Thursday, May 24, 2018

Kubatizwa kwa moto uwakao - 14



==== SIKU YA 23 ==== (1 John 3:7-10)  
Mchungaji Kim Yong Doo: * Mama Kang, Hyun Ja alishambuliwa na mapepo baada ya kujisahau
Kwenye saa 5 kamili asubuhi, mke wangu, Joseph, Joo Eun, na mimi tulisimama mbele ya mgahawa unaotazamana na jengo la Chama cha Ushirika cha Kilimo. Mke wangu alipoanza kutembea, alishambuliwa na kuanguka chini. Alianguka kwa nguvu sana kwenye barabara ngumu ya lami, takribani mita tano kutoka kwangu, utadhani alikuwa anateleza kwenye barafu. Jambo hilo lilitokea kwa haraka sana, hatukupata muda wa kumdaka wakati alipotupwa hivyo. Alipiga kelele za maumivu na sote tukamkimbilia ili kumsaidia ainuke. Viganja vyake vyote vilikuwa vimechanika, kucha zimevunjika, na mikono ilikuwa imefunikwa na damu.


Tuliangalia kote hapo barabarani ili tuone ni kitu gani kimemwangusha kwa nguvu kiasi kile. Lakini barabara ilikuwa safi kabisa, tambarare na haikuwa na shida yoyote. Hatukuona chochote ambacho kingesababisha ajikwae.

Baadaye, Joo Eun alimwuliza Yesu kuhusiana na jambo hilo. Bwana akaeleza kwamba kwa kuwa ratiba yetu ya kila siku inahusu kwenda kanisani, kuomba, na kwenda nyumbani, hatuna muda wa kujiburudisha, matokeo yake, mapepo wachafu hawapati mwanya mkubwa wa kubaini ni wapi mna udhaifu. Hata hivyo, leo, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, familia yangu ilitoka nje ya huo utaratibu wetu wa kiroho ili kuwa na muda wa kujiburudisha.  Nje ya huo utaratibu ndipo pepo likapata mwanya wa kumshambulia na kumwangusha.

Yesu aligusa mikono ya mke wangu iliyoumia. Nami pia nikaanza kumfariji mke wangu. “Mke wangu mpendwa, hebu tumshukuru Mungu. Ni lazima tutubu kwa kulegeza nguvu zetu na tumshukuru Bwana. Atatupatia neema kubwa zaidi. Hebu tuvumilie na kushinda hadi mwisho.” Wakati nikimtia moyo, alipiga magoti na kumshukuru Bwana huku mikono yake iliyoumia ikiwa imeinuliwa juu.

Kwa kuwa mapepo wachafu wanatushambulia na kutuzuia kiasi hicho, niliamua kwamba wakati wote nitakuwa makini na mwangalifu. Mara tunapojisahau kidogo, mapepo wachafu wanashambulia. Kama tukipitisha siku moja bila kuomba, akili zetu zinadhoofishwa na zinaweza kushambuliwa kirahisi. Mapepo waovu wanakuwa wanasubiri kwa hamu sana nyakati za udhaifu. Kwa hiyo, ni lazima wakati wote tuwe tumejivika silaha kikamilifu.

Ushirika wetu wa maombi ulikuwa bado umebakiza wiki moja na mashambulizi yaliongezeka zaidi. Sote tulikuwa tunafunguliwa macho yetu ya kiroho mmoja baada ya mwingine. Adui alihofia hili sana, lakini mashambulizi yake yalikuwa dhaifu. Kadiri maombi yetu yalivyoongezeka nguvu, imani yetu nayo iliongezeka. Mapepo yenye nguvu zaidi yalitumwa na vita vyetu vikawa vikali zaidi.

Baadaye, niliangalia mguu wa Joseph, ambao ulikuwa na uvimbe wenye maumivu. Tulishaomba kwa nguvu sana kwa ajili ya uponyaji. Nilipatwa na mshituko mkubwa kwa kile nilichokiona. Uvimbe ambao ulikuwa ndani ya ngozi, sasa ulitokeza nje ya ngozi. Kwa macho yangu ya rohoni, niliweza kumwona Yesu akipaka damu yake kwenye wayo wa mguu wa Joseph. Nikasema, “Ha! Safi sana. Joseph, unatakiwa uende kwa daktari wa ngozi na kutoa ushuhuda wako.”

Baadaye, mke wangu alianza kukohoa na kutoa makohozi. Joseph, Joo Eun, na mimi tuliweka mikono yetu kwenye shingo yake na kuomba kwa bidii. Pepo mchafu kwa sura ya msichana mdogo mwenye nywele ndefu akiwa amevaa gauni jeupe alijidhihirisha kwetu. Pepo hili ndio lilihusika na kuanguka kwa mke wangu, na sasa lilikuwa linamshambulia shingoni, huku likimsababishia maumivu, kukohoa na kutoa makohozi.
Niliweka mikono yangu shingoni mwa mke wangu na kupunga mkono mwingine huku nikiomba. Mara pepo mchafu alipiga kelele, “Mchungaji Kim, ondoa mkono wako! Ondoa mkono wako mara moja! Acha kuomba! Aaah, joto ni kali mno. Nadhani nitachanganyikiwa!” Lilipiga kelele na kutoweka.

Yesu alikuja na kusema, “Wanangu, pepo mchafu amekimbia. Lakini kwa kuwa huyo pepo mchafu amebakiza athari za maumivu, itabidi uyavumilie kwa muda. Ukiomba mfululizo, utapona kwa haraka zaidi. Usiwe na wasiwasi.”

Kim Joo Eun:
“Yesu, je, nyumba na hazina zetu kule Mbinguni ni kubwa kiasi gani?” niliuliza. Yesu akajibu, “Kwa nini usifanye maombi ili uone wewe mwenyewe kule Mbinguni? Siwezi kukuonyesha kwa sasa. Kwa imani na bidii yako mwenyewe, kuwa na shauku ya kujua jibu hadi macho yako ya kiroho yafunguke. Mara hilo litakapotokea, njoo Mbinguni ili uje upate jibu.”

 “Yesu, maombi ya baba yangu yameshapiga hatua kiasi gani?” Bwana akanijibu, “Mchungaji Kim anapoomba, Roho Mtakatifu hujidhihirisha. Mikono ya mchungaji inajizungusha kwa namna tofauti. Hii ina maana kuwa kipawa cha uponyaji kimekuja juu yake. Hata hivyo, kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Mchungaji Kim, anaendelea kufungua macho yake wakati wa maombi. Kwa hiyo, maombi yake hayafiki kwenye kiti cha enzi, lakini yanabakia kwenye galaksi. Kama ataendelea kuomba na asijali mikono yake inavyojizungusha, baada ya muda mfupi atafunguka kiroho na kuwa na uwezo wa kutembelea Mbinguni.”

Bwana pia alitaja toba ya kaka Joseph kwamba ilikuwa dhaifu sana. Bwana alimwambia atubu kwa dhati kabisa na kwa moyo. Hata hivyo, Mungu aliridhishwa na toba ya machozi na maombi ya huruma ya mama yangu.

