Wednesday, December 4, 2013

Jiandae kwa kurudi kwa Bwana! Sehemu ya 2




Mpendwa msomaji wa blog hii na mwana wa Mungu aliye hai, hii ni Sehemu ya 2 ya ushuhuda huu. Katika Sehemu ya 1, tuliona safari ya kwanza mbinguni ya dada Bernarda. Katika sehemu hii, anatueleza kile kilichotokea pale Bwana Yesu alipomchukua kwa mara ya pili na kwenda naye mbinguni kisha akamrudisha.




Safari Yangu ya Pili

Siku moja tulikuwa sote kwenye maombi; tulikuwa watu takribani ishirini. Kama kawaida, tulianza kwa kumsifu na kumtukuza Bwana.

Ghafla, tulihisi uwepo wa Mungu. Ulikuwa na nguvu sana kana kwamba ilikuwa ni siku ya Pentekoste. Nakumbuka mama mkwe wangu, bibi mzee ambaye alijitoa kwa Mungu, aliniambia, “Bernarda, hebu tupunguze kelele wakati wa kusifu. Tunapaza mno sauti.”

Alikuwa sahihi, maana kusifu kulikuwa ni kama sauti ya mafuriko ya maji. Wakati nikiwa tayari kuwaambia kaka zangu wapunguze sauti, nikamsikia Bwana akiniambia: “Usiseme chochote! Duniani, watu wanapopaza sauti, hakuna anayejali. Sasa, kwa nini usimamishe sifa?” Kwa hiyo tuliendelea kumsifu na kumwabudu Bwana. Nilihisi kuwa kuna kitu kikubwa kilikuwa kinaenda kutokea. Ghafla, nilikumbuka kile ambacho Bwana aliniambia wakati wa safari yangu ya kwanza. Alisema, “Nitarudi kwako tena.”

Mara moja niliona nuru kali ikijaza nyumba yangu. Kaka zangu nao waliiona nuru ile. Wote walipiga magoti mbele za Mungu. Sikujua cha kufanya; nilibaki tu nimesimama pale. Nuru ile ilizidi mng’ao zaidi, na mara ikawa umbo la mwanadamu. Mbele yangu, akawa ni Bwana Yesu Kristo; mzuri na aliyejaa upendo. Sijawahi kuona uzuri kama ule kwenye uso wa mtu yeyote duniani. Alikuja karibu na kila mmoja wa kaka zangu. Lakini nikiwa najiandaa kusema kwamba Bwana alikuwa amekuja kwa ajili yangu, nilianza kunena kwa lugha. (1 Wakor 14:39-40).

Kwa kule kunitazama tu, roho yangu ilitoka kwenye mwili na tayari nikawa hewani. Yesu alinishika mkono na tukaelekea welekeo wa Jamuhuri ya Dominika. Tulipofika kwenye jiji, Bwana akaniambia, “Kuna dhambi mbili kubwa ambazo nchi hii inatenda mbele za Baba Yangu; uchawi na kuabudu sanamu.” Niliwaona watu wa nchi ile wakiwakimbilia wachawi na miungu sanamu.

Baada ya hapo, Bwana alinileta hadi Venezuela. Nilikuwa niko hewani kisha Meksiko. Kule Venezuela, nilikuwa niko hewani na Bwana Yesu, lakini niliona watu wakigeukia uganga, mingu na uchawi. Kule Meksiko, niliona watu wakikusanyika na kuabudu mapepo. Bwana akaniambia, “Machukizo ya dhambi hii yamefika mbele za Baba Yangu. Ishara ya kwanza ninayotoa kama onyo ni kwamba kutakuwa na tetemeko Meksiko endapo wakazi wa nchi hii hawatatubu na kunirudia Mimi.” (Baadaye niliporudi duniani, nilienda Meksiko na kuhubiri ujumbe huu. Watu hawakusikiliza, na hivi karibuni, kulikuwa na tetemeko baya sana Meksiko).

Wakati tulipokuwa bado tuko hewani, Bwana aliniambia kuwa Mikono ya Baba Yake imeshanyoshwa juu ya watu wa dunia. Niliona bahari ikiwa na mawimbi makubwa sana, kama mazimwi. Pia niliona tufani zikitokea dunia. Nikamwuliza Bwana, “Bwana, itakuwaje kuhusiana na Wakristo wakati haya yote yatakapotokea?” Akanijibu, “Nenda na ukawaambie kwamba, kwa wale walio waaminifu Kwangu, hakuna hata unywele wao mmoja utakaoguswa.”

