Afshin Javid alikuwa ni
askari wa Hezbollah ambaye aliyatoa maisha yake kikamilifu kwa ajili ya Allah. Katika
maisha yake yote, alijifunza kumtii Allah na alikuwa tayari kufanya lolote,
ikiwa ni pamoja na kufa kwa ajili ya Allah.
Lakini baada ya kukutana uso kwa uso na Bwana Yesu, kila kitu kilibadilika. Sikiliza ushuhuda wake huu wenye nguvu sana, ambao si tu kwamba utakutoa machozi, kama yeye mwenyewe anavyoeleza kwa machozi mengi, bali pia utajua jinsi Bwana Yesu alivyo Mungu Mkuu na wa kweli ambaye, kila anayemtafuta kwa moyo wa kweli, anamwona.
******************
Nilizaliwa kusini mwa
Irani kwenye familia ya Kiislamu. Babu yangu alikuwa ni kiongozi wa Kiislamu.
Alijenga misikiti na nyumba za yatima. Kumbukumbu zangu za zamani kabisa ni
kuhusu mapinduzi ya Irani pale Shah alipopinduliwa. Na ninakumbuka jinsi baba
yangu alivyokuwa akinibeba mabegani mwake na akawa anapiga kelele akitaka
serikali ipinduliwe, maana tulikuwa tunataka Jamhuri ya Kiislamu ya Irani.
Nakumbuka jinsi askari walivyokuwa wakimtishia baba yangu na mimi nikiwa mtoto
juu ya mabega yake, wakisema, “Tutakuua.”
Na baba yangu anasema, “Kama tukifa leo, tutakufa kwa ajili ya Uislamu. Na hilo ni jambo zuri.”
Nakumbuka jinsi nilivyokua huku nikiwa na mtazamo huo. Babu yangu na baba yangu walikuwa na ushawishi mkubwa sana katika makuzi yangu; na nilikuwa nataka sana kufanya mambo ya kuwafurahisha. Kwa hiyo, nilianza kujifunza Quran nikiwa mdogo sana. Nikiwa na miaka 12, niliyatoa maisha yangu ili kuufuata kikamilifu Uislamu na kumpendeza Allah. Nikiwa na miaka 12 na nusu, nilihisi kuwa kuomba tu haitoshi, kufunga tu haitoshi, kufanya vitendo vyote vya kiibada wanavyotuambia tufanye haitoshi. Nilijiandikisha kwenye kundi la kijeshi la Hezbollah. Na nilitumika kwenye jeshi hilo kwa miaka 3.
Nikiwa na miaka 14, nilijitolea kwenda kwenye kitengo cha mabomu ya ardhini. Lakini niliondoka Irani mwaka 1997 kwa sababu babu yangu aliniambia, “Inabidi uende Marekani ili kuupeleka Uislamu kwa Wakristo hawa waliopotea na kudanganywa.”
Lakini nilipotoka Irani, nilienda Pakistani na kusomea Uislamu wa Kisuni kule Karachi; na mwaka 1999 nilienda Malesia. Huko walinikamata kutokana na paspoti haramu niliyokuwa nayo, na nikahukumiwa kwenda gerezani.
Nilipoingizwa gerezani, niliomba kupatiwa nakala ya Quran na nikaanza kusoma. Watu humo wakaanza kusema, “Ha, kumbe unaweza kusoma Kiarabu?”
Nikasema, “Ndiyo.” Nikawauliza, “Nani huwa anaadhini wakati wa swala?”
Wakasema, “Una maana gani? Hakuna mtu aliyekariri mambo hayo.”
Nikawaambia, “Waislamu gani nyie?”
Nikaadhini pale, nao wakaniteua kuwa kiongozi wa Kiislamu mle gerezani. Nikawa nawafundisha Quran na swala au hadithi. Na nilikuwa nikiwaeleza kuwa urithi wetu unahusiana na Quran na Uislamu. Nilikuwa nikikariri Quran kila baada ya siku kumi, kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Siku moja, nilipokuwa nikiomba, nilihisi roho ya kipepo imenivamia. Nikasema kuwa nahitaji msaada. Nikaanza kuliitia jina la Allah; nikaita jina la mtume Muhammad na maimamu wote kama mwislamu wa Kishia. Nikaanza kuikemea ile roho ya kipepo. Na kila nilichofanya; kila aya ya quran niliyosoma, haikunisaidia.
Ilifikia mahali ambapo niliita, “Hudaa, Mungu, nisaidie!”
Na mara niliposema hivyo, nilisikia sauti ikiniambia, “Ita jina la Yesu.”
Kusema kweli, wakati huo sikuzingatia sana. Maana nilikuwa kama mtu anayezama maji.
