Wednesday, December 12, 2012

Majibu ya Maalim Moses - Sehemu ya II5. Maalim Moses anasema: Quran ni kitabu pekee duniani ambacho muumini anaweza kukihifadhi kwa moyo. Hamlioni hilo?

Jibu langu:
Ndugu yangu Mzizimkavu, hivi kweli unaweza ukaona fahari na ukajisifia suala la KUKARIRI? Hebu nenda katika taasisi yoyote ya elimu duniani (of course, ukiacha elimu ya Uislamu) – kukariri ni jambo linalopigwa vita. Kukariri hakuna faida yoyote! Kukariri kunamfanya mtu asiwe na tofauti yoyote na roboti au kaseti ambazo ukifungulia zinaanza kutoa tu kile kilichoko ndani ingawa zenyewe hata hazielewi kitu.


Ni bora nikawa na mistari kumi tu ya Biblia MOYONI mwangu ambayo ninaielewa kwa moyo kuliko kuwa na Biblia nzima kwenye AKILI kupitia kukariri ambayo siielewi. SITAKI KUKARIRI! SINA HAJA YA KUKARIRI!


Hebu kuwa mkweli Maalim Moses. Ni Waislamu wangapi WANAELEWA kile ambacho WAMEKIKARIRI? Mahali fulani katika hoja zako umesema kuwa quran imeandikwa kwa lugha ya Kiarabu ambacho kipo hadi leo tofauti na Biblia ambayo imeandikwa kwa Kiaramu ambacho hakipo leo.

Hebu hapa nako uwe muwazi tu. NI JAMBO LINALOELEWEKA wazi kuwa Kiarabu cha quran na kile kinachozungumzwa Uarabuni leo ni lugha mbili tofauti.


Maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa Waislamu WENGI, ikiwa ni pamoja na Waarabu wenyewe, hata hawaelewi maana ya kile ambacho WAMEKARIRI na wewe ndugu yangu Mzizimkavu unatumia jambo hilo kama ni jambo la kujisifia!


Lakini Waislamu wenyewe wanasema nini juu ya KUKARIRI. Video ifuatayo niliiweka kwenye moja ya majibu yangu kwa Hamudi. Lakini si vibaya nikiiweka hapa tena ili huyu mama, ambaye ni Mwislamu, anisaidie kuonyesha jinsi suala hili la KUKARIRI, ambavyo badala ya kuwa baraka, limekuwa ni mzigo mzito kwa Waislamu wenyewe na wala si jambo la kujisifia hata kidogo. Na uzuri ni kwamba, pamoja na mambo mengine anayoongelea, anasisitizia kipekee sana, hususani, juu ya hasara mnazopata kutokana na jambo hilihili la KUKARIRI ambalo wewe unataka tuamini kuwa ni jambo la maana na kwamba eti linaonyesha upekee wa Quran.


6. Maalim Moses anasema: Je, ulikusanya sura zote katika quran ambazo zinaongelea itikadi ya dini yako kisha ukapata jibu la mwisho kwamba quran inakwambia nini? Hukufanya hivyo na hutofanya hivyo kwa woga wa kuukuta ukweli. Nakuwekea changamoto, tuzikusanye kisha tuone ukweli upo wapi. Kisha tuapishane mbele ya Allah (s.w) kwamba anayekataa ukweli laana ya Allah (s.w), malaika zake na walimwengu wote ziwashukie. Hakika huwezi kufanya hili na hutolifanya.

Maalim Moses, nimeshakutana na kila kitu ambacho quran inaniambia, na bado niko tayari kukisikia kutoka kwako. Lakini sina hofu yoyote juu ya hicho unachokiita laana na hata nikiapa kwa vigezo ulivyoweka HAKUNA LOLOTE litakalonifika. Sana sana, nakuhurumia wewe rafiki yangu.


Lakini hata hivyo, sitaapa, si kwa sababu ya kuogopa laana, (maana Bwana Yesu alishanikomboa kutoka kwenye laana zote), bali sitaapa kwa sababu Mungu wangu ananikataza kufanya hivyo. Biblia inasema: Usiape kabisa hata kwa mbingu … wala kwa nchi … wala usiape kwa kichwa chako … Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. (Mathayo 5:33-37).


Kwa hiyo, nakukaribisha tu unifafanulie mambo hayo ambayo unasema kuwa quran inaniambia kuhusu itikadi ya dini yangu nami siogopi hata kidogo kuupata UKWELI kama uko humo – maana maishani mwangu, kuitafuta KWELI ndilo jambo la muhimu kuliko mambo yote.


