Saturday, December 8, 2012

Je, Walikuwa Binadamu Kama Sisi?




Tunasoma katika maandiko juu ya mambo makubwa yaliyofanywa na watu wa nyakati za Biblia. Mambo hayo yalimfurahisha Mungu kiasi kwamba walioyatenda ilibidi Roho Mtakatifu ayaandike kwenye Biblia. Tunapoyasoma mambo hayo tunatiwa changamoto kiasi kwamba wakati mwingine tunajiona labda sisi ni wa hali ya chini sana na huenda Mungu hatufurahii. Mambo hayo ni pamoja na yafuatayo:


  • Ibrahimu anaitwa baba wa imani na rafiki wa Mungu (Yak 2:23). 
  • Daudi alimwua Goliathi na pia anaitwa mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu (Mdo 13:22). 
  •  Nuhu alijenga safina na alipata rehema kwa Mungu (Mwa 5:13-22). 
  • Samsoni alipigana na maelfu ya Wafilisti peke yake na kuwashinda kwa ajili ya Israeli (Amu 15:15). 
  •  Musa aligawa bahari ya Shamu na Israeli wakapita salama (Kut. 14:21-22). 
  • Elia aliomba mtoto mfu akafufuka (1Fal 17:23); aliomba mvua ikaacha kunyesha miaka mitatu na baadaye akaomba ikanyesha (1Fal:17:1); aliomba moto ukashuka toka mbinguni na kuwateketeka askari waliotumwa kumkamata (2Fal 1:10); aliomba moto ukashuka na kulamba sadaka ya kuteketezwa pamoja na mawe na mavumbi ya madhabahu (1Fal 17:38). 
  •   Elisha kwa imani alifanya shoka lililokuwa limetumbukia mtoni lielee (2Fal 6:6); aliomba na jeshi la askari lililokuwa limetumwa kumkamata likapigwa upofu (2 Fal 6:18).

Swali moja muhiumu la kujiuliza ni kwamba, je, watumishi hawa walikuwa ni wanadamu kama mimi na wewe au Mungu aliwapa kitu cha ziada katika ubinadamu wao?


Niseme moja kwa moja kuwa jawabu ni kwamba, hawa walikuwa ni wanadamu kama sisi kabisa. Walikuwa na upungufu kama sisi tulivyo na upungufu mwingi. Walitakiwa kutimiza kanuni zilezile za kiroho ambazo hata sisi wa leo tunatakiwa kuzitimiza ili tuweze kuishi katika ushindi wa kiroho.


Bwana Yesu alisema ... sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi. (Mathayo 9:13).


Mungu hahitaji wanadamu wakamilifu anapotafuta mtu wa kumtumia katika kazi yake. Kwa nini? Kwa sababu hakuna mwanadamu hata mmoja wa namna hiyo: Wote wamepotoka, wameoza wote pia; hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. (Warumi 3:12). Hii ni pamoja na Musa, Daudi, Elia, Elisha, na wewe na mimi, n.k.


Watu hawa wakubwa katika historia ya wokovu, walikuwa na upungufu mbalimbali kama ilivyo kwako na kwangu leo. Walijaribiwa, walianguka, walitubu, walisimama na wakasonga mbele.

  •  Je, Ibrahimu hakusema kwa Wamisri kuwa Sara alikuwa dada yake na si mke wake? (Mwa. 12:10-20). Pia alifanya hivyo hivyo kwa mfalme Abimeleki (Mwa. 20:5). Je, si hofu ndiyo iliyomfanya aseme hivyo? Na hofu si ni dhambi? Uongo pia nao si ni dhambi? Iweje basi aitwe ni baba wa imani wakati naye alifanya makosa yaliyo kinyume na imani?

  •  Je, Daudi hakumwua Uria kwa sababu ya kumtamani mke wa Uria, na hatimaye akamwoa mwanamke huyo, yaani Bethsheba? (2 Sam 11:14-17). Iweje Mungu aseme kuwa Daudi alikuwa ni mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu?

  •  Je, Musa hakumwua Mmisri na kumficha mchangani? (Kutoka 2:11-12). Je, si yeye aliyekuwa anaogopa kwenda kwa Farao hadi Mungu akakasirika? (Kutoka 4:14). Si Musa aliyelia baada ya kuona Bahari ya Shamu iko mbele na jeshi la Farao linakuja nyuma hadi Mungu akamwambia 'Unanililia nini?'? (Kutoka 14:15). Je, hizi si ni tabia za kibinadamu kama tulizonazo sisi?

  •   Tusemeje kuhusu Petro - mtume mkuu? Alipoenda kwa Paulo alikula pamoja na watu wa mataifa. Lakini walipokuja Wayahudi, alijitenga na watu aliokuwa anakula nao kabla ya hapo. Je, huu si unafiki ambao hata maandiko yanaita ni dhambi? Hata Paulo naye anakiri hilo kwa kusema: Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu ... Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawa na kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi? (Wagalatia 2:11, 14).

  • Vipi kuhusu shujaa wa imani na vita vya kiroho Paulo; mtu mwenye mafunuo makuu? Baada ya Marko kuwaacha wakati fulani walipokuwa Pamfilia, siku nyingine Paulo aligoma kuandamana naye.Imeandikwa: Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko ... Paulo akamchagua Sila ... (Matendo 15:39-40). Je, Bwana hasemi kuwa tusameheane? Je, huku ndiko kusamehe?

  •  Yakobo, je? Mungu wetu anaitwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Je, ni Yakobo huyuhuyu aliyesema uongo kwa baba yake kuwa "Mimi ni Esau" (Mwanzo 27:19) hadi akatwaa mbaraka wa Esau kwa njia hiyo? Jibu ni ndiyo.