Baada ya hapo, Bwana alinileta sehemu nyingine. Niliona mahali ambapo dunia ilipasuka. Bwana akaniambia, “Muda si mrefu ujao, nchi nyingi zitatoweka kwenye uso wa dunia.”

Kisha tuliondoka hapo na kwenda sehemu nyingine ambako niliona maji yakiwa katika mwendo. Tuliingia kwenye shimo la chini kwa chini hadi ndani kabisa ya dunia. Niliona milango mikubwa. Haikuwa inafanana na ile niliyoiona kwenye safari yangu ya mara ya kwanza. Kwenye milango hii kulikuwa na minyororo mikubwa. Bwana alienda kwenye ile milango. Aliondoa minyororo na kuniruhusu niingie ndani ya shimo.

Niliona maelfu ya watu wakiwa vichwa chini huku wamevaa mavazi machakavu. Walifungwa minyororo mikubwa. Nikasema, “Bwana, hii maana yake nini?” Akajibu, “Wanaume na wanawake hawa wote wanaelekea Kuzimu.” Miongoni mwao nilimwona kaka mkubwa wa mume wangu, Adolfo. Alikuwa ni mtu mwenye matatizo. Alikuwa akioa na kuacha kadiri apendavyo na alikuwa akimlaani Mungu. Kisha nilianza kumwomba Bwana nirudi duniani kwenda kumwonya Adolfo kwamba alikuwa anaelekea kuzimu; lakini Bwana hakunijibu. Nilimwona tena Adolfo na mke wake wakitembea kwenye lile shimo. Walikuwa ukingoni kabisa mwa shimo. Nilimwomba tena Bwana nirudi duniani ili nikawaambie watu kile nilichokiona. Bwana aliinua mkono wake na kusema, “Nenda kawaambie kuwa muda ni kama umekwisha … maelfu kwa maelfu ya watu wataenda kuzimu. Muda wa Adolfo umekwisha. Atakufa.”

(Niliporudi duniani, shemeji yangu Adolfo hakutaka kubadili maisha yake. Siku moja alirudi ghafla kutoka kazini na kumwambia mke wake, “Sitaki kufanya tena kazi. Kuna kitu kinaniambia kuwa nitakufa.” Mke wake akajibu, “Ni kwa sababu umelewa kama kawaida yako ndiyo maana unasema hayo.” Wote walienda kulala. Dakika chache baadaye, mke aliona maono. Alijiona yeye na mume wake wakiwa kwenye shimo, wamevaa nguo chakavu, na wanaekea kuzimu. Alimsikia Bwana akimwambia, “Muda wenu nyie wawili umekwisha.”)

Wakati nilipokuwa bado angani, Bwana aliniambia, “Unajua ni kwa nini nimekuleta hapa kwa mara ya pili? Ilikuwa ni kukuonyesha kwamba katika ziara yako ya mara ya kwanza idadi ya watu waliopotea ilikuwa ndogo kuliko sasa.” Hivi sasa kulikuwa na roho nyingi zaidi zilizopotea kuliko kwanza.

Kisha Yesu na mimi tuliondoka mahali pale na kupaa tukapita mbingu ya pili. Tulipofika kwenye mbingu ya tatu, Ufalme wa Mungu, niliona malaika wakienda mbiombio kutoka upande mmoja hadi mwingine. Nikamwuliza Bwana, “Kwa nini malaika hawa wako katika mwendo hivi?” Yesu akanijibu, “Ni kweli malaika zangu wako kwenye mwendo hapa. Lakini nitakuonyesha jinsi ambavyo dunia nayo iko katika mwendo. Kuwa mwangalifu kwa sababu mapepo mengi yameshavamia dunia. Ibilisi ana hasira sana dhidi ya Wakristo kwa sababu amebakiwa na muda kidogo tu.”

Bwana aliniruhusu kuona mapepo yakiwa yenye hasira mno, na akaniambia, “Mapepo hayo unayoyaona ni mapepo ya uzinzi. Yatashambulia maelfu ya watumishi Wangu na wengi wataanguka kwenye dhambi hiyo. Unajua ni kwa nini ibilisi anafanikiwa kuwaangusha watumishi wangu? Ni kwa sababu watumishi Wangu hawanipi utukufu wote. Wanaiba utukufu wangu na kuwa na kiburi. Zaidi ya hayo, wake zao wanaishi katika mvurugiko wa kiroho. Hawakujenga nyumba zao kwa hekima.” (1 Tim 2:11-14).

