Sunday, November 12, 2017

Kubatizwa kwa moto - 9

 ==== SIKU YA 18 ====      (Petro 5:6-10)
Lee, Haak-Sung: * Kushambulia Mapepo moja kwa moja!
Wakati wa mahubiri ya jioni, mchungaji alituambia, “Mapepo yakija, msiogope bali piganeni nayo uso kwa uso! Mapepo hayo machafu si lolote, kwa hiyo msiyaogope. Ukizama ndani kabisa ya ulimwengu wa roho na kuomba kwa ujasiri, utakutana na upinzani [toka kwa mapepo]. Ikitokea hivyo, likamate na kulichana vipandevipande; liharibu kabisa!” Nikawaza moyoni mwangu, “Tunawezaje kufanya mambo kama hayo kwa mapepo haya yanayotisha kiasi hiki? Mchungaji naye atakuwa anazidisha chumvi mno bwana.”  


Lakini mchungaji alirudia kusema hivyo tena kwa kujiamini kabisa, “Tunaweza kufanya hivyo! Tumeshashambuliwa na tumekabiliana na ubaya mwingi. Ni wakati wetu sasa kulipa kisasi na kuwashambulia wao.” Kisha akatuonyesha kimwili namna ya kuwashambulia mapepo moja kwa moja.
“Tunaweza kweli kuyakamata mapepo?” niliwaza. Hadi sasa, tulikuwa na uwezo wa kutumia Jina la Yesu kama silaha, lakini tuliambiwa tunaweza kukabiliana na mapepo kwa kuyakamata kabisa moja kwa moja!

Baadaye, wakati nikiomba kwa kunena, mapepo mawili yaliyokuwa yamekuja mwanzoni, yalirudi. Moja lilikuwa limejaa misuli na jingine lilikuwa na nyuso nyingi. Lilikuwa limeshikilia unyoya wa tausi, na kama mwanzo, lilitumia upande ulio laini  wa unyoya kunitekenya puani. Nikakumbuka mahubiri ambayo mchungaji aliyatoa jioni ile. (Yakobo 4:7). Nikanyoosha mkono wangu wa kimwili kuashiria kuukamata ule unyoya kutoka kwa lile pepo. Niliwaza, “Oh, inawezekanaje? Unyoya ule ulikuwa sasa mkononi mwangu!” Ilikuwa ni ajabu kweli.

Nikaanza kulichomachoma lile pepo kwa upande wa unyoya wenye ncha.  Pepo likapiga kelele , “Aaaa!” Kwa haraka nikalishambulia kila sehemu, huku nikilichomachoma bila huruma. Likalia, “Aaaa! Niokoe!” Majimaji ya kijani yakatoka kwenye matundu niliyolitoboa. Lazima ilikuwa ndiyo damu yake. Pepo jingine lilipoona hivyo, liliogopa sana. Likakimbia kwa hofu.

Mchungaji Kim aliendelea kuomba, huku akivumilia maumivu ya vidonda ambavyo mapepo yalimsababishia. Yesu alimkaribia na akaendelea kuvigusagusa vidonda vile kwa mikono yake. Yesu alikuja kwangu na kusema, “Haak-Sung, usishushe mikono yako ijapokuwa unajisikia ugumu. Maombi yanayofanywa huku mikono imeinuliwa juu yana nguvu zaidi sana.”

Kim, Joo-Eun:
Leo kulikuwa na mapepo mengi yenye sura za ajabuajabu na yaliendelea kunitokea mfululizo. Nilipiga kelele, “Enyi mapepo, kwa Jina la Yesu, kimbieni.” Yalitoweka. Nikaendelea kuomba. Ghafla, pepo la kiume lililoonekana lenye nguvu lilitembea kuelekea kwangu huku likisema, “Wewe, acha kuomba. Wewe mtoto mdogo tu lakini unaomba mno.” Nikasema, “Wewe, shetani mchafu! Kwa Jina la Yesu, ondoka kwangu!” Shetani lile likatoweka.