  • Je, Bwana Yesu hatoki kwenye ukoo wa Daudi? Biblia kwa kiasi kikubwa imeandikwa upande wa kuumeni na si wa kikeni. Hata zinapotajwa koo - fulani alimzaa fulani ... n.k., kwa kawaida wanatajwa wazazi wa kiume. Na hata watoto nao mara nyingi ni wa kiume. Kwa mfano, unadhani Adamu na Hawa walikuwa na watoto wa kiume tu? Sidhani hivyo! Naamini walikuwa pia na watoto wa kike.

Sasa, Daudi alizaliwa na Yese; Yese na Obedi; Obedi na Boazi; Boazi na Nashoni. Kisha Biblia inaongeza kusema kuwa 'kwa Rahabu'! Rahabu? Yupi huyo? Ni yule kahaba wa Yeriko! (Yoshua 2:1).


Kwa hiyo, katika ukoo wa Yesu kulikuwa na makahaba pia? Bila shaka! Tena Biblia imeacha kabisa kutaja wake wengine katika ukoo huo ikamtaja huyu Rahabu ambaye, licha ya kuwa alikuwa kahaba, lakini pia wala hakuwa Myahudi.


Katika watu hawa mbalimbali, tunaona tabia ambazo Biblia inazibainisha wazi kuwa ni dhambi na wazitendao hao mwisho wao ni katika jehanamu ya moto. Kwa nini basi Roho Mtakatifu hakukaa tu kimya kuhusiana nazo? Maana ni wazi kuwa tabia hizi ziko kinyume na utakatifu wa Mungu. Lakini badala yake tunaona kuwa aliruhusu ziingie kwenye Biblia.


Labda wewe umekuwa unawaza, "Mbona kila nikijitahidi kuacha dhambi hii naanguka tena na tena?"  Matokeo yake umekuwa unajisikia aibu na hatia kubwa mbele za Mungu na hofu ya jehanamu imekuwa inakutafuna kila wakati. Shetani amepata mwanya wa kukufanya unyong'onyee sana kiasi cha kutoona furaha ya maisha ndani ya Yesu.


Ndugu, sababu kubwa ni hiyohiyo, KUJITAHIDI! Tunapojaribu KUJITAHIDI kuacha dhambi tutaishia tu kuishi maisha yaliyojaa hatia na hofu nyingi. Kama tulivyoona kwenye mifano mbalimbali hapo juu, watu wote ambao Mungu amewapa sifa katika Biblia si kwamba wao walikuwa wakamilifu zaidi ya sisi. walikuwa ni wanadamu kama sisi kabisa.


Huko kujiona kwako kwamba umepunguka mbele za Mungu si tatizo. Huo ndio ubinadamu kabisa. Jambo la maana ni kutambua kuwa Mungu hana haja kamwe na jitihada zetu za kujisafisha, maana imeandikwa: Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipaka sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. (Yeremia 2:22).


Jitihada pekee ambayo Mungu anaitazamia kutoka kwetu ni hii: kumwamini Yesu (Yohana 6:29), kumtwika fadhaa zetu (Mathayo 11:28), kuungama dhambi zetu (Mathayo 4:17) na kuamini kuwa atafanya.


Mungu anatafuta watu ambao hawatafuti haki yao wenyewe, yaani wale ambao wanadhani wanaweza kuwa na wema wa kutosha kiwango anachokitaka Mungu. Badala yake,  anawatafuta wale wanaoitafuta haki ya Mungu (Mathayo 6:33). Huyu ni mtu anayesema, "Nimekosa; Siwezi; Nisaidie; Niwezeshe." Kisha anaiamini na kuikubali kazi ya Yesu aliyoifanya msalabani kwa ajili yake. Halafu anaamini kuwa kazi hiyo itamkamilisha kabisa.


Matokeo ya unyenyekevu huu: ... na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. (1 Yohana 2:7).


Na Roho Mtakatifu wa Mungu: ...ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa. (Warumi 8:11).


Kumbuka sijasema kuwa, Mungu anawatafuta wale wanaosema kuwa, "Acha nitende dhambi tu. Si Bwana atanisaidia kushinda?" Dhambi inapotokea, kinachotakiwa ni kuitubia na si kuitetea.


Bwana Yesu anasema: Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayeipoteza nafsi yake kwa jili yangu, ataiona. (Mathayo 16:25). Tunaponyenyekea na kumwamini Bwana na kumwachia kazi ya kutuokoa, Yeye sasa anashughulika na ile mizizi yenyewe na dhambi. Kwa asili sisi ni wenye dhambi. Kushindana na asili ni jambo gumu sana kwa mwanadamu - hasa hiyo asili ya dhambi.


Ndiyo maana Bwana anauliza, Je, Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya. (Yeremia 13:23). Jibu ni kuwa: Haiwezekani!


Shetani asitumie udhaifu wako kana kwamba ni jambo geni kukunyanyasa na kukufanya ushindwe kusonga mbele na wokovu. Ukishamkabidhi Bwana maisha yako, Yeye anaanza kazi mara moja ndani yako. Na Biblia inasema kuwa tumtazame: Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu (Waebrania 12:2). Maana anasema pia, Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote (Yohana 15:5).


Hakika Mungu hatafuti wakamilifu bali anatafuta watu walio tayari kutambua na kukiri kuwa wao ni wenye dhambi; wamepungukiwa na hawawezi kuwa na jambo linalowastahilisha mbele za Mungu. Ni Mungu mwenyewe ndiye anayewapa wanadamu haki yake, anawawezesha na kuwainua pale wanadamu wanapojinyenyekeza kwake. Kwa ufupi ni kuwa, mwanadamu anapojinyenyekeza mbele za Mungu, ni Mungu ndiye anayetenda kazi hizi kubwakubwa kupitia wao.

1 comment: