Thursday, March 28, 2013

Msamaha! Msamaha!




Kibinadamu ni vigumu na haiwezekani kufanya mambo ya kimungu. Upendo na msamaha ni jambo la kimungu. Lakini mwanadamu yumo ndani ya anguko; ndani ya dhambi. Je, anawezaje kutenda jambo la kimungu?


Bila shaka inahitajika nguvu tofauti na uwezo wetu wa kibinadamu. Sisi ni kama magari ambayo yanahitaji kupitia kituo cha mafuta ili kupewa nguvu ya kufanya safari ndefu. Kwa uwezo wake lenyewe gari haliwezi kufanya hivyo bila nguvu hiyo.


Bwana anatuambia: Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. (Waebrania 4:16).


Bila neema ya Mungu, haiwezekani kuenenda kwa namna ya kiungu. Haiwezekani kamwe!


Kwa hiyo, badala ya kusema kuwa jambo hili ninalopitia ni gumu sana; haliwezekani; ni vizuri kumwendea Mungu wetu kila siku na kuomba neema inayoweza kutusaidia kufanya mambo yasiyo ya kibinadamu.


Mojawapo ya jambo lisilo la kibinadamu kwa asili ni kusamehe wale waliotuudhi. Kwa asili kabisa, kile kinachokuja moyoni kwanza baada ya mtu kunikosea ni kumchukia, kutamani kulipa kisasi, na kutamani yamkute mambo mabaya ili akome.


Lakini Mungu wetu anasema:

  • Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. (Mathayo 6:14).

  • Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. (Mathayo 18:21-22).
 
  • Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu. (Marko 11:25-26).

  • Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. (Luka 6:36-37).

  • Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu. (Mithali 25:21-22).


Sasa nitawezaje kufanya jambo ambalo ndani ya ubinadamu wangu halipo? Inahitajika neema kutoka nje ya mwanadamu. Na neema hiyo inapatikana tele kwa Bwana. Lakini ni lazima kuiomba na kuwa tayari kuipokea na kuitumia.


Tazama video hiyo hapo juu, na hakika Bwana atasema nawe kupitia hiyo kuhusiana na suala la kusamehe.


Bwana Yesu akubariki.

No comments:

Post a Comment