Nikasema, “Yesu, bibi yangu mzaa baba ni shemasi, lakini inaonekana kwamba anakunywa sana pombe.” Bwana akajibu, “Kuna pepo mchafu wa ulevi ndani ya bibi yako. Kila Mchungaji Kim anapopata nafasi ya kuomba, amwombee. Pia amwongoze akiri kwa ajili ya uhakika wa wokovu na imani.”

Mchungaji Kim: (Yakobo 4:4-5) * Wachungaji na washirika wa Kanisa wanaofanya uzinzi
Moyo wangu unauma kila wakati vyombo vya habari vinapoandika juu ya watumishi na kuanika wazi uchafu wao wa siri kwenye TV. Ama ninazima TV au kuchanachana gazeti kwa kuhofia familia yangu kujua mambo hayo. Nikiwa kama mtumishi, ninajisikia aibu na fedheha kubwa sana. Ninapata mkanganyiko. Nashindwa kujua nifanye nini. Ninajiona kana kwamba ni mimi ndio nimeandikwa maana hata mimi ni mtumishi. Sina shauku ya kujadili au kufunua uchafu wa siri wa watumishi wengine walioanguka. Hata hivyo, Bwana amenisukuma kuandika habari hizo kwa undani kwenye kitabu hiki.

Yesu aliamuru kwamba tusifanye kabisa uzinzi. Kati ya watu wasio na idadi wanaoenda Kuzimu, wengi wao ni wazinzi. Bwana alitukumbusha, “Je, washirika wa kanisa lenu hawakushuhudia wazinzi wakiteswa Kuzimu? Uzinzi ni dhambi iliyo ngumu sana kutubia.” Bwana anachukia watu wanaotenda uzinzi wa kiroho, lakini pia anawadharau hata zaidi wanaotenda uzinzi wa kimwili.
Watumishi wengi na washirika wa kanisa wanadanganyika kwa kufikiri kuwa wakitubu tu dhambi zao kwa Jina la Yesu, basi wanasamehewa kabisa. Matokeo yake, wanaendelea kutenda dhambi ileile, wanatubu tena na kufikiri kwamba wamefunikwa kwa neema. Wanaikanyaga neema na hawasiti kutenda dhambi ileile ya uzinzi tena na tena. Bwana anachukizwa na kudanganyika kwao. (Ufunuo 2:21-23). Kabla ya mtu kuja kwa Yesu, anatenda dhambi kwa kutokujua. Yesu anakasirika sana kwamba watu wameshamkubali kuwa Bwana wao, lakini wanaendelea kutenda dhambi tena na tena bila kusita. Bwana alipaza sauti kwa hasira, “Itakuwa vigumu sana kuwasamehe watumishi wanaotenda uzinzi kwa siri. Kama hawatatubu kwa dhati kabisa, wataishia Kuzimu.”

Niliomba kwa huruma, “Bwana, wao ni wanadamu; wao ni nyama. Bado wanaweza kuanguka na kufanya makosa, si ndio? Kama mtu akifa, hatakuwa na fursa ya kusamehewa. Lakini awapo mzima, hatasamehewa kama akitubu? Kuna aya nyingi kwenye Biblia zinazosema kuwa utasamehe, kama mtu akitubu.” Bwana akajibu, “Watumishi wanajua maandiko vizuri sana na iwapo watafanya uzinzi, watapata hukumu kali sana. Itakuwa ni vigumu kwao kusamehewa.”
Nikang’ang’ania kusihi rehema za Bwana huku nikigoma kuacha. Niliomba kama Ibrahimu alivyofanya. “Bwana, japokuwa uko sahihi, kama ukiwapeleka Kuzimu kwa ajili ya dhambi zao za zamani bila msamaha, itaonekana kuwa si halali. Miongoni mwa kundi hilo, huenda kuna baadhi ya watumishi ambao wanaongoza makanisa yao sawasawa. Je, baadhi yao hawako hivyo ndani ya kundi hili la wazinzi?” Bwana akanikemea kwa utisho, “Wewe kama Mchungaji, haujui maandiko yako?” Yesu alinisaidia kukumbuka (Wafilipi 2:12), “utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.”

Pamoja na Bwana kunikemea, bado nikaendelea kujadiliana na kumtolea hoja. “Bwana wangu mpendwa, wale watumishi wameyatoa maisha yao yote kwa ajili yako. Wametumia muda wao duniani kukutumikia wewe. Hudhani kuwa unatakiwa kuwapa nafasi ya kutubu? Kama nikisema wachungaji wanaenda Kuzimu, nani ataniamini?”

Kulikuwa na kimya cha muda. Kisha Bwana akaongea polepole na kwa hadhi. “Mungu Baba anakubaliana na mimi. Iwapo watumishi waliofanya uzinzi wakitubu kwa dhati kabisa na kwa hofu, watasamehewa. Lakini kama wakirudia njia zao mbaya na kutenda dhambi ileile baada ya kuwa wametubu, watakuwa wanamdhihaki Mungu! Haitajalisha kama wanaongoza huduma ndogo au kubwa; watakuwa wametenda dhambi ambayo Mungu anaichukia kuliko zote. Lazima ukumbuke hilo.”

Katika maono, Bwana alinionyesha mchungaji fulani ambaye aliangukia kwenye mahusiano na binti mmoja kanisani kwake. Mara nyingi walikutana kufanya mapenzi. Hatimaye, uhusiano wao ukajulikana kwa mama mchungaji. Mama mchungaji alipatwa na mshituko mkubwa sana kiasi kwamba akawa na msongo wa mawazo ambao ulikuwa wa juu na hata wa hatari. Alijaribu kumshawishi mchungaji atubu, lakini hakusikiliza. Mke hakuweza tena kuvumilia maumivu na mshituko ule, hivyo akawa na mfadhaiko mkubwa sana. Aliamua kujiua, uchaguzi ambao wasioamini huufanya. Hivi sasa yuko Kuzimu na anateseka sana.

Bwana akasema, “Kila ninapomwona huyo binti, moyo wangu unararuka kabisa. Kwa nini nisimpeleke huyo mchungaji Kuzimu? Mchungaji huyo bado yuko kwenye huduma. Toba yake haikuwa ya dhati. Hata leo, anaishi maisha ya uongo na kujidanganya. Namna yake ya kufikiri ni potofu. Hakuna mtu anayeweza kunidanganya mimi. Hakuna mtu anayeweza kufunika ukweli kwa kutumia uongo.”