7. Maalim Moses anasema: Lugha nyingi zimekufa. Je, kama Kiaramu kilikufa, wafuasi wa Jesus (pamoja na Paulo) walitumia lugha gani? Unadhani Paulo alikijua Kiaramu sawasawa mpaka afikishe mradi wa Injili ya Jesus kama Jesus mwenyewe alivyohubiri katika lugha ya Kiaramu?


Jibu langu:

Kila unapotaja "Jesus" unanikumbusha marehemu shekhe Yahaya. Hata siku moja alikuwa hawezi kusema "Yesu". Siku zote alitaja "Jesus" hata kama anazungumza Kiswahili. Naliona hili na kwako pia Maalim Moses. Hivi ni kwa nini unaogopa kusema Yesu? Kuna kitu gani hapo?


Turudi kwenye hoja ya lugha. Ni kweli Yesu alitumia Kiaramu. Lakini unapouliza kama mitume walitumia lugha hiyo kwa usahihi, huenda unasahau kuwa mitume waliishi na Yesu. Kwa hiyo, kama Yesu alizungumza Kiaramu, basi na wao walikizungumza pia. Isigewezekana Yesu aondoke leo kurudi mbinguni, halafu kesho yake mitume wasahau lugha aliyotumia.


Labda mtu anaweza kuuliza kuhusu Paulo, maana yeye aliingia kwenye huduma ya Injili miaka takribani 60 baadaye. Lakini hata huu nao si muda mrefu wa kutosha lugha kufa – maana lugha haifi vup! kama mwanadamu.

Lakini hata hivyo, ni kitu gani kinachokufanya udhanie kuwa Injili ya kweli ni lazima ifikishwe kwa watu kwa lugha ya Kiaramu? Rafiki yangu, Biblia inasema kuwa “andiko huua, bali roho huhuisha” (2 Wakorintho 3:6).


Ni mambo hayohayo ya kuzuia watu kutafsiri maneno ya Mungu katika lugha zingine ndiyo yanayowanyima watu nafasi ya kumjua Mungu wa kweli. Kile kilichomo kwenye karatasi ni andiko. Lakini kile kinachowakilishwa na andiko hilo ni roho. Mwanadamu hahitaji andiko anahitaji roho.


Je, mtu akikuandikia barua akakwambia kwa Kiswahili  NAKUPENDA, kipi ni muhimu kwako? Je, ni hiyo mikwaruzo ya wino kwenye karatasi au kile kilicho kwenye moyo wa mwandishi ambacho kinawakilishwa na mikwaruzo iliyo kwenye karatasi hiyo? Mimi nakwambia ni kile kilichomo moyoni. Sasa, kama ni kile kilichomo moyoni, je, ni lazima kisemwe kwa Kiswahili ndipo kiwe cha kweli? Kung’ang’ania kuwa ni lazima kiandikwe kwa Kiswahili ni kung’ang’ania ANDIKO.


Ukilijua hili, hutakuwa na haja ya kugombana na mtu ambaye atachoma moto kitabu cha dini yako. Maana utajua kuwa alichochoma ni andiko na si roho. Andiko huua bali roho huhuisha!


Kwani katika mfano niliokupa hapo juu wa kuandikiwa NAKUPENDA, kama atatokea mtu mwingine akachoma moto karatasi hiyo, je, atakuwa amechoma na ule upendo moyoni mwa mtu aliyekuandikia? Kila mtu anajua kuwa jibu ni HAPANA.


Kwa hiyo rafiki yangu Mzizimkavu, Kiaramu ni lugha tu kama lugha nyingine ambayo haifanyi Injili iwe na nguvu zaidi ya Kiswahili. Cha msingi si andiko. Cha msingi ni roho.


Na cha msingi zaidi ni kuwa, lugha zinaweza kufa lakini Mwandishi wa Injili na Biblia yote yu hai milele. Alikuwapo wakati wa Musa; alikuwapo wakati wa Paulo; na yupo hata sasa. Huyu ni Roho Mtakatifu wa kweli atokaye kwa Baba mbinguni.


