizi ni 'ignorance' yao juu ya kile
wanachoambiwa. Lakini iko siku mtu huyo anapokuja kuijua kweli. Hapo ndipo
anapoachana kabisa na mtoa hoja za aina hiyo.
3. Maalim Moses anauliza: Wakristo
mnaona haya kurejea Torati. Mkirejea mnachagua story kwa mpito tu. Marejeo yenu
yote ni Injili tu au Zaburi kwa vile ibada yenu ni muziki, kuimba na kupiga
makofi (kama mapagani). Je, Jesus wa kihistoria na wanafunzi wake ndio ulikuwa
utaratibu wao wa kuabudu?
Maalim Moses, sisi hatuna woga hata kidogo katika kurejea Torati au Agano
la Kale lote kwa ujumla.
Wakati tunapokuwa shuleni huwa tunafundishwa Jiografia, Hisabati, Kiswahili na kadhalika. Ukishamaliza shule
kisha ukaajiriwa, itakuwa ni ajabu sana kama utaendelea kubeba mfuko wa
madaftari yaleyale na kwenda nayo ofisini. Mtu wa aina hiyo nadhani atakuwa
alishindwa kutambua kusudi la elimu aliyopewa.
Shule si maisha halisi bali ni sehemu ya muda ya maandalizi ya kuingia
kwenye maisha halisi. Ni wazi kuwa elimu tunayopewa shuleni ni chombo tu
ambacho ndani yake kimebeba kile ambacho ndicho hasa tunachotakiwa kwenda nacho
ofisini na katika maisha HALISI – na si kwa lengo la kutufanya tubebe madaftari
yetu ya Historia, Kiingereza na Fizikia maisha yetu yote.
Masomo haya, tunapokuwa shuleni, lengo lake ni kutufundisha mbinu za
kufikiri, kupima, kuchambua, kulinganisha, kutatua matatizo, kubuni njia, na
kadhalika. Hizi ndizo hasa stadi za maisha na si kukariri kuwa Ikweta ni nyuzi
0, oksijeni ikiungana na hidrojeni unapata maji, mtu mzima ana meno 32, n.k. Je,
Katika maisha yako ya kawaida (maisha halisi kazini, kwenye biashara, nyumbani
au kwenye jamii) – ni mara ngapi umetakiwa kutaja masuala ya nyuzi 0 za Ikweta,
meno 32 au oksijeni na hidrojeni? Ni mara ngapi Maalim Moses?
Agano la Kale lilikuja kwa ajili ya kutufundisha kile ambacho tunahitaji
katika maisha HALISI ya kiroho. Kuendelea kuling’ang’ania kama lilivyo hakuna
tofauti na waziri, mkurugenzi, meneja au mfanyabiashara ambaye hadi leo anaenda
ofisini kwake na madaftari yake ya Jiografia na Hisabati aliyojifunza miaka
arobaini iliyopita.
Akifanya hivyo tunajua tu kuwa kumbe kukaa kwake kote shuleni hakuwahi
kujua MAANA HASA ya elimu. Alifikiri kuwa elimu ni kukariri mambo yaleyale
maisha yake yote.
Naomba basi nikupe mifano michache tu ya kile ambacho kiko kwenye Torati na
nikuonyeshe kuwa hadi sasa bado tunakifanya:
- Torati iliagiza kuwa mtu akitenda dhambi, basi anatakiwa apeleke mnyama asiye na waa lolote ili akachinjwe na damu yake imwagike (KWA NIABA YA MTENDA DHAMBI), kisha huyo aliyetenda dhambi anasamehewa dhambi zake. Hata leo sisi bado tunafanya hivyohivyo lakini kwa namna iliyo kamilifu zaidi. Yesu Kristo ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi za ulimwengu. (Yohana 1:29). Kwa hiyo, sisi hatuna haja ya kung’ang’ania madaftari ya Jiografia ya kuchinja mbuzi na kondoo wakati tayari tulishamaliza shule na tuko ofisini ndani ya maisha halisi ya kiroho. Uchinjaji wa wanyama ulikuwa ni mafunzo kwa ajili ya kile ambacho kilikuwa kinasubiriwa. Na sasa kimeshakuja (yaani Yesu), hivyo tunaishi kwenye uhalisia na si kwenye mfano.