* Kufuta majina kutoka kwenye Kitabu cha Uzima

Alikuwapo shemasi mmoja kanisani kwetu. Alipokuwa akiishi kwa uaminifu, alipokea vipawa vingi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Hata hivyo, vipawa vyote viliondolewa. Muda mfupi baadaye, alianza kulewa na kuvuta sigara mara kwa mara. Zaidi ya hayo, aliongea na mwanamume kwenye simu kila siku ambaye alienda kukutana naye kwa siri. Nilijaribu kwa bidii kumshawishi aache kukutana na mwanamume yule. Niliongea naye hata kwa ukali lakini bado aliendelea kukutana naye. Mungu ni mvumilivu kwa watu. Hata hivyo, kama watu hawatatubu, watakabiliwa na hasira yake. Mungu alinionyesha kwenye maono kwamba alishafuta jina lake kwenye kitabu cha uzima. Tulipojua hilo, sote tulitetemeka kwa hofu.

Mungu anapotupa nafasi, ni lazima tuitumie, haijalishi hali ilivyo. Yesu alisema, “Yule mtakatifu alimdhihaki Mungu na kumkasirisha Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, kama hataomboleza na kutubu kwa dhati kabisa, hataingia Mbinguni. Kama hukumu ya washirika ni kali, si zaidi nitakavyowahukumu wachungaji wanaozini? Wahudumu ni lazima watubu hata kufikia mauti.

Wahudumu wa leo wanamdhihaki Mungu. Wanasema, ‘hizi ni nyakati za neema na injili inatuweka huru. Wewe tubu tu na utasamehewa bila masharti.’ Hizi ni nyakati ambazo mtu anatakiwa kuwa katika hofu zaidi kuliko nyakati za Agano la Kale.”
Bwana alituonya kuwa siku inakuja tutakapotoa hesabu ya matendo yetu yote.
Ninapoandika sura hii, napitia saa nyingi za hofu na mfarakano. Yesu alisema, “Je, twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” (Warumi 3:31) Kimsingi, tunaishi maisha yetu ya kila siku ndani ya  neema ya ajabu ya Bwana. Hata hivyo, kuishi kwenye neema yake haimaanishi kuwa dhambi zetu zinapotea tu. Tutakuwa tunatumia vibaya neema ya Mungu kama hatutubu. Maisha yenye toba kila siku ndiyo njia ya haraka na fupi kwenda kwenye neema na huruma za Mungu.

* Watu wanaowapinga Wachungaji (Mamlaka ya Kiroho)
Inaweza kuonekana kana kwamba ninaandika kitabu hiki kutoka kwenye mtazamo wa kichungaji, maana mimi pia ni mchungaji. Lakini sina nia yoyote moyoni mwangu ya kuficha vitendo vya wachungaji wengine. Ninarekodi na kuandika kwa sababu nimeamriwa kufanya hivyo. Sitaki kuandika nikiwa nimeegemea upande fulani.

Bwana alisema, “Nawaadibisha watumishi wangu.” Zaidi ya hayo, Bwana alisema kuwa hawezi kutumia washirika kumwadibisha mchungaji wao. Yesu atawahukumu na kuwaadibisha kwa nguvu wale wenye dhambi za siri.

Bwana alitoa (1 Samweli 4:11-22). Bwana pia alisema hatakubali au kuvumilia vitendo vya waumini wa kanisa ambao wanajiunga pamoja kumpinga na kumfukuza mchungaji. Atawaadhibu vikali watu wa hivyo kama alivyofanya kwa Kora, Dathani na Abiramu katika (Hesabu 16:26-35).

Nilimsihi tena Bwana, “Yesu, wakati mwingine washirika huunda vikundi kwa kutojua na nia yao inaweza kuwa ni kuboresha kanisa. Kama ikiwa hivyo, kwa nini wahukumiwe?” Yesu akajibu, “Linapokuja suala la kanisa, hakuna anayeweza kusuluhisha hilo kibinadamu. Hiyo haitakubalika kamwe.”
Bwana aliongeza kwamba, iwapo mtakatifu alikosa kwa habari ya mamlaka ya kiroho kwa kumpinga mchungaji zamani au sasa, ni lazima atubu kwa hofu. Vinginevyo, atakuwa katika hatari ya kuingia Kuzimu. Baada ya hapo aishi kwa uaminfu, katika kweli na kwa umakini.
Wachungaji ambao waliruhusu washirika kukosa kwa habari ya mamlaka ya kiroho nao pia ni lazima watubu kwa dhati sana, kuliko hata waumini. Bwana alisisitiza kwamba waumini na wachungaji ni lazima wote watubu kwa kuogopa. Kama wangemwomba Yesu, angeingilia kati kusuluhisha matatizo yao.

(Ufunuo 2:1) * Bwana hutembelea makanisa duniani kote
Niliendelea kumwuliza Bwana, “Bwana, kuna mtu alisema kwamba wewe unaweza kutokea kwenye makanisa yote duniani kwa wakati mmoja. Je, hiyo ni kweli?” Bwana akajibu, “Kwa vile mimi ni Roho, sizuiliwi na hali ya kimwili ya dunia hii. Ninaweza kutokea mahali kote, wakati wowote, kwenye kanisa lolote au makanisa yoyote kwa mara moja. Siwi kwenye kanisa moja maalum kwa wakati mmoja. Ninaangalia makanisa yote duniani. Roho ni yuleyule. Roho haichoki. Kwenye kanisa lolote, mtu anapoomba, mara moja nasikia maombi hayo. Ninaweza kusikia yote na kuwa pembeni ya kila mtoto wangu kwa wakati mmoja. Kama mtu akiomba kwa bidii kubwa, macho yake ya rohoni yanaweza kufunguliwa na kwa nyakati fulanifulani, naweza kumwonyesha mtu huyo Mbinguni na Kuzimu. Mchungaji Kim, wewe na mkeo endeleeni kuomba kwa bidii juu ya macho ya rohoni. Wewe na mkeo pia mjifurahishe kwangu. Kwa kuwa mara nyingi, unalia kwa machozi na kuwa na shauku kubwa, ninafikiria kukupa upendeleo wa kuona Mbingu na Kuzimu. Ombeni kwa bidii. Mwanzoni, Mungu Baba hakuruhusu wewe na mkeo kuamshwa kiroho. Lakini kwa kuwa wewe na mkeo mna shauku kubwa juu ya hilo na mna ibada za kuabudu kila mapema jioni hadi asubuhi inayofuata, Mungu Baba aliguswa sana. Pia mmelia kwa namna isiyo ya kawaida. Mungu Baba alisema, ‘Sijaona watakatifu wengine kama wao.’ Alisema kuwa atawafungua macho yenu ya kiroho.”

Ziko namna mbili za kuamshwa kiroho. Ya kwanza ni kwa kufunguliwa macho ya kiroho na ya pili ni bila kufunguliwa macho ya kiroho. Makanisa mengi yameamshwa kiroho bila kupewa uwezo wa kuona ulimwengu wa roho. Karibu kila kanisa lina aina hii ya kuamshwa kiroho. Aina hii ya kuamshwa kiroho ni Roho Mtakatifu anatoa mawazo, hukumu, na maneno kwa mtakatifu kama inavyotakiwa.