Nikasema, “Yesu, kama wewe ni wa kweli, nataka nikuone.” Na sijui kwa nini nilisema maneno hayo kwa namna hiyo. Lakini mara nilipomaliza kusema maneno hayo; mara moja, kila kitu kilirudi kwenye hali ya kawaida.
Sasa, hilo silo lililonifanya niokoke. Huo ulikuwa ni mwanzo wa kuchanganyikiwa kwangu. (Kicheko).
Kweli kabisa, niliwaza, “Kwa nini Yesu amsaidie Mwislamu? Kwanza niliwaza kuwa mimi ni Mwislamu kati ya Waislamu! Sikuwahi kuona Mwislamu aliyejitoa kikamilifu kama mimi.
Na nikaanza kujaribu kusahau tukio lile, lakini kila siku nilipoamka, kila nikitembea, kila nikitaka kulala, swali lilinijia, “Kwa nini Yesu akusaidie wewe? Kwa nini Yesu …?
Ilifika mahali ambapo nilisema, nitaomba na kufunga. Na nitamwomba Mungu anionyeshe KWELI! Kwa hiyo, kwa siku 14 niliomba na kufunga. Na siku ya 14 sikupata jibu. Nikawa nimeghadhibika kwelikweli! (Kicheko). Hezbollah style. (Kicheko zaidi).
Kisha nikasema, “We Mungu, kwanza we haupo kabisa. Haupo! Umenifanyia hivi? Umenichanganya. Sasa nitafanya kile ninachotaka mwenyewe. Na siku nikifa, kama kuna hukumu, hautanihukumu kwa sababu Mungu anaweza kuona hadi moyoni. Na moyoni mwangu ulijua kuwa nilikupenda. Ulijua nilikuwa tayari kufanya chochote kwa ajili yako. Haijalishi ni jina gani nitakalokuita. Na kama inajalisha, nimekuomba unionyeshe, nami nitakufuta. Lakini hutaki kunionyesha! Nitakufuataje sasa? Nimefanya kila kitu kilicho ndani ya uwezo wangu. Kabla ya kutoka Irani, nilijitoa ili kufa kwa ajili yako. Nilishiriki hata katika kunyonga watu. Nimefanya kila kitu. Lakini hukutosheka na hayo yote. Sasa, nitafanya kile ninachotaka na hutanihukumu! Na ukinihukumu, wewe si wa haki! Na kama wewe si wa haki, haijalishi ni nini nitafanya! Kwanza hata hivyo utanihukumu isivyo haki!
Palepale, chumba chote kilijawa na uwepo wa Mungu na nilijua kuwa niko kwenye uwepo wa Mungu. Lakini vilevile nikajua kuwa nimejitumbukiza kwenye shida kubwa.
Maana Yeye ni Mtakatifu na ni wa haki. Na nikawaza …, ukumbuke kwamba, nikiwa kama Mwislamu, kusema kuwa kuna Mungu mwingine zaidi yake …, na nilikuwa nimejiinua juu ya Mungu … ; na ukumbuke kuwa, nikiwa kama Mwislamu, ninajua kuwa Allah hakuwahi kuwatembelea wanadamu. Lakini huwa anakuja kuwafutilia mbali makafiri kutoka kwenye uso wa dunia. Na nilijua kuwa na mimi ni mmoja wao. Na nilijua kuwa dhambi iliyokuwa ndani yangu ilimpa haki ya kunifutilia mbali na mimi.
Nilikimbilia kwenye kona ya chumba na nikaanza kulia. Nikasema, “Nisamehe! Nisamehe! Nisamehe!”
Lakini nilijua kuwa hakuna matumaini. Nilijua hakuna tumaini! Hawezi ... maana Yeye ni mwenye haki. Yeye ni Mtakatifu. Na niliendelea tu kulia, “Nisamehe! Nisamehe! Nisamehe!”
Ndipo aliponigusa begani na kusema, “Nimekusamehe.”
Nikasema, “Ngoja kidogo. Mbona nahisi kama nimesamehewa? Wewe ni nani? Wewe ni nani unayenisamehe na ninajisikia kusamehewa leo?”
Maana huwa tunasema, bismillah rahman rahim – kwa jila la Allah mwenye rehema na neema – lakini (sisi Waislamu) hatujui kama unakuwa umesamehewa hadi siku ya hukumu.
“Wewe ni nani unayenisamehe?”
Akasema, “Mimi ni njia, na kweli, na uzima.”
Na nilijua; nilijua; nilijua kuwa kuna jambo kubwa sana limefanyika lakini sikujua ni nini; maana nilikuwa sijawahi! Sijawahi! kamwe kusikia maneno hayo!
Nikasema, “Sielewi. Jina lako ni nani?”
*******************
Tafadhali endelea na
sehemu ya pili hapa.
No comments:
Post a Comment