Adui alijaribu kutumia mbinu hii mara tu baada ya Bwana Yesu kuondoka. Kanisa Katoliki lilikuwa linazuia Biblia kutafsiriwa kwa lugha za watu. Hata ibada nazo zilikuwa zikiendeshwa Kilatini. Na hata watu wachache waliojitolea kutafsiri Biblia kwa lugha za watu walipigwa vita na wengine hata kuuawa. Yote hii lengo lake ni moja - ILI WATU WAISHIE KUKARIRI KILE WASICHOKIELEWA; WAISHIE KUNG'ANG'ANIA ANDIKO BADALA YA ROHO. Lakini Bwana wetu alimkemea adui kwa sababu haikuwa kusudi la Bwana Injili ibakie kuwa andiko. Ndiyo maana leo Injili au Biblia inapatikana katika lugha hata za makabila madogo kabisa usiyoyatarajia. Na hiyo SI hasara kama unavyotaka kutuaminisha bali NI faida sana sana!


8. Maalim Moses anasema: Itikadi yenu inayojenga mnayoamini ni batili, batili, batili!!!! Ulisema kuwa Mungu wa kweli ni mkamilifu kwa asilimia mia moja. Je, ni Mungu gani huyu unayemkusudia hapa? Ni Mungu BABA, Mungu mama (Maria), Mungu mtoto (Jesus) au Mungu Roho Mtakatifu, au Mungu wote hao wanne hatimaye wanageuka kuwa Mungu mmoja?!!


Jibu langu:

Swali hili nimeshalijibu. Lakini kwa kifupi ni kuwa, kwanza, Biblia haisemi popote kwamba Maria ni Mungu. Hilo ni jambo ambalo ninyi wajenzi wa hoja wa Kiislamu mmeanzisha ili kuwanasa watu wasiotaka kujisumbua kutafuta ukweli wa mambo.


Kuhusu Mungu gani ninayemmaanisha, ni Mungu MMOJA muumba mbingu na nchi kama Biblia inavyosema. Hili nalo nimeshaliongelea kuwa Ukristo unaamini katika Mungu MMOJA TU.


9. Maalim Moses anasema: Ninyi mnaamini kuwa Mungu Baba alijiona mpweke akatafuta mke (Maria). Baadaye walishauriana wazae mtoto. Hata hivyo wakaona bado wanahitaji msaidizi wa kusaidia kulea mtoto na wakamleta Roho Mtakatifu ….


Jibu langu:

[Hoja kama hizi nazipenda sana. Hoja hizi wala si ngeni miongoni mwa wachambuzi wa Biblia wa Kiislamu mahali popote. Uzuri wa hoja hizi au kuzipenda kwangu ni kwa sababu: msingi wake ni uongo; ni mambo ya kutunga ambayo kwenye Biblia hata hayapo. Ukisoma kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo huyakuti.


Sasa kwa vile wafuasi wa hoja hizi huzishikilia kiushabiki tu, jambo moja ni dhahiri – pale wanapokuja kugundua kuwa kumbe Maalim Moses alikuwa anatuambia mambo ambayo hata hayapo kwenye kitabu cha Wakristo, hapo ndipo wanaanza kuhoji mambo kimantiki badala ya kishabiki. Watajiuliza, "Kama ameweza kutudanganya katika hili, ni mangapi mengine ametudanganya?"


Kila mmoja atasema, “Yaani siku zote nilidhani hivyo ndivyo Biblia inavyosema kumbe si kweli!” Matokeo yake nini? Matokeo yake watapeleleza ukweli zaidi na kugundua kile ambacho Mwokozi wao aliyewafia msalabani, yaani Yesu Kristo, anachosema.


Kwa hiyo rafiki yangu Maalim Moses – Mzizimkavu, mimi nafurahi kwelikweli unapoleta hoja za mtindo huu – ambazo hazina kamwe ukweli wala hazitokani kamwe na Biblia bali ni mawazo yenu tu. Basi onyesha japo ushahidi wa kihistoria juu ya haya usemayo kama upo ili tupate msingi wa kujadiliana kwa namna iliyo 'serious'. Maana hapa ni kama tunapoteza tu muda.


Sasa hebu nije basi kwenye hiyo hoja yako ya Mungu kuwa na mke, Maria kuwa Mungu, ... n.k., nk.


Kimsingi unachofanya hapa ni kutumia tu ‘emotive language’ badala ya ‘factual language.’ Yaani unatumia lugha kwa lengo la kuamsha hisia za wale wanaokuunga mkono badala ya kuamsha ujenzi wa hoja na mantiki. Hii ni kwa sababu hisia huwa ni rahisi kuwashwa moto na hazihitaji kutafakari mambo.