Macho ya kiroho ya mtu yanapofunguliwa, yanaweza kuwa na mazungumzo na Yesu. Kule Korea, mbali na Kanisa la Bwana (the Lord’s Church), kuna waumini wachache wenye uwezo huu. Waumini hawa wana uwezo wa kuzungumza na Yesu pale wanapomtafuta na kumwita. Yesu alisema kuwa watu kwenye Kanisa la Bwana ambao macho yao yamefunguliwa wanayo fursa ya kuzungumza na Bwana mara nyingi.

Kim Joo Eun: (1 Yohana 5:1-5) * Kupambana na mapepo mbalimbali
Kwa jinsi nilivyoongeza bidii kumwomba Mungu kwenye ibada zetu, pepo lililojionyesha kama msichana lilisogea mbele yangu. Huku macho yangu  ya nyama yakiwa wazi, nililikimbilia na kulidaka nywele zake na kulizungusha bila huruma. Liliendelea kupiga kelele na nikalitupa kwenye kona ya chumba. Kisha, pepo lenye umbile la kivuli lilinijia. Kwa mara ya kwanza, sikuwa nimejua, lakini kwa msaada wa Bwana, niliweza kulikamata, nikalizungusha juu, na nikalikanyagakanyaga kwa miguu yangu.

Pepo lililofuata liliponijia, nililikimbilia na kulikamata miguu nikanyonga shingo yake, nikalipiga na kulikanyaga kwa miguu yangu. Lilivuja damu nyingi sakafuni. Kabla sijapumzika, pepo jingine lilitokea, ambapo nililipiga ngumi ya tumboni. Lililia na kukaa sakafuni huku likisema, “Aaagh! Tumbo langu!” Nilikamata baadhi ya nywele zake nikalikabidhi kwa Dada Yoo Kyung. Nikasema, “Dada, shika kwa nguvu hapa!” Dada akajibu, “Sawa, nimeliona!” Alilizungusha na kulitupilia mbali.

Ilionekana kana kwamba tunashambuliwa kwa nguvu zote leo. Kwa kawaida, huwa yanatokea tunapoanza kuomba kwa pamoja, lakini sasa inaonekana kama yanabadili mbinu zao na yanajaribu kutuzuia mwanzoni kabisa mwa ibada yetu. Kwa namna fulani, tunakutana na mapepo mengi yaliyovaa sura za wasichana leo. Pale mojawapo liliponijia tena, nililikamata na kulipiga makofi kwenye mashavu yote mawili na kuparua uso wake. Lilipiga kelele, “Aaagh! Naumia!” Nalo liliniparua, kitu ambacho kilinishangaza. Niliweza kuona wazi mahali ambako makucha yake yalipita mgongoni mwangu. Nilimwonyesha hata mchungaji na washirika wengine ili kuthibitisha kwa macho yao ya nyama.

Lee Yoo Kyung:
Nilipokuwa nikimsifu Mungu wakati wa ibada ya kuabudu, pepo lenye rangi mbili usoni lilinijia. Upande mmoja wa uso wake ulikuwa mweupe na mwingine mweusi. Pepo jingine lenye uso wa buluu liliungana nalo. Mara moja niliyakamata mapepo yake mawili na kuanza kuyazungusha juu bila huruma. Niliyatupa mbali yale mapepo yenye nyuso za rangi. Pepo lenye uso wa buluu halikuweza kustahimili nilivyolizungusha. Hivyo, kwa hasira likaparua upande wa nyuma wa mkono wangu. Na baada ya kuniparua, lilinifinya na kuning’ata. Nilijawa na hasira sana, nikalitupa mbali kadiri niwezavyo. Nilipotazama mahali lilikonifinya na kuning’ata, niliona alama nyeupe huku ngozi yangu ikiwa imebanduka. Kidole changu kilianza kuvimba kutokana na alama za kung’atwa.  Washirika walishuhudia alama kabisa na wakashangaa sana. Alama na majeraha kutoka kwa mapepo yaliuma sana. Nilianza kutokwa na machozi na nilijaribu kuvumilia maumivu yale.

Lee Haak Sung: *Joseph aumwa na nyoka
Yoo Kyung, Joo Eun na mimi tumeshafunguliwa macho yetu ya rohoni na tunaweza kuona shughuli za mapepo na roho ovu. Hata hivyo, Joseph anaonekana kuwa na mfadhaiko kwa sababu hana uwezo kama wetu. Joseph alisema kuwa, kila anapoanza kuomba mwili wake unahisi joto kama moto kutokana na kazi ya Roho Mtakatifu. Mara zote huwa anakaa karibu na mimi wakati wa ibada. Matokeo yake, kila ninapoomba, nafanya maombi maalum kwa ajili yake.

Wakati nikimwabudu na kumsifu Bwana tukiwa na Joseph, pepo lenye sura ya nyoka lilikuja taratibu kwetu. Lilimfikia Joseph na kujizungusha miguuni pake. Nikasema kwa sauti, “Joseph, nyoka anajiviringa mwilini mwako!” Akasema, “Nini? Sioni kitu chochote.” Nilimkamata yule nyoka shingoni na kumkabidhi Joseph. Nikapaza sauti kwa msisimuko, “Mshike kwa nguvu na umzungushe juu kisha umtupe chini!” Joseph alionekana amechanganyikiwa kwa kuwa hakuweza kuona kile nilichokuwa nakiona. Hakuweza kuelewa uhalisia wake. Akasema, “Kaka Haak Sung, Mimi sioni chochote!” Nikarudia tena kusema, “Joseph, mzungushe juu umtupe chini!” Alimkamata yule nyoka na kuanza kumzungusha.

Mtu yeyote ambaye angekuwa anatazama hali ile angeweza kudhani kuwa Joseph alikuwa anazungusha tu mikono mitupu hewani huku akijifanya ameshikilia kitu. Hata hivyo, kama mtu angekuwa na macho ya rohoni, angeshuhudia Joseph akimkamata nyoka shingoni na akimzungusha. Kusingekuwa na namna yoyote ya kuelezea tukio lile kwa ulimwengu wa kawaida bila ya kuwa na macho ya rohoni.

Kwa kuwa Joseph hakuweza kumuona huyo nyoka, alizungusha tu mikono yake hewani kiulegevu. Matokeo yake, nyoka aliweza kujiweka vizuri na kujiviringa kwenye mkono wake. Nyoka yule alimuuma mkononi. Kukaonekana alama kabisa za kuumwa na nyoka nyuma ya mkono wa Joseph. Kulikuwa na alama mbili za meno ya nyoka na zilianza kutoka damu. Mchungaji, kwa kugundua kilichotokea, alituambia tupande madhabahuni tukiwa na yule nyoka. 

Huku ameinua mkono wake, mchungaji alisema kwa sauti, “Kwa Jina la Yesu!” Kwa hayo maneno tu, yule nyoka alikatika katikati na kichwa chake kikapasukapasuka.  Huku nikiwa naangalia tukio lile, nilibakia nashangaa.

