Tuesday, August 7, 2012

Je, Watakatifu Hutuombea Tulio Duniani?



Kanisa Katoliki limekuwa likifundisha kwa miaka na miaka kwamba tunaweza kuwaomba watakatifu walioko mbinguni watuombee kwa Mungu. Je, jambo hili lina ukweli kibiblia? Je, hili ni fundisho la Mungu au ni la wanadamu? Je, mtu anayefanya hivyo anampendeza Mungu au anamuudhi?

Hakuna mahali popote katika Biblia ambapo tumeagizwa kuwaomba watakatifu ili watuombee kwa Mungu. Sasa haya mafundisho yanatoka wapi? Unawezaje kuwafundisha watu kitu kisicho kwenye Biblia halafu usiwe na hatia ya kuongeza au kupunguza ujumbe wa Mungu; maana Bwana anasema kuwa atakayeongeza au kupunguza katika neno lake ana hatia. (Ufunuo 22:19).


Je, mtu anatakiwa afanye nini ndipo tumhesabu kuwa ameongeza au kupunguza katika Neno la Mungu? Je, kuongeza au kupunguza si ni kusema chochote ambacho hakimo ndani ya Biblia – bila kujali aliyesema ni maarufu au anaheshimiwa na wanadamu kiasi gani?

Lakini tunaona Petro anavyosema juu ya wanadamu wenye heshima lakini wanapingana na Mungu: Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. (Mdo. 4:19-20). 

Petro na Yohana hawakujali uzito wa wakuu wa dini waliotawala nyakati zao. walichojali wao ni kweli ya Neno la Mungu. Na walipinga waziwazi mambo ya wakuu wa dini kwa vile yalienda kinyume na kweli ya Injili.

Sijui wewe msomaji wangu una msimamo gani juu ya mambo ya wanadamu ambayo yako kinyume na Biblia. Je, unayakataa au unayabeba kwa sababu waliokufundisha ni watu wenye heshima kubwa katika jamii au katika dini?
Mwanadamu ni mwanadamu tu. Hakuna anayeweza kuwa juu ya Mungu na Neno lake. Kama mwanadamu akifundisha kilicho kinyume na sheria ya Mungu, mafundisho yake hayo ni ya kupuuzwa tu bila kujali msemaji ana elimu au heshima kiasi gani!

Paulo anasema wazi: Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. (Gal. 1:6-8).

Sasa je, tunaweza kuwaomba watakatifu walio mbinguni? Injili ya Kristo inasema nini juu ya kuomba? Tazama maandiko yafuatayo:

  • Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. (Mathayo 7:7-8).
  • Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. (Yohana 15:7)
  • Nanyi mkiniomba neno lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya. (Yoh. 14:13-14).
Kumbe tunatakiwa kuomba sisi wenyewe kuhusiana na mahitaji yetu. Kuomba ni agizo halali kabisa kutoka kwa Bwana. Je, mwanadamu mmoja anaweza kuomba kwa niaba ya mwanadamu mwingine? Jibu ni ndiyo. Biblia inasema: 

  • Mchukuliane mizigo na kuitimiza hiyo sheria ya Kristo. (Gal. 6:2). Kuchukuliana mizigo ni pamoja na kuombeana.
  • Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. (Mt. 5:44).
  • Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu… (Kol. 1:9).
  • Ndugu, tuombeeni. (1 Thes. 5:25).
  • Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, siku zote katika sala zangu... (Rum. 1:9-10).
  • Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe. (Rum. 10:1).
  • Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; na kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. (Rum. 15:30-32).
  • Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo... (Fil. 1:19).
Maandiko haya yanatuonyesha kuwa pamoja na kwamba tunaweza kufaidika kwa maombi ya watu wengine; au wengine wanatarajiwa kufaidika na maombi yetu; lakini waombaji hawa wote ni wanadamu walio hai – si wale ambao tayari walishakufa!

Haishangazi basi kuona Mungu akisema: Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao. (Zab. 16:3).

Sasa je, kuna maombi yoyote kutoka mbinguni ambayo tunaweza kufaidika nayo?

Jibu ni ndiyo. Tazama maandiko yafuatayo:

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye aliyejaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi, na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. (Ebr. 4:14-16).