Mungu hana mke na wala Maria si Mungu. Jambo jingine ni kuwa, mbingu ambayo wafuasi wa Yesu wanaenda (yaani aliko Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo) ni tofauti na mbingu ya Allah.


Kwenye mbingu ya Allah watu wanaoa na kuolewa (tazama Sura Al-Baqara 2:25). Lakini Bwana Yesu anasema hivi: Mwapotea kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. (Mathayo 22:29-30).

Ndugu, mbinguni hakuna kitu kama wanaume kupewa wanawake wenye macho makubwa kama vikombe rafiki (sijui wanawake nao watapewa nini?). Mungu hahitaji mke. Neno lake linatosha kuleta kile anachokihitaji kwa njia anayoichagua Yeye.


10. Maalim Moses anasema: Je, ni kweli kwamba wanadamu wamerithi dhambi ya asili toka kwa mwanadamu wa kwanza na mkewe?


Jibu langu:

Ndugu Mzizimkavu, hivi unaelewa nini kuhusiana na dhambi? Dhambi ni nini? Na je, tunaposema kuwa Mungu ni MTAKATIFU unaelewa nini kuhusiana na hilo?


Najua Mungu wako amekupa ruhusa ya kufanya dhambi anazoziita kuwa ni "ndogondogo", maana anasema katika sura 53:32, To those who avoid the grossest sins and indecencies and commit only small offences, Allah is of vast forgiveness.


Yaani: Kwa wake wanaojizuia kutenda dhambi kubwakubwa kabisa ila wakafanya dhambi ndogondogo tu, Allah ni mwingi wa msamaha.

Hili ni jambo ka kushangaza kwelikweli! Sijui dhambi ndogondogo ni zipi? Licha ya kwamba dhambi ni dhambi tu, lakini vilevile ukimruhusu mwanadamu kufanya dhambi ndogondogo, KAMWE hawezi kuishia hapo! Ni lazima atasonga mbele zaidi. Nirudie kusema tena – Adamu na Hawa walifukuzwa kwa kutenda dhambi MOJA. Iweje leo Mungu huyohuyo aruhusu wanadamu wengine watende dhambi nyingi ndogondogo?


Lakini ngoja nikuambie kile ambacho Mungu wangu anasema.
Imeandikwa kwenye Biblia: Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake (1 John 1:5).


Pia, Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. (Walawi 20:7).


Pia, Ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. (Mathayo 5:48) - kama Mungu ni mkamilifu, unadhani hii ina maana ya kuwa hafanyi dhambi kubwakubwa lakini anaweza kufanya "dhambi ndogondogo"?


Vilevile, kuhusiana na mji ambao watakatifu watakaa baada ya dunia hii kufikia mwisho, imeandikwa kwamba: Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27).


Sasa, unafikiri Adamu alipoumbwa na Mungu alikuwa mtakatifu au hakuwa hivyo? Kama alikuwa mtakatifu, unadhani alikuwa na tabia kama tulizonazo sisi - yaani za uongo, wivu, hasira, uvivu, n.k.?


Endapo alikuwa kama sisi, basi sisi kwa jinsi tulivyo sasa ni watakatifu na tunastahili kuingia mbinguni. Lakini kama sisi hatustahili kuingia mbinguni kutokana na uovu wetu, basi Adamu na Eva hawakuwa kama sisi wakati ule walipoumbwa.


Lakini pale walipomsikiliza ibilisi ndipo waliporuhusu dhambi kuingia ndani yao, ndani ya ulimwenguni, na ndani ya uzao wao, yaani sisi. Dhambi, ndugu yangu Maalim Moses, ni jambo au tabia YOYOTE iliyo kinyume na utakatifu wa Mungu.


Mungu ninayemwamini mimi, ambaye aliumba mbingu na nchi na kila kitu ni mtakatifu na mkamilifu kwa asilimia mia moja. Yeye haruhusu kwenye mbingu zake zilizo takatifu kama Yeye, dhambi YOYOTE iingie humo - hata kama ni zile ambazo Mungu wako wewe anaziita ni ndogondogo. Hapana!


Kwa hiyo, ni kweli kabisa kwamba kutokana na uasi wa Adamu na Eva, sisi tulio uzao wao, tumezaliwa na asili ambayo siku zote inapingana na utakatifu wa Mungu, yaani tuna asili ya dhambi.


Kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kuwa, NI KWELI SISI TUMERITHI ASILI YA KUTENDA DHAMBI kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza, yaani Adamu na Eva. Ili ujue kama sisi ni wenye dhambi ni lazima kwanza ujue maana ya UTAKATIFU. Huwezi kujua maana ya uchafu kama hujui kuwa safi maana yake ni nini. Mungu alileta Torati ili tuweze kuiona na kuitambua asili hiyo, kisha tuchukue hatua ya kukubali kutakaswa na Yeye kwa njia ya damu ya Yesu Kristo.

5 comments:

 1. "Quote"
  Majibu ya Maalim Moses - Sehemu ya II


  5. Maalim Moses anasema: Quran ni kitabu pekee duniani ambacho muumini anaweza kukihifadhi kwa moyo. Hamlioni hilo?

  Jibu langu:
  Ndugu yangu Mzizimkavu, hivi kweli unaweza ukaona fahari na ukajisifia suala la KUKARIRI? Hebu nenda katika taasisi yoyote ya elimu duniani (of course, ukiacha elimu ya Uislamu) – kukariri ni jambo linalopigwa vita. Kukariri hakuna faida yoyote! Kukariri kunamfanya mtu asiwe na tofauti yoyote na roboti au kaseti ambazo ukifungulia zinaanza kutoa tu kile kilichoko ndani ingawa zenyewe hata hazielewi kitu.

  Brother,
  KUKARIRI HAKUNA FAIDA?
  haya hiyo computer unayoitumia inafanya Lipi jipy ila ni KUKARIR
  naomba uangalie vyema baina a Kuhifadhi na Kukarir
  asante.

  ReplyDelete
 2. JIBU KUTOKA KWA ABJAD

  Brother,
  KUKARIRI HAKUNA FAIDA?
  haya hiyo computer unayoitumia inafanya Lipi jipy ila ni KUKARIR
  naomba uangalie vyema baina a Kuhifadhi na Kukarir
  asante.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Salim, basi bora hata kukariri kuliko kuhifadhi. Kukariri angalau unakuwa uko active lakini kuhifadhi unakuwa domant. Ila sasa, iwe ni kukariri au kuhifadhi, kwa kweli bado KUELEWA machache ni bora zaidi kuliko ama kukariri au kuhifadhi mengi.

   Delete
 3. Dini inayomfundisha mtu auwe wengine kisa sio waumini wa dini hiyo ujue hiyo dini ni ya kishetani. Mungu wa kweli hawezi kumuumba mtu kisha akamwambia mwingine amuangamize. Angeamua kuviangamiza vizazi vyote vya hao wanaoitwa kafir bila hata mkono wa bin adam. Dini ya kiislam ni nzuri. inahitaji kujirekebisha kidogo tu na kuwa ya kibin adam maana yote yaliyo andikwa hayafai kufuata, yamejaa umwagaji damu kwa wasio waislam.Tena ukifanya hivyo ndio unaenda peoponi kwa kuwa unaitetea dini(Jihad)!! Dini gani inayofundisha chuki na uhasama?? Utamshauri vipi asiye muislam aione imani ya kiislam kuwa nzuri? Achana na maneno mengine yaliyo jaa uongo kwenye quran tukufu, katika hali ya kwaida ya kibin adam uislam unahitaji kuona mabadiliko ya dunia maana unaendana na miaka mingi ya nyuma hasa kipindi cha utumwa ambapo watu mtume pia alikuwa akifanya biashara hiyo kama ilivyoandikwa kwenye khadith za bukhari. Uislamu ukiacha chuki na ubaguzi sitakuwa na sababu ya kuiheshimu kama dini ya mwenyez mungu subhanna wa taallah!!!

  ReplyDelete
  Replies
  1. Nashukuru rafiki kwa kutembelea blog hii na kwa kutoa maoni yako. Biblia inasema kuwa hakuna mtu anayeweza kusema Yesu ni Bwana isipokuwa kwa Roho Mtakatifu (1 Wakor 12:3). Tuzidi kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie wanadamu wenzetu ili wamjue Bwana wa amani, furaha, upendo, uvumilivu na wokovu. Ni Yeye peke yake ndiye mwenye uwezo wa kumfanya mtu akawa na mtazamo tofauti kabisa na aliokuwa nao mwanzoni. Ubarikiwe.

   Delete