Leo, tumetumia muda mwingi tukipambana na mapepo waovu. Ama tulikuwa tukijilinda au tukishambulia. Tulitumia nguvu nyingi sana tukifukuza na kuyaondosha mapepo na kuyashinda. Hata hivyo, kila tulipoweza kuyakamata na kuyaleta kwa mchungaji, mapepo yale yalidhoofishwa na yeye. Mchungaji amebarikiwa kwa Moto Mtakatifu Unaowaka, na kwa amri yake, Moto Mtakatifu unatoka kwenye mwili wake na kuyateketeza mapepo maovu na yanageuka kuwa vumbi na kutoweka.

* Kuwinda mapepo
Tulipoyaona mapepo yote, tuliyakamata na kuyaleta madhabahuni ambako mchungaji alisimama. Aliyaharibu kwa Moto Mtakatifu Uwakao. Ilikuwa inachosha sana na ilionekana kana kwamba tunashambuliwa kwa nguvu zote. Kulikuwa na mapepo mengi sana na hatukuweza kuyahesabu. Haijalishi ni mangapi tuliyafukuza au tuliyashinda, makundi zaidi ya mapepo yalitokea. Kutokea kwenye madhabahu, Yesu alitutazama huku akifurahia jinsi tulivyopambana. Alikuwa amesimama mbele ya msalaba. Muda wa ibada ulipofika nusu, tulifukuza na kupambana na mapepo. Tulishavuruga kila kitu na hatukuweza kumaliza ibada. Sote tuliungana pamoja  kuyawinda mapepo.

Wakati wa mapambano hayo, Joseph alijeruhiwa maeneo matatu tofauti; sehemu mbili kutokana na kuumwa na nyoka na nyingine kutokana na kuparuliwa na pepo lenye sura ya msichana. Majeraha yake yote yalikuwa yakitoa damu. Niliweza kuona wazi alama za kung’atwa na kuparuliwa. Zilikuwa upande wa nyuma wa mikono yake.  Tulijaribu kupuuza majeraha ya Joseph ili kwamba asijisikie kunyanyasika. Sote tuliongea maneno ya kumtia moyo na kumwambia yalikuwa ni majeraha ya heshima ya vitani.

Kang Hyun Ja:
Katikati ya ibada, Haak Sung, Yoo Kyung, Joo Eun, na Joseph walipaza sauti, “Mchungaji! Mama Kang Hyung Ja! Kuna makundi ya mapepo yanayoshambulia kundi letu. Tufanyeje?” Mchungaji akawaambia, “Msiogope. Tuna Mungu wa Utatu upande wetu. Wote mtaweza kuyashinda kwenye mapambano.” Watoto walipaza sauti kwa msisimuko, “Haa! Safi sana! Mapepo machafu! Leo ndio mauti yenu!” Wote walikimbia huku na kule chumbani, wakipambana na mapepo yale.

Kwa macho yetu ya nyama, tuliweza tu kuona watoto wakikimbia huku wakitupa mikono yao hewani. Lakini kwa macho ya rohoni, tuliweza kuona kile ambacho hasa kilikuwa kikitokea. Nyakati za udhaifu, niliwaza, “Vipi kama watu wa makanisa mengine wangeona kinachofanyika hapa? Vipi kuhusu wageni au washirika wapya?” Hata hivyo, haikuwa muhimu kwangu kujisumbua na hayo kwa wakati huu. Wakati watoto wakikimbia huku na kule wakifukuza mapepo, niliomba kwa bidii kwa kunena kwa lugha na kucheza katika Roho. Nilihisi mkono wangu wa kulia umejaa nguvu na nikahisi kuwa nimeshika kitu fulani. Mkono wangu ulianza kujongea kwa mwendo wa duara, kama kataupepo. Mjongeo ule wa duara ukaendelea kuongezeka kasi na nguvu. Nikawaza, “Kitu gani kinaendelea?”

Sikupata muda wa kutafakari nini kilichokuwa kikiendelea. Kiganja na mkono wangu vilizunguka kwa kasi zaidi na zaidi na kwa nguvu zaidi. Sikuweza kuvisimamisha. Nikaona nisikae tu huku nikiona jambo hili likiendelea. Nilinyanyuka na kuanza kukimbia. Lakini mkono wangu ulikuwa bado ukijizungusha. Nilitupia jicho kwa Dada Baek Bong Nyu naye pia alikuwa akifanya vivyo hivyo. Bila kutarajia, mkono wangu uligonga kona ya kiti. Kwa mtazamo wa kimwili, sikuweza kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

Niliwauliza watoto ambao macho yao ya kiroho yalishafungiliwa, “Joo Eun, angalia mkono wa Mama. Kwa nini mkono wake unajongea katika duara? Kwa nini hausimami?” Huku akiwa na uso wa mshituko, alijibu, “Mama, umelikamata pepo mkononi mwako! Endelea kulizungusha ili uweze kulibamiza.” Japokuwa sikuwa na uwezo wa kuitawala hali ile kwa akili yangu, nilijaribu kuzungusha kwa nguvu zaidi. Mchungaji akasema, “Mama Kang Hyun Ja, njoo madhabahuni huku ukiendelea kuzungusha mkono.” Nilitembea kuelekea madhabahuni na mchungaji akasema kwa sauti, “Moto Mtakatifu!” Mkono wangu ulisimama wenyewe na pepo lilipigwa. Liliteketezwa kwa Moto Mtakatifu. Likageuka majivu.

Kwa kweli, ilikuwa ni tukio la ajabu na la kushangaza. Nikiwa naangalia, mapepo yote yalishindwa kabisa. Kwa mara nyingine tena nilitambua jinsi ambavyo uwezo wetu wa kiroho ulivyo mkubwa na wenye nguvu.

Kim Joo Eun: *Mapepo yanapogusa mwili wa mchungaji, yanasambaratika na kuwa majivu

Baada ya ibada ya jioni, wakati nikiomba kwa kunena, pepo moja lilinijia. Nililishinda kwa mamlaka ya Jina la Yesu. Hata hivyo, makundi mengi zaidi ya mapepo yalitokea, yote yakiwa yamevaa sura za wasichana wadogo wenye magauni meupe. Nilishangaa jinsi yalivyokuwa mengi, yasiyo na idadi. Yalitembea kwa makundi ya manne manne au matano matano na kujipanga katika mistari. Japokuwa yalionekana kama wasichana wadogo, nyuso zao hazikufanana; kila moja lilikuwa tofauti. Huku nikiwa nimezungukwa, niliamua kukamata lolote lililokuwa karibu yangu, nikalipiga na kuliparua. Japokuwa yalijaribu kukimbia, niliyakamata kirahisi na kuyazungusha juu kisha nayatupa kule kama wamasesere wa matambara. Niliyapeleka kwa mchungaji, ambaye alikuwa akiwaka moto. Yalimchukia na yalijawa na hofu kubwa. Kila nilipoyaleta kwa mchungaji, yaliteketea kabisa kwa kugusa tu mwili wake. Yalipiga kelele na kugeuka majivu. Mchungaji mwenyewe wala hakujua kuwa hayo yalikuwa yanatokea. Yeye aliendelea tu kuomba. Tulipofikia katikati ya mapambano, nilikasirika sana na kuwaza, “Leo nilikuwa nina shauku na nimepania kuomba na kumwuliza Bwana kama ningeweza kutembelea Mbinguni. Lakini haya mapepo yamenizuia hivyo sikuweza kuwa na uzingativu na kufanya haja zangu zijulikane. Sijaweza kutembelea Mbinguni leo. Nitamalizia hasira zangu kwa haya mapepo!” Niliyashinda yote yaliyokuja mbele yangu.