Je, una mahitaji gani? Yupo kuhani katika patakatifu pa patakatifu mbinguni, yaani Yesu Kristo. Huyo ndiye Mwombezi wetu ambaye anafikisha maombi yetu kwenye kiti cha rehema cha Mungu – si mtakatifu awaye yote! 

Unajuaje hili?

Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya  Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote. (1 Tim. 2:5-6).

Iweje basi leo watu wengine wafundishe kuwa Maria mtakatifu mama wa Yesu anaweza kutuombea msamaha kwa mwanawe? Yesu ndiye mpatanishi pekee kati yetu na Mungu. Unataka hadi mtu aseme nini ndipo ujue kuwa fundisho hili ni la uongo na hili ni la kweli?

Maandiko pia yanasema: ... basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.  ... yeye, kwa kuwa anakaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai siku zote ili awaombee. (Ebr. 7:22-25).

Vipi sasa kuhusu watakatifu walio mbinguni?

Maandiko yanasema wazi: Asionekane kwako ... mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA. (Kumb. 18:10-12).

Je, wafu maana yake nini? Watakatifu walio mbinguni ni sehemu ya wafu au ni sehemu ya walio hai?

Labda utaniambia, “Ah, wafu maana yake ni watu wenye dhambi waliotengwa na Mungu.” Sikatai. Maana hiyo ni sawa. Ni mojawapo ya maana ya kuwa mfu. Lakini, Biblia inasema kuhusu maskini Lazaro: Ikawa yule maskini alikufa... (Lk 16:22). 

Je, ‘alikufa’ maana yake si alikuwa mfu? Na tunafahamu kuwa Lazaro alienda mbinguni. Kwa hiyo, kwa sisi tulio duniani, Lazaro ni mfu aliye mbinguni. Ni vivyo hivyo kwa habari ya watakatifu wote ambao hawako duniani leo. Ni wafu! Je, haijaandikwa kwamba: Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. (Ufu. 14:13). Je, ‘wafu wafao’ katika Bwana ni watakatifu au si watakatifu?

Biblia inasema: Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. (Hosea 4:6). “Wanaangamizwa”, sio “wanaangamia!” Siku ya mwisho hutasema, “Bwana, mimi sikujua.” Ni kweli hukujua, lakini hicho hakitakuwa kigezo cha kusamehewa. Kujua ni sehemu ya wajibu wa kila anayetarajia wokovu wa Bwana. Ni jukumu lake kujua! Ukimtumainia mwanadamu badala ya Neno la Mungu uko kwenye hatari kubwa ya kupotea kutokana na kudanganywa!



Mungu tunayemwabudu anaona yote, anasikia yote, anajua yote, na yuko mahali pote kwa wakati uleule. Sasa, unaponiambia kwamba mtakatifu Petro au Yohana au Maria anaweza kusikia maombi ya watu milioni moja wanaoomba Tanzania; milioni moja Kenya, milioni tano Marekani, nk, na kuweza kuyafanyia kazi; una maana kuwa mtakatifu huyo ni lazima awe na tabia zote hizo hapo juu ambazo ni za Mungu Mwenyezi peke yake!! Je, hilo ni jambo linaloingia akilini? 

Acha kudanganywa kwa mafundisho ya uongo! Acha kuangalia wanadamu usoni na kusema, “Huyu kwa elimu aliyo nayo hawezi kunidanganya.” Elimu na cheo si hoja ya msingi. Hoja ni kuwa je, anachosema kinatokana na Neno la Mungu? 

Mwisho nakuomba utafakari maneno yafuatayo kutoka kwa Bwana:  

Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa); kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lolote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lolote lililofanyika chini ya jua. (Mhubiri 9:4-6).

Kazi kwako! Usiuze haki ya mzaliwa wa kwanza kwa ujira wa kunde za mlo mmoja kama alivyofanya Esau!

Tumeitwa kupokea wokovu; si kushikilia dini. Okoka leo. Mkaribishe Yesu awe Bwana na Mwokozi wako. Yesu hakuleta dini bali alileta wokovu.

Biblia inasema: Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. (Warumi 10:9).

