Monday, June 3, 2013

Akef Tayem, Mwislamu Kutoka Palestina Akutana na Bwana Yesu na Kuokoka - Sehemu ya 2





Hii ni sehemu ya 2 ya ushuhuda wa Akef Tayem, Mwislamu wa kutoka Palestina ambaye alikutana na Bwana Yesu, kisha akawa Mkristo. Ili kupata picha kamili, tafadhali anza kusoma sehemu ya 1 HAPA.

…………………….


Baada ya Akef Tayem kukataliwa na familia yake kwa sababu amekubali kumpokea Yesu Kristo maishani mwake, alijikuta akikosa kabisa hamu ya kula kwa siku zaidi ya 40 akiwa porini. Mwili wake ulidhoofika sana na kuishiwa maji. Yafuatayo ni mahojiano kati ya mtangazaji, Sid Roth and Akef Tayem:

Sid Roth:
Je, ulimwomba Mungu akunyeshee mvua?

Akef:
Ndiyo. Ndiyo. Nilikuwa na kiu sana, na nilikuwa dhaifu mno.

Sid Roth:
Je, ilionekana kama kuna mvua itanyesha?

Akef:
Hapana. Hakukuwa hata na dalili; wala hata wingu. Nilidhoofika sana kiasi kwamba sikuweza hata kutembea kwenda kwenye kutafuta maji au chochote kingine.

Sid Roth:
Ulinieleza kuwa ngozi yako ilianza kupasukapasuka.

Akef:
Nikiwa huko porini, nilikuwa nikisoma Biblia kwa sauti na nilikuwa nikipenda kusikia mwangwi. Na baada ya muda, sikuweza kusoma Biblia yangu kwa sauti, maana kila nilipofanya hivyo, midomo yangu ilichanika na damu ilitoka. Hata vidole vyangu navyo vilipasuka kwa sababu ya kuishiwa maji mwilini.

Sid Roth:
Kwa hiyo uliomba ili upewe muujiza wa mvua?

Akef:
Ndiyo, niliomba mvua. Niliwaza kuwa labda nimepitiliza. Haikuwa ni mpango wangu kuwa kwenye mfungo wa siku 40. Kwa hiyo, nilimwomba Mungu alete mvua.

Sid Roth:
Na ulianza kutoka kwenye mwili wako?

Akef:
Kilichotokea ni kwamba, kulikuwa na mwamba ambao nilikuwa nikikaa hapo. Na nilikuwa na Biblia yangu. Na kilichotokea ni kwamba, ilikuwa kama napoteza fahamu. Nilikuwa naona mwanga, mara giza; mara mwanga, mara giza. Na ikawa kama vile miti na  mbingu zinazunguka. Nadhani nilikuwa kwenye hali fulani ya kupoteza fahamu.

Kilichofuata hapo, nilijiona niko kama futi 10 hivi juu, huku nikiangalia kwa chini ule mwamba, ile Biblia na ule mwili ambao sikuweza kuutambua. Ilikuwa ni kama natazama kwenye kioo. 

Sid Roth:
Yaani ulikuwa unajitazama lakini hukutambua kuwa ni wewe?

Akef:
Ndiyo. Kwa sababu nilikuwa naangalia huyu mtu ambaye alikuwa amekonda, ana damu mdomoni, vidole vimepasukapasuka na macho yametumbukia ndani. Sikuweza kumtambua.

Sid Roth:
Nini kilitokea baada ya hapo?

Akef:
Ninachokumbuka, kilichofuata nilianza kupaa kuelekea mbinguni.  Nilianza kujaribu kujishika mikononi lakini sikuweza. Nikawa nawaza, kwa nini? Nyama ya mwili wangu imeenda wapi?
Niliendelea kwenda juu hadi nikavuka eneo lenye mwanga. Nikaingia kwenye eneo la giza nalo nikalipita. Nikafika kwenye eneo lenye mwanga, kisha kwenye giza tena. Halafu kwenye eneo la tatu lenye mwanga, nilisimama.

Hapo, kama futi kumi hivi mbele yangu, niliona  umbile la mtu linaanza kutokea. Na cha ajabu ni kuwa, japo hakuna mtu aliyenieleza, nilijua kuwa yule alikuwa ni Yesu Kristo. Na umbo lake lilipokamilika, alianza kuelekea kwangu. Alipofika kama umbali wa mkono, akasimama. Akasema, “Gusa.” Nikanyosha mkono wangu hadi kwenye mbavu zake. Na mara nilipomgusa tu, nikajikuta niko tena kwenye ule mwamba; na mvua ilikuwa inanyesha!

Sid Roth:
Lipi lilikuwa ndilo wazo lako la kwanza mara uliporudi ndani ya mwili wako?

Akef:
Nilianza kurukaruka na kucheza. Nimeona nguvu za Mungu, nimemgusa Mwana Kondoo wa Mungu. Hilo lilikuwa ndilo jambo pekee nilililojua. Maana kabla ya hapo nilikuwa siwezi hata kusogeza mguu.

Sid Roth:
Watu walijua habari zako na wakakualika kwenye Kanisa la Kibaptisti ambao hawaamini miujiza ili ukaongelee kile kilichokutokea. Hebu nieleze kuhusiana na hilo.

Akef:
Mimi sikujua, na namshukuru Mungu kwamba sikujua hilo – kwamba wanaamini au hawaamini. Nilichofanya mimi ni kuongea tu kile nilichokifahamu. Ni kama yule aliyesema, nilikuwa kipofu na sasa naona. Mimi nilieleza tu kilichonitokea. Na kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mshirika wa kanisa lile kwa miaka zaidi ya 30; na alikuwa kwenye kiti cha magurudumu.

Na inashangaza kwamba alianza kuelekea mbele ya kanisa kama vile anataka kuzungumza na mimi au kunigusa. Na niligundua kuwa mkono wangu wa kushoto ulianza kupata joto.

…………………………………

Je, nini kilitokea baada ya hapo?
Fuatilia sehemu ya tatu ya ushuhuda huu ili kujua kile ambacho Bwana Yesu alifanya kupitia kwa Akef Tayem, ambaye alikuwa Mwislamu na sasa anamwamini Bwana Yesu. Tafadhali bofya HAPA.

No comments:

Post a Comment