Niliona maelfu ya malaika ambao sikuweza kuwahesabu wakiwa
tayari kwa vita. Kisha Yesu aliniambia, “Sasa nawatuma maelfu kwa maelfu ya hawa malaika duniani ili kuwalinda watu Wangu. Katika siku hizi za mwisho, ulinzi utakuwa mara dufu. Shetani naye pia atazidisha mashambulizi yake mara dufu, lakini msisahau kuwa Mungu wenu ni Mkuu na Mwenye Nguvu. Kama umejiungamanisha naye, hakuna kitu kitakachotokea kwako.”




Karamu

Kisha Bwana alinileta kwenye sehemu nyingine. Niliona meza kubwa imezungukwa na viti vya dhahabu. Kwenye kila kiti liliandikwa jina; na joho la kitani liliwekwa hapo. Mbele ya kila kiti, juu ya meza, niliona mataji.  Kisha niliona kuwa kulikuwa na kiti kikubwa kuliko vingine. Mbele ya kiti kile kulikuwa na kikombe kikubwa cha dhahabu. Yesu aliniambia nikachungulie nione kilichomo kwenye kikombe kile. Kilikuwa kimejaa mvinyo, tayari kwa kugawiwa. Yesu akaniambia, “Unajua ni kwa nini mvinyo uko tayari kugawiwa? Nenda kawaambie watu Wangu kwamba Mimi ndimi mlango. Ninakuja hivi karibuni.”

Bwana alinipa joho la kitani safi na taji. Nilivaa joho na taji lile na kwenda kwenye sehemu ambako kulikuwa na namna ya kioo. Yesu akaniambia, “Hakuna doa wala mkunjo kwenye joho lako, si ndiyo? Hakuna mtu atakayepita kwenye mlango huu wala kushiriki meza hii ambaye hajavaa kwa namna hiyo. Baadhi miongoni mwa watu Wangu duniani wameshachafua mavazi yao. Wengine wana mavazi yenye mikunjo, na bado kuna ambao wameyaweka pembeni ya kwao na kuyasahau. Waambie watu wangu kuwa ni wakati wa kuosha mavazi yao, kuyanyoosha na kuyachukua tena. Wakristo wanatakiwa kumwambia Roho Mtakatifu awasaidie kuyaweka mavazi yao katika hali nzuri, maana si muda mrefu Mfalme atasherehekea Karamu ya Harusi kwenye ufalme wa Baba Yake.” (Mathayo 22:1-14).

Familia yangu

Ninatokea kwenye familia iliyotalikiana na nimekulia kwa baba yangu. Mama yangu alikuwa ni muumini sana wa dini. Lakini baba yangu alikuwa haamini chochote. Nina dada yangu ambaye yuko kwenye nyumba ya utawa, lakini ninajua kuwa Yesu atamtoa huko hivi karibuni naye atahubiri Injili pamoja nami. Huwa ninaomba sana kwa ajili yake. Nilipokuwa ninatafakari juu ya maisha ya mama yangu kwenye dini hiyo ya ajabuajabu (mystic), wakati wa safari yangu ya kwanza paradiso, nililia mbele za Bwana na kumwambia, “Bwana, mama yangu amepotea, lakini nimeshahubiri Injili kwake naye hataki kusikia. Anaendelea tu kung’ang’ania zaidi na zaidi dini hiyo ya kipagani.” Bwana akaniambia, “Nitamwokoa mama yako, lakini nitamleta nyumbani mara moja, vinginevyo ataanguka tena dhambini na kwenda Kuzimu. Kwa sababu hiyo, mara baada ya kuokoka, atakufa muda mfupi baadaye na kuja hapa paradiso.”

Niliporudi duniani, niliomba, nililia, nilishusha pumzi na kumkumbusha Bwana juu ya ahadi aliyonipa, lakini nilimwona mama yangu akizama tu kwenye ibada ya sanamu ya dini yake. Siku moja Bwana alimtumia mwanangu wa kiume kumbadili mama yangu. Siku tatu tu baada ya kuokoka, alikufa!