Mafundisho mengine ya uongo ni ya watu kusema, “Hakuna kuokoka duniani.” Bwana Yesu alipoenda nyumbani kwa Zakayo, alitamka maneno haya: Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. (Luka 19:9). 

Maandiko pia yanasema: ... wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. (2 Wakorintho 6:2). 

Sasa unaokokaje? Imeandikwa: Kwa maana, kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. (Warumi 10:10).

Tafuta watu wanaokiri wokovu nao watakusaidia. Mungu akubariki na kukufungua macho ya rohoni ili uweze kufanya yale aliyoagiza Bwana wetu Yesu Kristo na si kutumainia maagizo ya wanadamu na wanadini. Ubarikiwe na Bwana.


15 comments:

  1. jamani mtumishi barikiwa sana,nimependaje hii mada?

    ReplyDelete
  2. Mungu akubariki sana kwa kuwa mfuatiliaji na mwenye kiu ya kweli yake.

    ReplyDelete
  3. Kaka asante kwa somo zuri. Ndio maana unakuta wanafuata mapokeo na wala sio Biblia.

    ReplyDelete
  4. Amina. Ubarikiwe. Ni kweli kwamba watu wanafundishwa hicho kinachoitwa mapokeo. lakini hawajishughulishi kupima kama yanaendana na Maandiko au la. Na tatizo kubwa ni kwamba humo walimo hakuna mafundisho ya Injili bali kuna mafundisho na maagizo ya wanadamu kama Biblia inavyosema.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Yan mkuu mwenye ni mkatoliki yan hua najiuliza saana kwann tuna waomba walio kifa watuombee et tukifa tunaenda toharani ,,,mara tuna muomba mt lita atuombee hii hua siielewi kabisa ila leo nimeelewa

      Delete
  5. Ukweli utabaki kuwa Kweli. Mungu awafungue watu wote wenye mwili kwa maneno mazuri yasiyo ya hekima ya kibinadamu ila ni kutoka kwa Roho wa Mungu aliyekutumia. Ubarikiwe na kukuzidisha Katika Jina la Yesu

    ReplyDelete
  6. Asante bro. Revocatus kwa kutembelea blog hii. Nashukuru pia kwa maoni yako. Ni kweli kabisa unavyosema. Tunatakiwa kusimama na neno la Mungu. Tupime mafundisho ya walimu wetu kwa Neno na si kupima Neno kwa mafundisho yao. Mungu akubariki.

    ReplyDelete
  7. mh! Umesema kweli lakini jambo moja najiuliza kama wote wangekuwa wa kanisa lako na wawe na uelewa kama wako, nani angeandika kama ulivyoandika kwaajili ya nani na kwa utukufu wa nani.

    Siku zote naamini kuwa Mungu anawajua walio wake popote, iwe ni ndani ya kanisa katoliki au lako. Na kwamba katika nyumba ya mfalme huwezi kukuta vyombo vyote ni vya dhahabu, bali viko vya aina mbali mbali; vya majani, miti, chuma, n.k. Na iko hivyo kwa makusudi maalumu. Ni kama wewe usivyoweza kuvaa suti unapoenda kupalilia migomba!

    Ubarikiwe kwa uchambuzi na uandishi wako mzuri wenye kushawishi! Lakini Mungu haangalii kama mwanadamu bali anaangalia zaidi ya jinsi tunapoweza sisi wanadamu kukoma kuangalia.

    Kinachonifurahisha zaidi ni kwamba sisi wote ni marehemu watarajiwa na kama si hivyo basi siku ya kiama yaja ambapo kila mmoja atapiga magoti mbele ya kiti cha enzi zetu zote ambapo ukurasa wa kila mmoja utafunguliwa kuona tulivyokuwa hapa duniani. Sina hakika kama hayo ya kila mmoja yatakuwa wazi kwa watu wote, ikiwa hivyo nitafurahi zaidi maana hata ya sisi wachambuzi na waandishi wazuri yatajulikana pia maana Mungu hana upendeleo!

    Kwaajili ya kunipanua zaidi na au kuniuliza au hata kunisema tahadhali tuwasiliane kwa e_mail hii: mbilinyig@gmail.com

    Asante!

