Karen
Kama ilivyo kwa wanadamu wote,
Karen naye alikuwa na dhambi yake imzingayo kwa upesi. Dhambi hiyo ilimfanya
ajisikie hatia (ambalo si jambo baya), lakini sasa alijikuta akikwamia
humohumo. Matokeo yake akawa na matatizo mawili, kwanza ni hiyo dhambi yenyewe;
na pili ni hatia kutokana na dhambi hiyo.
Alijua kuwa Bwana Yesu ni lazima
atakuwa ana hasira sana naye. Lakini kwa neema ya Bwana, Karen aliweza kumwona
Bwana Yesu. Matarajio yake yote yalibadilika pale alipogundua kuwa, kumbe Bwana
hakuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
Si tu kwamba dhambi yake iliisha,
bali na hatia nayo. Hivi sasa Karen anasema, "Siwezi kuacha kumpenda
Yesu!"
Ufuatao ni ushuhuda wake alioupa
jina: Nilimwona Yesu.
***************
Nilimwona Yesu
Nilikuwa sijaenda kanisani kwa miaka mingi, ingawaje nilikuwa namwamini
Yesu - nilimpenda. Ghafla, nilihisi kama alikuwa ananiita nipate kumjua zaidi.
Nilianza kusoma shuhuda za watu wengine kumhusu Yeye; pia shuhuda za wale
waliokufa na kwenda Mbinguni, na kukutana naye. Kadiri nilivyozidi kusoma, ndivyo
nilivyojihisi kuwa karibu naye zaidi. Siku moja nilikutana na rafiki mpya
ambaye alinialika kanisani. Nikasema, "Sawa" – ilimradi iwe ni jambo
litakalonileta karibu naye.
Nilipokaa kanisani, mtumishi aliuliza swali, "Je, ni mlima gani ulio katika maisha yako?" Alituambia tutumie dakika chache kutafakari kuhusu hilo. Niliwaza juu ya mambo ambayo nilikuwa nashindwa kuyaacha katika maisha yangu. Mlima wangu mkubwa kabisa ulikuwa ni kushindwa kusamehe wale watu ambao nilifikiri walikuwa wameniumiza au kunikosea. Nilikuwa ni mtu ambaye naweza kushikilia kinyongo au kisasi kwa miaka ishirini au kwa maisha yangu yote.
Kadiri nilivyotafakari mambo haya, nilihisi uchungu mkubwa katika moyo wangu, hata maumivu ya kimwili kana kwamba moyo wangu ulikuwa ukibanwa kwa nguvu kifuani mwangu. Niliinamisha kichwa changu. Nilijua Biblia inasema nini kuhusu kusamahe. Nilidhani kuwa huenda Yesu ana hasira sana na mimi.
huku ningali nahisi maumivu katika moyo wangu, niliwaza ... utazame uso wa Yesu. Nilishasoma maneno hayo mahali fulani, lakini sikuwaza kuwa labda ningemwona kabisa kwa macho ya nyama. Na hata kama ningemwona, basi nilikuwa nina uhakika kuwa atanijia akiwa ananihukumu.
Nilipokuwa nikiwaza kwamba niangalie uso wake, niliinua macho yangu. Kile nilichokiona kilinishangaza mno! Nilimwona Yesu! Alikuwa kweli pale! Ulikuwa ni uso wake, lakini alikuwa hai, huku anatembeatembea. Alikuwa na nywele nyeusi zinazofika mabegani zikiwa na mvimvi chache, na alikuwa amevaa taji ya miiba. Nilimtazama tu. Naye alinitazama kwa tabasamu kwa upendo sana kuliko nilivyowahi kuona maishani mwangu!
Jambo la kwanza nililofikiri ni kuwa - Anaonekana tofauti kidogo kuliko anavyokuwa kwenye picha zake, lakini tofauti kidogo tu. Nilitarajia nywele zake ziwe ndefu zaidi, na pua yake ilikuwa tofauti kidogo.
sikuhisi hukumu yoyote kutoka kwake. Hilo lilinishangaza sana. Kisha nilihisi akituma kwangu upendo uliojaa huruma na rehema. Ulikuwa upendo mkubwa sana ambao nilikuwa nina uhakika kuwa binadamu hawezi kuwa nao. Nilijawa na ushangao kuona anaweza kunipenda kiasi hicho! Ilikuwa ni raha sana. Nilivutwa kabisa na upendo ule, kiasi kwamba nilihisi moyo wangu unaweza kupasuka. Sijawahi kuona kitu kama hicho, na nina uhakika sitakaa nione tena maadamu niwapo kwenye dunia hii.
