Katika kukua kwangu, mara
zote nilimwona Mungu kama yuko mbali sana. Nilikuwa nikimuogopa sana. Na nilikuwa
nikijaribu kumpendeza kwa matendo yangu yote, huku nikijitahidi kubakia safi
kulingana na mafundisho niliyopokea, nikiwa kama mwislamu wa kishia.
Nilikuwa nikijitahidi
kufanya zile swala 5 kwa siku, huku nikigeukia kwenye Ka’aba, Makka. Pamoja na
matendo yangu haya mazuri, nilikuwa sina uhakika ni wapi nitakwenda baada ya
maisha haya.
Na tena, kwa sababu ya
vita na hali ilivyokuwa nchini, nikiwa nimezaliwa wakati wa mapinduzi na kuona
vijana hawa wote waliouawa, nilianza kumhoji Mungu. “Hivi wewe kweli upo ilhali
haya yote yanatokea?” Na mara zote mama yangu alikuwa akiniambia, “Nyamaza. Utakwenda
motoni. Hutakiwi kumhoji Mungu!”
Kwa hiyo, nilikuwa
nikisoma Quran. Kilichokuwa kinanishangaza ni kuwa, nilijifunza kuwa Allah ana
majina 99 – kwamba yeye ni Muweza, ni hivi, ni vile; lakini hakuna hata jina
moja linalomaanisha upendo!
Kulikuwa na mikanganyiko
mingi; maswali mengi na nikawa natafuta kweli halisi. Na hofu kubwa niliyokuwa
nayo ni kuwa, kama nikimkataa huyu Allah, ataniadhibu na nitaishia kwenye moto.
Nilikuwa nikisema tu, “Inshallah, nitakwenda peponi.”
Maana yake kwamba, “Mungu
akipenda, nitaenda mbinguni.” Inakatisha sana tamaa kujua kuwa unaishi kwenye
maisha haya bila hasa kuyaishi.
Baadaye nilienda chuo
kikuu. Niliona tangazo kwenye ubao kwamba wataonyesha sinema ya Yesu. Kutokana
tu na shauku na udadisi, nikasema, “Alikuwa ni nabii mzuri, alitenda miujiza
mingi. Nabii niliyekuwa nikimwamini wakati ule hakuwahi kufanya miujiza yoyote,
hivyo acha tu nikaangalie sinema hii. Kwani nitapoteza kitu gani?”
Nilienda na kwa mara ya
kwanza nilikutana na Waislamu waliobadili dini na kuwa Wakristo. Walikuwa ni
madaktari, wengine walikuwa mahaji (waliwahi kwenda kuhiji). Kwa hiyo nilikuwa
nasema, ni kitu gani kiliwafanya wamwamini Yesu, si kama nabii mkuu tu, bali
kama Mwana wa Mungu; kama Mwokozi wa ulimwengu?
Baada ya kutazama sinema
hii, nilianza tena kuhoji mafundisho ya Quran. Maana niliona kwenye sinema ile kwamba
Yesu alisulubiwa; alienda msalabani kwa ajili yetu wenye dhambi, kisha
akafufuka kutoka kwa wafu siku tatu baadaye na kaburi lake ni tupu!
Hii haikuwa ni namna
ambayo nilijifunza kuhusu Yesu; na jinsi alivyozaliwa; alizaliwa Bethlehemu. Quran
ilinifundisha kuwa alizaliwa kwenye sehemu tu ya jangwa jangwa. Kulikuwa na mambo
mengi yaliyokuwa yanakanganya.
Baada ya kutazama sinema
hii walikuja kwangu wakaanza kuongea, na kidogo kidogo nilianza kubishana nao. Kwa
namna fulani nilijua kuwa walichokuwa wakisema ni kweli, lakini kutokana na ile
roho ya hofu iliyokuwa imenikamata, sikuweza kukubaliana nao. Hasa pale
waliposema kuwa sisi sote ni wenye dhambi. Nilisema, “Hapana. Mimi sijatenda
dhambi yoyote, uzinzi, ulevi au chochote.”
Nilikuwa naogopa sana
kutokana na mafundisho ya Quran niliyofundishwa kwamba tukiukataa Uislamu,
tutakwenda motoni. Kwa hiyo niliwaambia, “Mtakwenda motoni.” Nilijaribu kuwashawishi
warudi tena kwenye Uislamu, lakini bado walinionyesha upendo. Hilo kwa kweli
lilikuwa ni jambo kubwa sana lililogusa moyo wangu. Na kwa mara ya kwanza maishani
mwangu niliona Biblia – Agano Jipya.
Na kulingana na tena na
mafundisho niliyokuwa nayo, Biblia ni kitabu kilichobadilishwa. Na kutokana na
ile shauku ya kutaka kujua ni sehemu gani hizo ambazo zimebadilishwa, nilianza
kusoma na kujifunza Biblia.
Na kwa mshangao mkubwa, si
tu kwamba sikuona kujikanganya kwa aina yoyote, au kubadilishwa kokote, lakini nikuwa
naona tu uthibitisho wa pendo la Mungu kuanzia mwanzo hadi sura ya mwisho!
Siku moja, nilikuwa
nimepiga magoti; na nikasema, “Mungu, kwa kweli sitaki kwenda motoni. Kama wewe
ni huyu ambaye hawa marafiki wananieleza, tafadhali jidhihirishe! Tafadhali jionyeshe
kwangu!”