Kiroho, nilikuwa na siku ngumu sana; nilikutana na mamia ya mapepo. Baada ya muda mrefu, Yesu alitokea na akaenda madhabahuni ambako mchungaji alikuwa akiomba. Mchungaji alikuwa hajapona kabisa maumivu ya majeraha yaliyosababishwa na mapepo siku chache zilizopita. Aliendelea kuongoza ibada kanisani na kuabudu, licha ya hayo maumivu. Hata katika kuomba, alikuwa na maumivu na aliyedhoofika. Yesu alisimama karibu yake na kwa upendo alipitisha mikono kichwani mwake, mgongoni na mwilini, hasa mahali palikokuwa na majeraha. Kila Bwana anapomwona mchungaji, anakuwa mcheshi. Yesu anapenda kuwa na mchungaji. Yesu aliimba hata wimbo. “Licha ya majeraha, bado unaomba kwa bidii. Unafanya vizuri sana!” Bwana aliridhishwa sana. 

Nilipokuwa nikitazama haya, nilijisahau kidogo na pepo ambalo lilikuwa halionekani lilianza kunyonga mkono na kiganja changu cha kulia. Nguvu ya baridi ya pepo lile ilienea polepole toka kwenye ncha za vidole hadi juu ya mkono. Mara moja nilibinya mkono wangu wa kulia kuzuia ile nguvu ya baridi kusambaa. Nikasema kwa sauti, “Nakuamuru kwa Jina la Yesu, ondoka kwangu ewe pepo mchafu! Ondoka!” Ile nguvu ya ubaridi wa kipepo ikaanza kupotea taratibu. Kadiri nilivyoomba, nilipigapiga mkono wangu hadi ukawa katika hali ya kawaida tena.

* Jitihada za kiwazimu za Yoo Kyung za kuwinda mapepo
Pepo lenye uso mweusi na miili mitano iliyoungana lilinijia. Nililikamata na kuanza kulizungusha juu, huku nikiita Jina la Yesu. Pepo jingine kwa sura ya mwanamume aliyevaa nguo nyeupe lilitokea. Pepo hili lilikuwa refu sana. Lilionekana kama vile linaweza kufika mawinguni. Niliyazungusha mapepo yale mawili na kuanza kuomba kwa kunena. Nikiwa naomba, pepo lenye pembe kali kichwani lilianza kunidhihaki huku likiwa limekaa kwenye kinanda. Pepo hili lilikuwa na mkia mrefu na lilikuwa na mwonekano unaotia kinyaa. Niliweza kulikamata pepo hili nalo na lilishituka sana. Lilijaribu kukimbia kwa kutumia mabawa yake kama ya popo. Lakini nililikokota hadi chini na kuanza kulikanyaga kanyaga. Nililishambulia bila huruma.

Wakati nalipiga pepo lile, Bwana alikuja karibu yangu. “Oh, Yoo Kyung, unafanya kazi nzuri. Unalishinda pepo. Nilipanga kukupeleka Mbinguni na kukuonyesha sehemu za kule, lakini naona una shughuli kubwa ya kupambana na mapepo. Unaonaje?” Nikasema, “Yesu, nitatembelea Mbinguni baadaye. Acha niyashinde mapepo yote kwa sasa!” Bwana akasema, “Vizuri, yashinde mapepo yote na uwe mshindi.” Bwana alisimama karibu yangu na kuangalia. Mapepo yaliogopa hata zaidi na yalijaribu kukimbia yalipomwona Yesu.

Yesu alitembea kuelekea madhabahuni, ambako mchungaji alikuwa akiomba. Alipitisha mkono wake kichwani, hasa mahali ambako kunaota kipara. Bwana akaenda kwa Joseph na kwa upole, akagusa mguu na mwili wake.  Yesu alikuwa anagusa mahali panapouma. Sikufurahi sana Yesu alipoondoka karibu yangu. Nikapaza sauti, nikisema, “Abba, Abba!”
Mara Yesu alipoondoka, pepo lilitokea madhabahuni na likaja kuelekea kwangu. Nilikerwa na maneno yake ya kejeli. Nikajaribu kulipuuza, lakini liliendelea kunichokoza na kusema maneno ya kunitukana.  Hasira yangu ilikuwa ikijaribiwa. Nikajawa na hasira kali. Nikalikamata na kulizungusha juu. Pepo likaanza kulalamika, “Nasikia kizunguzungu. Naona kizunguzungu! Niachie!”
Nikabaini kuwa pepo lile lilikuwa na macho ndani ya jicho lake. Macho yote ya ndani yalikuwa yananitazama. Ilikuwa inatisha. Kwa sauti ya ukali nikasema, “Unawezaje kunikodolea macho hivyo!” Nikatia kidole kwenye jicho lake. Kwa vile pepo lile lilikuwa na macho mengi ndani ya jicho, ilibidi niingize kidole mara kadhaa. “Ah! Macho yangu! Macho yangu!” Pepo lilipiga kelele kwa hofu, lakini sikuliachia. Niliendelea kulizungusha juu tena na tena. Lilipiga kelele, “Niache! Niache! Usiponiachia, nitakung’ata!” Liliponitishia hivyo, nililizungusha hata zaidi. Pepo lile liling’ata mkono wangu kwa nguvu zake zote.

Mara liliponing’ata, niliachia na kulitupa mbali kabisa. Yesu alikuja karibu yangu na kunisifu kwa maneno ya kutia moyo. “Oh, Yoo Kyung wangu ana uwezo mkubwa wa kuyashinda mapepo. Wewe una akili sana!” Kwa upole alinishika mkono wangu na kuendelea kunitia moyo. “Yoo Kyung, naona kuna pepo jingine linakujia. Lishinde hilo nalo!” Bwana alisimama na kunitazama ninavyofanya vita na mapepo.
Pepo lenye umbo la mifupa mitupu lilitokea na kupaza sauti, “Twende Kuzimu na mimi!” Nilitikisa kichwa changu na kusema, “Hapana! Hapana!” Nikalikamata na kulitupa sakafuni kwa nguvu. Lilipiga kelele na kutoweka. Yesu akiwa amesimama karibu yangu, alipiga makofi na kusema, “Safi! Yoo Kyung wangu anafanya kazi nzuri sana! Imani yako hakika imekua sana.” Alibaki nami kwa muda, huku akinitia moyo.

Yesu alirudi Mbinguni. Niliomba kwa kunena kwa muda mrefu kidogo. Nadhani nilipambana na kuyashinda mapepo yapatayo 50 siku ile.