Katika safari yangu ya pili paradiso Bwana aliniambia, “Tazama! Kile ambacho kinywa Changu kinasema, mikono Yangu inakitimiza.” Nilimwona mama yangu kwenye ile paradiso nzuri. Alikuwa miongoni mwa wanawake wengine. Tulienda mahali ambako niliona maelfu ya watoto wamevaa mavazi meupe wakimsifu na kumtukuza Bwana. Yesu akaniambia, “Watoto hawa ni wale ambao mimba zilitolewa na wazazi wao na madaktari wahalifu. Watoto ambao watu waliwaua wangali kwenye matumbo ya mama zao, na ambao wanakutwa kwenye mapipa ya taka na kwenye mito, wote wako hapa mbinguni.”

Wapendwa kaka na dada zangu, tofauti na vile ambavyo mnaweza kufikiri, kwa Bwana, mimba ikitungwa tu inakuwa ni binadamu tangu siku ya kwanza.

Yesu aliniambia tena, “Bernarda, fanya kazi maana Mimi ni nguvu zako. Ujumbe huu ni lazima uende duniani kote. Ni ujumbe kwa ajili ya Wakristo, wachungaji, na watu wote wakaao duniani, ikiwa ni pamoja na wewe. Yeye aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”

Wakati huo malango ya mbinguni yalifunguliwa. Kulikuwa na ngazi inayopanda yenyewe (eskaleta) nzuri sana. Yesu aliwaita maelfu ya malaika waje, kisha Bwana alinisindikiza kurudi nyumbani.

Tulipofika nyumbani, nilimwona mume wangu na ndugu zangu wa Kikristo wakiwa wanangoja roho yangu irudi. Niliutazama mwili wangu wa nyama, na nikamwambia Bwana kuwa sikuwa nauhitaji tena mwili ule. Bwana akaniambia, “Huwezi kurusi mbinguni pamoja nami, maana muda wako haujafika bado. Unatakiwa ukawaambie watu Wangu kwanza kile ulichokiona, ili kwamba wajiweke tayari.” Kwa sauti yenye nguvu, aliniambia, “Ingia na upokee uzima. Mimi ndimi ufufuo na uzima. Yule aniaminiye Mimi, hata ajapokufa, atakuwa hai.” (Yohana 11:25-26).
Mwisho wa ushuhuda.

………………………………..

Mpendwa msomaji wa blog hii kama ungependa kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza, bofya HAPA.

5 comments:

  1. Mungu akubariki kwa kazi nzuri. Ni ushuhuda mzuri sana unaotuonya siku hizi za mwisho, wakristo tumejisahau sana ni wahubiri wachache sana wanowakumbusha waumini zao juu ya kujiandaa kurudi kwa mwokozi wetu Yesu. Ki ukweli muda umeisha sana lakini wahubiri wengi wamejikita kuhubiri utajiri na kusahau misingi ya injili ya kuwaokoa watu wasiende jehanmu. Brother John kuna yale maswali uliulizaga ndugu zetu walikujibu? karibia mwaka sahvi unapita sioni majibu?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom Nicky. Asante kwa maoni yako. Bwana akubariki sana; tuzidi kusimama imara kwa Bwana tukimtanguliza Yeye katika mambo yote maishani mwetu.

      Kuhusiana na yale maswali ambayo niliuliza ndugu zetu waislamu, sijapata jibu hata moja hadi leo. Ukweli ni kwamba maswali hayo hawawezi kuyajibu kwa sababu Uislamu hauna majibu juu ya mambo yake. Ndiyo maana inabidi utumie kulazimisha mambo kwa kuwa akili ya kawaida tu haikubaliani na mambo yake.

      Na kusema kweli, sikuyaweka hapa ili wanipatie majibu (maana najua hawawezi kuyapata), bali nimeyaweka ili wajihoji na kujipima juu ya hayo wanayoyaamini; ili yamkini watambue hatari waliyomo na kuja kwa Mwokozi wetu na wao, Yesu Kristo, ambaye ndiye PEKEE njia, na KWELI, na uzima.

      Ubarikiwe na Bwana, Nicky.

      Delete
  2. Barikiwa mpendwa kwa kutuwekea shuhuda zenye kujenga IMANI ZETU. Mungu wangu azidi kukutumia katika huduma hii hujui wangapi wanabadirisha maisha yao na wangapi wanarekebishwa kiimani ila ni kusudi la YESU KRISTO ALIE HAI kufanya ujumbe wake upite kwa walio wake. MUNGU azidi kukubariki.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante sana Upendo kwa maoni yako yenye kutia moyo. Ubarikiwe sana na Bwana Yesu.

      Delete
  3. Amen nimebarikiwa na we uvarikiwe

    ReplyDelete