Na kwa neema kuu ya Mungu,
alinitokea kwenye ndoto. Usiku ule, katika ndoto hiyo niliyoota, wanaume watatu
waliovaa mavazi meupe, na kandambili za Kirumi; zenye umbo la pembetatu,
walisimama mbele yangu. Sikuweza kuona nyuso za wawili kati yao. Lakini yule
aliyesimama mbele yangu, alijibu maswali yangu. Maswali ambayo nilienda kulala
nayo.
Alisema, “Kwa nini una
mashaka sana na mimi, wewe niamini tu.”
Niliamka. Sikuwahi kukutana
na Mungu kwa karibu namna ile! Sikuwahi kuzungumza na Mungu kibinafsi namna
ile! Maana kwangu mimi, Allah alikuwa mbali sana, juu sana nisikoweza kufika. Ndiyo
maana ilikuwa inabidi upitie kwa maimamu au watu wa kati ili kuomba hata sala
rahisi tu.
Na nilipoamka, kwa mara ya
kwanza amani ilikuja ndani yangu; maana nilijua kuwa ndani yetu kuna utupu au
uwazi fulani ambao ni Muumba wetu tu ndiye anayeweza kuuziba.
Kwa hiyo, nilipoamka
(asubuhi) naelekea chuoni, ndoto hii ilikuwa kama sinema mbele ya macho yangu. Nilimwita
yule dada aliyewahi kwenda kuhiji, nikamwambia, “Nimeota hivi na hivi.” Akasema,
“Hatuwezi kuona uso wa Baba au wa Roho Mtakatifu. Lakini kwa imani tu kama Yesu
anavyosema, “Kama ukikiri kwamba wewe ni mwenye dhambi na ukanipa maisha yako;
na ukaamini kuwa nilikuja kwa ajili yako; kwamba mimi ni Mungu; nilikufa
msalabani kwa ajili yako na kwa ajili ya dhambi zako; nilifanyika dhambi kwa
ajili yako; nilimwaga damu yangu ili kukusafisha na uchafu huu wote; na
nikafufuka tena siku tatu baadaye; umeokoka.”
Kwa hiyo, ni kwa imani tu.
Japokuwa nilikuwa bado nahoji kama Yesu ni Mungu; ni Mwana wa Mungu; maana
nilikuwa bado nina mawazo ya kimwili juu ya Yesu kuwa Mwana wa Mungu akilini
mwangu.
Niliomba sala hii kwa
imani tu na baada ya kumaliza, nilijihisi kama unyoya kwenye hewa. Nilijisikia mwepesi
mno! Ilikuwa ni kama mizigo mizito inaondolewa kutoka kwangu!
Na wakati fulani nilisoma
Biblia tena kwenye sura ya kwanza ya kitabu cha Yohana kabla ya kunjua Bwana na
kumkiri kama Bwana na Mwokozi wangu. Nilisoma Biblia na sikuwa na Roho wa
Bwana. Kama Roho wa Mungu asipokufunulia kuwa Yesu ni Bwana, hakuna jinsi.
Nilisoma aya ya kwanza:
Hapo mwanzo kulikuwako na Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno
alikuwa Mungu. Na sauti ya wazi kabisa kama ninavyoongea na kusikia sauti yangu
sasa hivi ndani yangu ilisema, “Angalia aya ya kumi na nne.”
Nilitazama aya ya 14 na
inasema: Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.
Mara moja lile giza
liliondoka machoni mwangu! Na kwa mara ya kwanza maishani mwangu nilikiri kwa
moyo wangu wote kwamba Yesu ni Bwana. Na hakuna jina jingine humu duniani;
chini ya mbingu hizi tunaloweza kuokolewa kwalo, bali ni jina la Yesu!
Yesu Kristo ni Mwokozi
wangu; wako; na wa ulimwengu! Niwaambie kaka na dada zangu kwamba, mikono ya
Mungu aliyetuumba; aliyejibadili na kuvaa mwli, na kusema, Niko hapa; ninakukubali
hivyo hivyo ulivyo. Huna haja ya kuniridhisha mimi kwa matendo yako mema ili
upate uzima wa milele. Nakukubali hivyo hivyo ulivyo, na mikono yangu ni mikuu
sana na imenyooshwa kukuelekea ili kukupokea kwa upendo; na kukujaza kwa amani,
na furaha, na upendo; kiasi kwamba, hakuna jambo maishani litakaloweza
kupokonya hiyo amani, furaha na upendo; maana mimi ni mtoa uzima. Mimi siondoi
uzima bali natoa uzima. Alisema, Nilikujua wewe kwa jina tangu ulipokuwa tumboni
mwa mama yako.
Tunamwongelea Mungu mkuu
anayeweza kujaza mioyo yetu; anayejua kinachoendelea ndani kabisa ya mioyo
yetu. Yeye ni njia pekee! Hasemi, Mimi ni njia mojawapo, au mimi ni nabii tu. Alisema,
Mimi ni njia, na kweli, na uzima. Yeye ni kila kitu. Ndiyo maana alisema
tutaijua kweli; kuijua kweli; kumjua Yesu, kutakuweka huru!
No comments:
Post a Comment