*Kubadilishwa kwa Haak Sung na upako wa Roho Mtakatifu  Idadi ya mapepo iliendelea kuongezeka zaidi. Yalitushambulia kwa makundi. Nitoboa macho yao, niliyachana, niliyapiga, na kuyazungusha juu. Kwa vile nina mikono miwili tu, sikuweza kujilinda wakati nikiyashambulia menyewe. Yalikuwa ni mengi sana. Nguvu zangu zilianza kupungua nilipofikiria, “Kama ningekuwa tu na Upanga Mtakatifu, ningeweza kuyashinda yote kwa uhakika kabisa.” Katikati ya mapambano hayo, mara nyingi niliwaza hivyo. Inanibidi niombe zaidi ili kupokea nguvu za Mungu. Pia nisome kwa bidii neno lake. Kama ningefanya yote haya, ningeweza kupokea upanga wa Roho Mtakatifu.  Kadiri nilivyoendelea kupambana na mapepo leo, nilitambua mambo mengi. Kadiri nilivyoyashinda, ndivyo mengi yalivyotokea na kushambulia yakiwa mengi. Sijui hata yanajificha wapi! Si tu mapepo mapya yanatokea na kushambulia, bali pia yale ambayo yalishindwa na Joseph, Joo Eun, na Yoo Kyung nayo yalirudi tena na kushambulia. Yalituzuia wakati wa saa za ibada na wakati wa maombi. Kimsingi tulishangazwa na idadi kubwa ya mapepo yaliyotushambulia wakati wa maombi.

Kama tai, yanazunguka juu ya mawindo yao huku yakizidi kuongezeka. Unapofika wakati wa kula, tai kwa idadi kubwa wanashuka kwenye mawindo yao.  Mapepo nayo yanashambulia kwa mtindo huo, yote kwa pamoja na yale ambayo yalikuwa hayaonekani, yanaonekana ghafla kutoka kusikojulikana. Yale yanayojificha, mara zote husubiri wakati mwafaka. Niliweza pia kumwona Shetani Kuzimu. Alikuwa akitoa amri kwa sauti kwa walio chini yake, wakati walipotumwa ili kuungana kwenye mashambulizi. Nilikuwa sijawahi kukutana na mapambano yenye mapepo mengi kiasi kile. Leo kulikuwa na makundi ya mapepo yaliyojishikiza kwenye dari na kuta za kanisa. Yalikuwa mengi sana kiasi kwamba hakuna kilichoonekana bali mapepo tu.

Nilimlilia Mungu anipe Moto Mtakatifu. “Mungu wa Utatu, tafadhali nipe Moto Mtakatifu! Moto unaoteketeza mapepo!” Mungu alinipa rundo la moto, ambalo kwa haraka liliingia ndani ya kifua changu. Mara tu Moto Mtakatifu ulipowekwa ndani ya mwili wangu, mapepo yalianza kunikwepa. Kabla moto haujaingia mwilini mwangu, nilikuwa nachoka sana. Mara tu baada ya ule moto uwakao kuingia, nguvu zangu zilinirudia. Nikawa na uwezo wa kuyawinda na kuyashinda mapepo. Nikasema maombi ya shukurani kwa Bwana. Nilikuwa na shukurani kwa kila kitu. Kisha, nikakumbuka siku ambazo nilivunja moyo wa mchungaji na kwa mawazo yale, machozi yalianza kujaa machoni mwangu.

Katikati ya kipindi cha maombi, mchungaji aliita, “Sam,” na mara moja nikaitikia kwa amen. Mchungaji aliongoza ibada yenye nguvu sana. Nilitambua kwamba nilibadilika moyo na roho yangu kwa haraka sana. Sasa ni mtu tofauti kabisa na nilivyokuwa miezi miwili iliyopita. Zaidi ya hayo, nimeamshwa kiroho na ninaweza kutabiri, kupata maarifa, kupata hekima, na nina nguvu katika imani. Ninapozungumza na Yesu, mara nyingi huwa nakiona kiti cha enzi cha Baba.

Japokuwa Roho Mtakatifu ni Roho, ninaweza kumwona kwa macho yangu ya rohoni. Napenda kuja kanisani; inaburudisha na kusisimua. Nafurahia kuwa kwenye ibada usiku kucha. Ni vigumu kwangu kuelezea furaha ninayoipata pale ninapofanya uinjilisti na kuomba. Ibada hufanyika usiku hadi mapema asubuhi, mara nyingi kwenye saa 12 au saa 1 asubuhi. Baada ya maombi, tunashuhudiana wenyewe hadi saa 11 asubuhi. Pia tunakaa pamoja kula mabumunda ya mchele. Mara baada ya kula chakula chetu cha asubuhi, tunaendelea kuomba kwa muda hadi jua linapoanza kuangaza. Baada ya maombi kwisha, mchungaji hutuendesha hadi majumbani kwetu. Yesu hutusindikiza hadi nyumbani. Haleluya!

Dada Baek Bong Nyu: *Mateso ya kusulubishwa yanasubiri Kuzimu

Nilipokuwa naomba kwa bidii kwa kunena, Yesu alitokea. Kwa haraka nilihisi amekuja kunichukua tuende Kuzimu. Ilionekana kana kwamba Bwana alikuwa anasitasita kuweka wazi safari hiyo yangu. Kabla ya Bwana hajaweza kuniuliza swali, mimi nilimwuliza, “Yesu, kwa nini unasitasita? Najua unataka kunipeleka kutembelea Kuzimu tena, si ndio?” Bwana alinionyesha ishara ngumu. Hata hivyo, sikuweza kumkaidi Bwana. “Yesu, kama hutanionyesha watu wa familia yangu wakiwa kwenye mateso, nitakufuata hadi mwisho wa Kuzimu. Sitaki tu unionyeshe familia yangu wakiwa kwenye mateso.” Bwana alinishika mkono na hakusema neno.

Kama kawaida, mara Bwana aliponishika mkono, tayari tukawa tuko Kuzimu. Tukaanza kutembea kwenye barabara nyembamba. Baada ya muda mfupi, harufu ya maiti ikaanza kujaa hewani. Tulifika kwenye eneo pana. Kulikuwa na misalaba iliyopangwa mstari usio na mwisho. Misalaba yote ilikuwa imechimbiwa chini sana ardhini. Kulikuwa tayari na watu wengi wamening’inia kwenye misalaba ile na wengine wengi kwenye mistari mirefu wakisubiri kusulubiwa. Mama yangu alikuwa miongoni mwa kundi lile akisubiri kupigiliwa misumari kwenye msalaba. Alikuwa amesimama chini ya msalaba mmojawapo usiokuwa na mtu.