- Torati ilikuwa inawataka watu wanawe na kufua nguo zao na kuoga miili yao kwa maji haya kisimani tunayoyafahamu ili waweze kwenda kukutana na Mungu wao. (Kutoka 19:10-11). Hata leo bado tunafanya hivyo, lakini ni kwa namna iliyo halisi na si kwa namna ya mfano iliyokuwapo zamani. Mungu ni roho, dhambi hukaa rohoni, na dhambi husafishwa rohoni. Ukifa, kinachoenda mbinguni ni roho, si mwili, Maalim! Mwili ni kitu kinachoozea ardhini. Sasa, kuoga na kufua nguo ilikuwa ni ISHARA ya utakaso wa kiroho ambao wakati wa Agano la Kale ulikuwa unangojewa. Sasa hivi Yesu alishakuja na alishamwaga damu yake. Hiyo ndiyo inayotakasa roho zetu. Tatizo la mwanadamu si uchafu wa mwili kama vile jasho na harufu mbaya. Tatizo la mwanadamu ni dhambi zilizo rohoni, Maalim Moses! Napenda nikuulize swali ambalo huwa nawauliza Waislamu mbalimbali: JE, MWANAO AKIWA MWIZI AU MWONGO, UTAMPELEKA BAFUNI AKAOGE ILI WIZI WAKE UISHE NA AWE MWEMA? Unafahamu kuwa jibu ni HAPANA! Sasa kwa nini ninyi Waislamu mnadhani kwa kunawa na kuoga MIILI yenu kwamba ndio mtaweza kufaa mbele za Mungu? Amka Maalim Moses! Amkeni! Huko ni kwenda ofisini na daftari la Jiografia rafiki yangu. Mambo hayo yalishapita muda wake. Uhusiano na Mungu si jambo la mwilini. Ni jambo la rohoni. Mifano ni mingi lakini niishie katika hiyo miwili kwa sasa. Kwa kuwa tunaweza kuendelea kujadili suala hili, basi tunaweza kufanya hivyo baadaye. Lakini cha msingi ni kuelewa KANUNI na si kukariri mambo. Torati ilikuja kwa ajili ya mwili kwa lengo la kumwandaa mwanadamu kuishi kiroho.
4. Maalim Moses anauliza: Hushangai kuwa pamoja na Waislamu kupigana
wenyewe kwa wenyewe baada ya mtume kufa hakuna aliyegusa Quran?
Jibu langu:
Jibu la swali hili nilishalitoa kwa ndugu yangu Hamudi. Kwa kifupi nilisema
kuwa si kweli kwamba quran inafanana kote. Maana najua lengo lako unataka
kwenda kwenye hoja ya kwamba Quran ni moja lakini Biblia ina 'version' nyingi.
Kwa hiyo mimi sishangai na sikubaliani na hoja kwenye Quran ni moja.
Ushahidi wa hilo ni kuwapo kwa madhehebu na kuwapo kwa Waislamu wa siasa kali
na wale wa wastani. Hii yote inaonyesha kuwa, hata kama kwa nje quran
inaonekana ni moja, lakini mioyoni mwenu ziko quran nyingi ndiyo maana
mnatofautiana. Na hizo ndizo zinazotenda kazi duniani leo.
Nakukaribisha ufuatilie Sehemu ya Pili ya mjadala huu
ambapo nitaendelea kujibu maswali mengine ambayo Maalim Moses – Mzizimkavu ameuliza.
No comments:
Post a Comment