Niliendelea kukodoa macho kwake. Naye pia aliendelea kutabasamu kwangu kana
kwamba nilikuwa ni mtu peke yangu duniani ambaye alikuwa wa muhimu kwake,
ingawaje nina uhakika lazima huwa anamwangalia kila mmoja wetu kwa njia hiyohiyo.
Katika maono hayo yote, Yeye kamwe hata mara moja hakuacha kutabasamu kwangu.
Baada ya hapo, nilimwona akituma miali angavu ya mwanga kuelekea kwenye moyo wangu. Nilihisi mwanga ukipenya utu wangu. Mwanga ulikuwa ni pendo safi na huruma safi. Yesu alikuwa mwema sana na mwenye upendo mkubwa kwangu – hakuwa na hukumu hata kidogo. Mimi nilihisi tu kumwagiwa upendo kutoka kwake. Yeye alionekana mkamilifu katika wema wake na ukarimu wake.
Kisha alianza kuwasiliana na mimi, lakini hakukuwa kwa maneno. Aliwasiliana nami kwa kutuma hisia. Kulikuwa na ujuzi fulani kwenye hisia ulioniwezesha kuelewa kwa urahisi na kwa uwazi kadiri zile hisia zilivyokuwa zinahamishiwa katika akili yangu.
Alisema kuwa tayari alijua kila kitu - ukosefu wangu wa msamaha kwa wengine - jinsi nilivyokuwa nimeumizwa na watu wengine, na mazingira katika maisha yangu yaliyonifanya nijisikie hivyo. Alisema, "Mimi najua kila kitu kuhusu wewe." Hilo lilinishangaza sana, lakini lilinifariji. Ilimaanisha kuwa Yeye kamwe hajawahi kuwa mbali na mimi kama ambavyo nilikuwa nikidhania. Nilitambua kwamba alikuwa daima akiniangalia, kama ambavyo watoto wetu wanapokuwa wadogo, na sisi kamwe hatuwaachi wawe mbali na macho yetu.
Hapo tena nilihisi huruma kutoka kwake zikimwagwa kwangu. Alisema, "Mimi nahisi maumivu yako. Nahuzunika pamoja na wewe." Alikuwa kama mzazi mwenye upendo ambaye atakuinua wewe wakati unapoumia, na kukushikilia katika mikono yake ya upendo. Atakufariji, na kuyafutilia mbali machozi yako yote. Kwa kweli nilijisikia nimetulizwa, na kushikiliwa kwenye mikono ya Yesu.
Baada ya kunifariji, alizungumza tena. Aliniambia nisiwe na wasiwasi au kujihangaisha na mambo haya kwa sababu Yeye angeenda kushughulika nayo kwa ajili yangu. Mimi nilihisi nguvu ya ajabu katika Yeye. Nilihisi kama mzigo umeondolewa kwangu, na nilihisi kuwa anaweza kubeba mizigo yangu yote kirahisi. Sisi sote tumefundishwa kuhusu mtu mpole na mnyenyekevu, lakini yeye anazo nguvu, na mimi niliweza kuhisi hivyo.
Nilikuwa bado namwangalia. Nilikuwa bado nashangaa baadhi ya mambo ambayo alisema. Bado alikuwa akiniangalia. Bado pia alikuwa na lilelile tabasamu kwenye uso wake ambalo linaweza kuyeyusha moyo wa mwenye dhambi mbaya na mgumu kabisa. Bado alikuwa anatuma kwangu upendo, na ulikuwa ni mwingi sana. Ulikuwa mwingi kiasi kwamba nilihisi kama moyo wangu haungeweza kuubeba wote, na kwamba ungeweza kupasuka kama ningeendelea kuupokea zaidi. Nikaanza kujisikia kuwa singeweza kustahimili tena. Labda katika hali ya kibinadamu hatuwezi. Mimi sijui.
Nikiwa na wema na usafi wote huo ndani yake, nilijisikia kama naweza kuanza kulia. Nilianza kujisikia sistahili utakatifu wake ulio safi. Yeye alikuwa ni roho katika ngazi ya juu kabisa ya ukamilifu. Unapoona hivyo, inakufanya uone hata dhambi yako ndogo kabisa. Nilihisi sistahili mbele zake, na kisha nikageuza macho pembeni.
Nilipokuja kurudisha macho, akawa ameshatoweka. Lakini niliachwa nikiwa na hisia ya hofu ya Mungu. Yesu alikuwa pale. Nilimwona. Nilimhisi. Alisema na mimi. Kitu kikubwa kuliko yote ambacho aliniacha nacho pale ni ufahamu kuwa, alinipenda kuliko mtu yeyote alivyowahi kunipenda katika maisha yangu!
Siku chache baadaye, niliwaza jinsi ambavyo nilikaa pale kanisani
siku ile huku nikijua kuwa nimetenda dhambi. Lakini kumbe Yesu akanibariki kwa maono
ya ajabu. Nilijua yeye bado ananipenda, bila masharti, licha ya upungufu wangu.
Niliwaza, hii inawezekanaje ...?
Baadaye usiku, nilianza kusoma Biblia, kitabu cha Yohana. Yesu alijibu
swali langu waziwazi:
Yohana 3:16: "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima
wa milele."
Niliposoma zaidi, akasema: "Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa kwa sababu hakuliamini jina pekee la Mwana wa Mungu."
Nilitafuta kumjua Yeye kwa moyo wangu na kwa roho yangu yote, na Yeye wala hakuniaibisha.
Alirejesha katika roho yangu utayari wa kuwasamehe wale wote walionikosea, kwa
sababu upendo hufunika hasira yetu, hofu, chuki, na hisia zingine zozote mbaya unayoweza
kufikiria.
Nilikumbuka kwamba kwenye maono yangu alikuwa amevaa taji ya miiba. Sasa nilitambua kwamba hiyo ilitakiwa kuwa ishara, ukumbusho wa jinsi alivyotupenda kiasi cha kuinuliwa na kusulubiwa msalabani kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu. Taji ya miiba ni ishara ya upendo alionao kwa kila mmoja wetu. Alikuwa kweli amenionyesha jinsi ya kusamehe.
Nilimwona Yesu Tena ...
Nilisoma kuhusu Sala ya Yesu. Ni tafakari ambapo unarudia maneno haya tena na tena kwa Yesu. Kwa mara ya kwanza nilipoomba Sala ya Yesu, nilisema, "Yesu, Mwana wa Mungu, nihurumie." Nilikuwa nimelala kitandani kwa muda wakati binti yangu mwenye umri wa miaka sita alipokuja chumbani, na kuniomba maji ya kunywa.
Nilipogeuka na kufungua macho yangu, nikaona msalaba mdogo katika kona ya
chumba changu, karibu na dari. Ulikuwa wa mti, karibu inchi nne kwa urefu, ukiwa
umefungwa pete nne za dhahabu kwenye kona zake zote nne. Niliutazama kwa
sekunde kadhaa. Niliuona kwa ufasaha kabisa. Nilipogeza macho kwingine, kuja
kurudisha, ukawa umetoweka.
Mara ya pili nilipoomba Sala ya Yesu, nilisema, "Yesu, Mwana wa Mungu, nakuamini wewe." Niliisema sala ile kwa muda wakati nikiwa nimelala kitandani. Hatimaye nilianza kupatwa na usingizi. Ghafla, kitu kilinigutusha kutoka kwenye usingizi ule.
Niliporudiwa na fahamu zangu, niliona upande wangu wa mgongni, nyuma ya
kichwa changu na mabega. Kisha nikaona mikono miwili ikinyooshwa kuelekea
kwenye shingo yangu kwa ili kunikumbatia. Mtu huyu aliponikumbatia, niliona uso
wa Yesu juu ya bega langu wakati alipokuwa tayari amenikumbatia, na kisha alitabasamu
kwangu, yaani kwangu mimi niliyekuwa nikiangalia maono yale! Niliwaza, mbona ni
mwema kiasi hiki kwangu?
Siwezi kuacha
kumpenda!
Na: Karen
Templin
******************
[Ukipenda kusoma ushuhuda huu kwa lugha ya Kiingereza, bofya HAPA.]
Enter your comment...Naitwa Miraji Niko Iringa ,nabarikiwa kuliko maelezo napoendelea kusoma shuhuda zako MTUMISHI wa Baba yetu wa Mbinguni ,Tafadhali nakusihi endelea kutoa shuhuda nyingine nyingi kadiri uwezavyo!Na Roho wa Mungu wetu yuu juu yako kukuwezesha haya!
ReplyDeleteAmen Miraji.
DeleteAshukuriwe Mungu kwa kusema nawe kupitia shuhuda hizi.
Kusema kweli natamani sana kutoa shuhuda zaidi lakini kumekuwa na mambo mengi mno kiasi kwamba nakosa nafasi ya kufanya hivyo. Mara nyingi nakuwa facebook ambako hakuhitaji shuhuda ndefu kuandaa makala ndefu kama za blog na pia majadiliano yanakuw ani ya papo kwa hapo. Ubarikiwe ndugu.