    ReplyDelete
  8. kaka mafundisho yako yana tija na yanaeleweka wazi sana,nimependa sana na nitaendelelea kusoma nakala zako

    ReplyDelete
  9. Asante Chipengwa kwa maoni yako na kwa kutembelea blog hii. Mungu akubariki.

    ReplyDelete
  10. Mbilinyii asante sana kwa kutumia muda wako kutembelea blog hii; na pia kutoa maoni.

    Kama kuna jambo ambalo sijasema hata siku moja kwenye makala yote ambayo huwa naandika ni kumwambia mtu yeyote aje kwenye kanisa langu.

    Mimi si mchungaji na wala sina kundi lolote ninalochunga. Labda unaweza kuniweka kwenye huduma ya ualimu. Kwa hiyo, sina kabisa maono ya kuwakusanya watu kwenye ‘kanisa langu’.

    Msimamo wangu daima ni huu: Mtu amjue Kristo ambaye ni Mwokozi wa wanadamu WOTE bila kujali hayo tunayoita madhehebu. Kristo wala hakuja na madhehebu. Ukipekuapekua kwenye blog hii, utakuta makala niliyoiita ‘Madhehebu: Mzigo usio wa lazima’.

    Kile ninachoamini Mbilinyi, na ambacho ndicho nakiona kwenye Biblia, ni watu wamjue na kumkubali Kristo kama Mwokozi wao BINAFSI na kuwa na uhusiano naye KIBINAFSI kila dakika ya maisha yao. Mtu akifanya hivyo, haijalishi yuko kwenye dhehebu gani. Tatizo tu litakuja kwenye ukweli kwamba taratibu za kimadhehebu zitamwekea uzio katika safari hiyo ya kuwa na huo uhusiano binafsi na Mwokozi wetu.

    2 Timotheo 2:20 ambayo umenukuu, inayohusu kuwapo kwa vyombo vya thamani mbalimbali, vikiwamo hata vya udongo na miti, inasema kuwa unaweza kuviweka katika makundi mawili – vyenye heshima na visivyo na heshima.

    Ila ukiendelea kusoma utaona kuwa haimaanisi kuwa hayo ndiyo kweli makusudi ya Mungu. Mstari wa 21 unasema: Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.

    Kumbe lengo ni kila mmoja wetu achukue hatua ili atoke kwenye kuwa chombo kisicho na heshima na kufanywa mwenye heshima.

    Sasa watakuwaje wenye heshima?

    Bila shaka Mungu au malaika hawaji kuhubiri; wala Roho Mtakatifu hafanyi kazi hii peke yake. Mungu anasema kwamba: Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. (Eze. 3:18).

    Je, Mbilinyi, Bwana Yesu hajatuagiza kwenda kila mahali kuwahubiria habari njema ya ufalme wa Mungu? Imeandikwa: enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi (Mt. 28:19) - si wanadini au wanamadhehebu.

    Nikikunukuu ,unasema kwamba: “Ubarikiwe kwa uchambuzi na uandishi wako mzuri wenye kushawishi! Lakini Mungu haangalii kama mwanadamu bali anaangalia zaidi ya jinsi tunapoweza sisi wanadamu kukoma kuangalia.”

    Je, unamaanisha niache au tuache kueleza habari za ufalme wa Mungu kwa vile Mungu anawajua walio wake?

    Mimi naamini kuwa suala hapa si ushawishi wangu, bali ni je, hivyo ndivyo Biblia inavyosema? Kama nilichoandika ni kinyume na Biblia, hapo ndipo kuna haja ya kukikataa na kuachana nacho kabisa. Kama kuna jambo ambalo najaribu kusimamia siku zote ni Biblia – si dhehebu lolote. Hata ninapotaja kile ambacho kiko kwenye madhehbu fulani, ambacho nakiona hakiko sawa, sifanyi hivyo kwa kulinganisha na kilicho kwenye madhehbu mengine; bali nakilinganisha na Biblia. Biblia ndilo Neno la Mungu wetu.