Kiumbe mkubwa wa kutisha alikuwa akiilinda misalaba ile. Ilipofika zamu ya mama yangu, kiumbe kile kilimfunga mama yangu kwenye msalaba na kumwandaa kupigiliwa misumari. Kiumbe kile kilinitupia jicho na kilipomgeukia mama kikasema, “Mwambie binti yako aache kwenda kanisani na aache kumwamini Yesu sasa hivi. Vinginevyo, utakufa leo hakika!” Mama yangu alionekana ameogopa sana. Kiumbe kile kiligeukia kwangu na kusema kwa sauti, “Ukisema kwamba utaacha kumwamini Yesu, nitamwacha mama yako na sitamtesa. Sema kuwa utaacha kumwamini!” Kilijaribu kufanya mapatano na mimi. “Sema sasa! Toa kiapo chako! Fanya haraka!” kiumbe kile kiliamurisha. Hali ilikuwa tete sana. Kiumbe kile kilikuwa na mwili wa mwanadamu na kichwa cha farasi. Kilikuwa kibaya cha kutisha. Sikuweza kukitazama moja kwa moja machoni.

Kiumbe kile chenye kichwa cha farasi kilitoa upanga mkubwa unaomeremeta na kuwaamuru walio chini yake. Hao walitii haraka haraka. Halafu kiumbe kile kilimlazimisha mama yangu. “Haraka, mwambie binti yako! Sasa! Kuzimu kumechafuka kwa sababu ya binti yako. Kanisa ambako binti yako anasali linaomba usiku kucha. Tunazuiliwa kwa kila njia. Wanadamu wanaotakiwa kuja Kuzimu wanaenda kanisani na sisi tumevurugikiwa. Haraka! Mwambie binti yako aseme sasa! Mchungaji wake anaandika kitabu ambacho kitasababisha tutambulike na Kuzimu kujulikane. Ni lazima tumzuie kuandika kitabu hicho. Sasa, haraka mwambie binti yako atoe kiapo!”

Machozi ya mama yalitiririka mfululizo mashavuni mwake huku ananitazama mimi. Kwa kuwa Yesu alisimama karibu yangu, mama yangu hakuweza kusema neno. Aliinamisha tu kichwa chake na kuendelea kulia. Kiumbe kile kiliishiwa uvumilivu na kikalipuka kwa hasira. Mama yangu alivuliwa nguo na kuning’inizwa msalabani. Walimning’iniza kwa nguvu kwa kamba msalabani. Baada ya muda mfupi, kaka yangu mdogo na mpwa wangu nao waliletwa na kuvuliwa nguo. Nao walining’inizwa kwenye misalaba pia. Kiumbe kile kiovu bila huruma kilianza kuwapigilia misumari kwenye misalaba. Kisha kilianza kukatakata nyama za miili yao.

Nyama za miili zilikatwa kuanzia juu ya kichwa hadi chini kwenye vidole. Miili yao ilikatwa hadi ndani kabisa kwenye mifupa. Nyama za watu wa familia yangu zilitupiwa ndani ya chungu cha mafuta yanayochemka. Chungu kilichemshwa kwa moto mkali sana. Mama yangu, mdogo wangu na mpwa wangu walibakiza tu macho na masikio kwenye mifupa yao. Kila kitu kilikatwa. Katika hali yao hiyo iliyotia huruma, walikuwa bado na uwezo wa kupaza sauti, “Bong Nyu, ondoka haraka! Tulishakuambia usije huku tena. Kwa nini bado unaendelea kuja? Je, huoni uchungu unapotuona tukiteseka hivi? Tafadhali, usirudi huku tena!”
Huku nikilia, nilisema kwa sauti, “Mama, maskini mama yangu! Baada ya kuja mara tatu zaidi, sitakuja tena hata kama nikitaka kufanya hivyo. Yesu alisema mara safari ya tatu itakapomalizika, hatanileta hapa tena moyo wangu uko kwenye mateso ninapowaona mko kwenye mateso hivi! Kiumbe kile kiliingilia kati na kusema kwa sauti kama radi, “Nitakuambia mara ya mwisho! Hii ni nafasi yako ya mwisho! Mwambie binti yako aache kumwamini Yesu. Haraka! Mlazimishe aache kuomba na kwenda kanisani! Haraka!” Kiumbe kile kilivyoendelea kumsumbua mama yangu, niliongea kwa niaba ya mama yangu. “Ewe kiumbe mwovu! Kama una chochote cha kusema, ongea na mimi. Kwa nini unamtisha mama yangu? Nikikukamata, ujue umekufa!” Nilipokikemea kiumbe kile, kilimkimbilia mama yangu mbio kama risasi. Kiumbe hicho kikamchuna ngozi ya kichwa, kikakata masikio yake, na kunyofoa macho yake. Mama alipiga kelele kwa uchungu, “Nisaidie! Tafadhali!” Sikuweza kuvumilia zaidi kuona mama yangu akiwa kwenye maumivu. Hakuna maneno yanayoweza kuelezea hali hii ya kusikitisha! Kaka yangu mdogo na mpwa wangu nao walipatwa na hayohayo yaliyompata mama yangu. Kiumbe kile kilitupia sehemu za mwili zilizobakia kwenye chungu cha mafuta yanayochemka. Kutokea kwenye chungu hicho, niliweza kusikia vilio vya maumivu vya familia yangu.

Hasira za kiumbe kile hazikuisha. Safari hii, kilijaza chombo kikubwa kwa wadudu na kukiweka chini ya wanafamilia yangu. Kwa haraka, wale wadudu walianza kuwaguguna na kuwatafuna, waliingia ndani ya mifupa. Familia yangu walipiga kelele sana. Ilionekana kana kwamba mama yangu alikuwa akipata maumivu makali zaidi.
Mama alipiga kelele, “Ibilisi! Mimi tayari nimekufa! Kwa nini unamtesa mtu aliyekufa? Ibilisi, ondoa wadudu hawa! Sitisha maumivu haya! Tafadhali!” Japokuwa nilijua haiwezekani, bado nilimwomba Yesu, “Yesu, mateso yao yataisha lini?” Nilikuwa nalia kwa huzuni. Yesu alisema, “Mara unapoingia Kuzimu, hautaweza kuponyoka au kupata nafasi nyingine. Utakuwa kwenye mateso milele yote.”

Niliomba huku nimemng’ang’ania Bwana, nikilia, “Yesu, mama yangu atakuwa kwenye maumivu milele Kuzimu. Nitawezaje kuishi kwa furaha Mbinguni? Siwezi tena kushuhudia mateso ya mama yangu. Tafadhali, acha mimi nichukue nafasi yake ili yeye aokolewe!”  Kwa haraka Yesu aliwaita malaika. Kidogo nipoteze fahamu kutokana na mshituko wa hali ilivyokuwa. Kwa amri ya Bwana, Malaika mkuu Mikaeli na baadhi ya malaika wengine walikuja na kunirudisha kwenye Kanisa la Bwana. Yesu alimwita hata Musa na kumwambia anifariji. Yesu na Musa nao walikuwa wameumia mioyo. Walinikumbatia na kufuta machozi yangu na kunifariji. Walipoona machozi yangu yakitiririka, walihuzunika pamoja na mimi.

No comments:

Post a Comment