Tuesday, March 19, 2013

Je, Tuache Kula Nyama Zilizochinjwa na Waislamu?



Kumekuwapo na migogoro hivi karibuni inayohusiana na suala la uchinjaji wa wanyama.

Baadhi ya watu wanaamini kuwa Wakristo tunatakiwa tuache kulala, badala yake tudai serikali itupe uhuru au ‘haki’ ya kuwa na bucha zetu wenyewe. Baadhi ya viongozi wa dini hata walifikia kuwaambia waumini wao (Wakristo) wasinunue nyama kutoka kwenye bucha za Waislamu. Tazama hapa

Sababu mojawapo inayotolewa ni kuwa tunalishwa nyama zilizoombewa dua zisizohusiana na Mungu wetu. Je, tuache sasa kununua nyama kutoka kwenye bucha za Waislamu? Je, tuwe na bucha zetu?

Kama kanuni hii ni sahihi, basi nadhani inatakiwa isiishie tu kwenye nyama, bali iende kwenye maeneo yote ya maisha. Kama kula nyama zilizochinjwa na Waislamu ni jambo linaloathiri hali yetu ya kiroho, vipi kuhusu mambo yafuatayo:

  • Tunapanda mabasi yasiyo ya Wakristo na inaaminika kwa wengi kwamba mabasi mengi yamepatikana kwa njia ya wenyewe kutoa kafara kwa shetani, ikiwa ni pamoja na kuwatoa watoto wao, wake zao, n.k.? 

  • Unajua kuwa wabunifu wengi wa mavazi ambayo sisi tunaita ni 'fasheni' na tunayavaa sana ni mashoga? Hebu tazama, kwa mfano hapa.

  • Vipi pia viongozi wetu wa kisiasa wanaotuongoza na tunawatii. Je, wote ni Wakristo? Mbona wengine ni Waislamu na hata wapagani? Sasa, kama kanuni ya kukataa nyama za wachinjaji Waislamu ni sahihi, si maana yake tunatakiwa pia kukataa kutawaliwa na viongozi wasio Wakristo?

  • Vipi huko mahotelini tunakoenda kula wali na ugali? Na huko nako inabidi tuende kwenye hoteli na kwa akina mama lishe wa Kikristo, si ndiyo?

  • Vipi kwenye nyumba za kulala wageni unakoenda kulala kwa siku moja? Unajua ni nani alilala jana yake? Au hata siku hiyohiyo? Na unajua alikuwa anafanya nini hapo kitandani?

Ndugu zangu, Mungu wetu tunayemwabudu ni Mungu mkuu sana. Mungu wetu ni Roho na mambo yake ni ya kiroho. Je, tumeanza sasa kupambana kimwili badala ya kupambana kiroho? Ukianza kupambana kimwili utakwepa mangapi? Utaweza?


Baba yetu amesema wazi: Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. (Waefeso 6:12).

Kukataa kununua nyama kwenye bucha ya Mwislamu ni kushindana kimwili kabisa; wala hiyo si vita ya kiroho. Hii ni aibu kwetu! Tunamwaibisha na Baba yetu, Yesu Kristo.

Katika Wakorintho wa kwanza 8:1-8, Bwana ana neno kwa ajili yetu:

1)  Na kwa habari ya vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.

2)  Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.

3)  Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye.

4)  Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu.

5)  Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi;

6)  lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.

Kama unaamini kuwa Mungu wako ndiye Mungu Mkuu peke yake (na hivyo ndivyo ilivyo), kwa nini uogope kile kinachotoka kwa yule asiye Mungu?

Bwana anaendelea kusema:


8)  Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.

Tunayo kila silaha ya kubomoa, kufuta, kubatilisha, na kuharibu kila dua na manuizo yasiyohusiana na Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Lakini kukataa kununua nyama kutoka kwenye bucha za Waislamu na kudai kupewa haki ya kuwa na bucha zetu wenyewe, hakika, hiyo si mojawapo ya silaha hizo.

Silaha zetu ni Jina la Yesu, Neno la Kristo, Damu ya Yesu, na Bwana mwenyewe. Kama nyama imeombewa dua mbaya, itakase kwa Damu ya Yesu.  Itakase kwa Jina la Yesu. Itamkie Neno la Kristo lililo kinyume na kile kilichosemwa na mchinjaji. Kwisha kazi!

Tusikubali mafundisho manyonge yanayoleta ugomvi na uhasama ndani ya taifa letu; ambayo hata hayaendani na nguvu ya Ukristo na Bwana wetu.

Imeandikwa:

Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome (2 Wakorintho 10:3-4).

Ngome za giza zote zinaanguka, sembuse ka-dua tu kalikoombewa nyama!!!

 

3 comments:

  1. Halleluya! Habari za siku nyingi ndugu yangu katika Kristo. Hakika Mungu akubariki maana mbegu unayopanda si yako ila yatoka kwake, bila uaminifu mtu hawezi kupewa hivi vitu yaani uelewa huu. Mahali pengine yasema kiasi unachotoa ndicho utakachopimiwa tena kwa kusukwasukwa. Sipo hapa kwa ajili ya kukupamba ila narudisha sifa kwa Yule anayekutumia, aliye Juu ya Yote-Baba Yetu wa Mbinguni.
    Taabu ya watu wengi hivi sasa wanaangalia na kusikiliza kila kitu na halafu wanabeba hivyo hivyo vilivyo pasipo hata kumuuliza aliyetuweka hapa Duniani. Na ndiyo maana shetani na mamlaka yake wameendelea kufurahi kwasababu iwachukui nguvu nyingi kufanya yale wanayotaka.
    Kinyume kabisa na Neno la Mungu, ambalo limetupa mamlaka ya kuwa juu ya huyu shetani na hivyo kuweza kulinda vile ambavyo Mungu ametupa ikiwemo amani. Ni maombi yangu kwa Roho Mtakatifu kuwa wengi watapata Maarifa haya ili tushiriki Upendo Mkuu wa Baba Yetu wa Mbinguni kwa Yesu Kristo. Amina

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom brother Revocatus. Ni kweli umepita muda sasa tangu uonekane kwenye blog hii. Natumaini Bwana wetu anaendelea kukupigania kama ulivyo hakika uaminifu wake usiokoma.

      Ni kweli kabisa tunaanza kujisahau na kumwacha shetani anapata ushindi kwa ulaini kabisa kwa sababu, badala ya kupambana kwa silaha za Mungu dhidi ya shetani, tunaanza kupambana kwa silaha za adui dhidi ya wanadamu wenzetu. Hii ni hatari sana.

      Ubarikiwe sana brother.

      Delete