    Lakini pia, haimaanishi hata kidogo kuwa mimi najua kila kitu. Inawezekana kabisa nikawa nimeenda kinyume mahali fulani. Niko tayari kusahihishwa wakati wowote kwa ushahidi wa maandiko.

    Asante sana Mbilinyi. Mungu akubariki sana.

    ReplyDelete
  11. Kaka James,

    Hakika nina kila sababu ya kukushukuru na kukutakia kila la kheri katika kazi hii Njema sana, maana naamini kuwa hata kwa swali langu kwako; jibu lako halikuwa kwangu tu bali maneno uliyoyasema yatakuwa yamewajenga na wasomaji wako wengine. Maana kama nilivyokuelewa bila shaka na wengine watakuwa wamekuelewa vivyo vivyo. Asante!

    Tahadhali, usiache kazi hii kwasababu ya maswali ya watu wachanga kama mimi wa Neno la Mungu ama kwa kuto soma Neno la Mungu ipasavyo au kupata mafundisho hafifu toka katika 'Mzigo usio wa lazima' - Dhehebu, tulimo!

    Kukuandikia na kukuuliza maswali kuna malengo mengi ikiwa ni pamoja na kukuonyesha kuwa wasomaji wako tupo hivyo kazi yako haiendi bure, au wasomaji wako tunahitaji kujua zaidi maeneo tunayokuuliza kutokana na shaka tuliyonayo, n.k. Kwa maneno haya naomba tafsiri ya maswali yangu kwako ya lale hapo na si kama ninavyoona ulikuwa unaelekea kunitafsiri. Ingawa huko ulikoelekea kunitafsiri kumeniongezea faida ambapo pia umewaelimisha watu wengine.

    Hata hivyo, nimefarijika sana na mstari wako wa mwisho ambapo umenionyesha kuwa umenielewa kuwa maswali yangu kwako hayakuwa na nia mbaya bali njema, kwani umenishukuru na kunitakia baraka za Mungu. Nawe ubarikiwe zaidi ili uendelee na kazi hii kwaajili ya kutuelimisha, kutujenga na kutuimarisha katika imani wasomaji wako. Asante!

    G. Mbilinyi

    ReplyDelete
  12. Ndugu Mbilinyi ankushukuru tena kwa kuniandikia na kutembelea kwenye blog.

    Pia samahani kama nimekuwa careless katika kuchagua maneno yangu kiasi kwamba ikaonekana naelekea kukutafsiri vibaya.

    Mungu akubariki kwa nia yako njema ya kutaka kumjua zaidi na zaidi. Naomba tuendelee kujengana, maana naamini kuwa Bwana Yesu hana watu wa hovyo kamwe.

    Kila mwanadamu, amempa kitu fulani cha kipekee kwa ajili ya faida ya wengine. Labda sisi wenyewe ndio tunaweza kujidhania hatufai, lakini kwa hilo unalofanya la kuitafuta kweli, utazidi kugundua mambo makubwa ambayo amewekeza ndani yako kwa ajili ya faida yako na kanisa kwa ujumla. Uzidi kubarikiwa.

    ReplyDelete
  13. mungu roho mtakatifu ndio chanzo cha hekima, na kanisa takatifu katoliki la mitume hufuata hekima kwanza, maana hekima ni roho mtakatifu.hii desturi ya watakatifu wote wa mungu mtuombee haikuanza leo, ilianza toka simon petro akiwa pope wa kwanza wa kanisa takatifu katoliki la mitume. biblia ni lugha ya mafumbo ambayo kama huna roho mtakatifu kuyafumbua hutawzea. ZABURI 16:3, “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio ninaopendezwa nao ”. tofautisha kuomba na utuombee!. na pia mkae mkijua cha kale ni dhaabu.

    ReplyDelete
  14. na kweli wakatoliki wanaonekana kujawa na hekima sana maana wanaheshimu imani za wenzao na kutozizungumzia sababu haziwahusu,na huku wakijua mapungufu tumeumbiwa sisi wanadamu. japokuwa wao ndio kanisa na dheebu la kwanza ulimwenguni huku aliyekabiziwa funguo ya kanisa mtume petro ndiye aliyekuwa pope wa kwanza wa kanisa hilo.mathayo 7:3 mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?

    ReplyDelete