Kadiri nilivyoendelea kuomba, likaja pepo lenye sura ya mwanamke mzuri. Pepo hili lilikuwa zuri na kuvutia kiasi kwamba sikudhania ni pepo mchafu. (2 Wakorintho 11:14-15). Hata namna lilivyoongea, ilikuwa ni nzuri sana. Likasema, “Tafadhali usiombe. Kwa nini unaomba?” Nikalipuuza na likakasirika. “Wewe, kwa nini unaombae? Ukiomba, je, unaona kitu chochote maalumu?” lilisema kisha likasema kwa sauti, “Acha kuomba!” Na mimi nikapaza sauti, “Kwa Jina la Yesu, ondoka kwangu,” na mara moja likaanza kuchanika katikati kuanzia juu kichwani hadi katikati ya miguu. Nikajisikia kinyaa, nikasema, “Aaagh, baya kabisa!” Mwili ule ulipogawanyika katikati, ndipo ndani yake kukaonekana pepo baya. Bado siwezi kusahau ukweli kwamba, mwonekano wake wa nje ulikuwa tofauti kabisa na wa ndani.

Baadaye, niliona pepo lililoonekana kama katoto ka kiume ambako huwezi kudhania kana ubaya wowote. Kalikuwa kamejifunga kitambaa chekundu shingoni. Kalikuwa na uwezo wa kufanya mauzauza makubwa kwa kutumia macho yake. Nilijaribu kukafukuza , lakini kapepo kale kaling’ang’ana na hakakushtuka kirahisi. Nikaendelea kuomba, huku nimeuma meno. Ndipo kakatoweka.

* Kubatizwa kwenye Moto Uwakao
Nilitambua ni mapepo aina ngapi yalikuwapo. Nilishuhudia yakiwasumbua washirika wengine. Yalifululiza kuja na kuondoka, na yalikuwa yakipitapita kwa vurugu kubwa. Wakati naendelea kuomba, nikajiuliza, sijui Mchungaji Kim atakuwa anaendeleaje. Nikageukia upande wake na, badala ya kumuona yeye, niliona moto mkubwa unawaka kwenye sehemu anakokuwa. Kutokana na mshangao, nilifungua macho yangu ili kuwa na uhakika na kile nilichokuwa nimekiona. Lakini nikamuona Mchungaji Kim amekaa kwenye kiti chake kama kawaida, akiomba. Nilipofumba macho yangu tena, nikauona tena moto mkubwa umezingira sehemu hiyo. Mapepo yalikuwa yamesimama pembeni ya mchungaji wetu, huku hayana uwezo wa kumshambulia. Kwa hiyo, yakaondoka kwenda kuwashambulia washirika.
Ghafla, pepo la kike lenye nywele ndefu lilitokea na kuniuma mkono wangu wa kushoto kwa meno yake kama ya joka. Nilijaribu kulisukumia mbali, lakini sikuweza. Sikuweza kufikiri sawasawa kwa sababu maumivu yalikuwa makali sana. Kisha, pepo jingine tena likanishambulia. Nikaita, “Bwana, Bwana, nisaidie. Tafadhali nisaidie!” Nilisogea karibu na mke wa mchungaji na nikaendelea kuomba huku mikono yangu ikiwa imeinuliwa juu. Karibu mapepo 100 yalikuja ili kunifanya nishindwe kuomba. Nami nikajibu mapigo kwa kusema kwa sauti, “Enyi mapepo machafu, kwa nini mnaishi kwa namna hii? Kwa nini mnanighasi?” Pepo moja lenye meno makali likakimbia kuja kwangu huku likisema kwa sauti, “Tunataka tukupeleke kuzimu.” Nikajibu, “Nini? Kuzimu? Unachekesha! Enyi mapepo wachafu, ondokeni kwangu. Kwa Jina la Yesu, ondokeni kwangu!” Palepale, yote yakatoweka. Nikagundua kuwa kama nina shauku ya kutembelea Mbinguni, basi inanibidi kupigana kwelikweli dhidi ya nguvu za kipepo.

* Wachungaji walioacha huduma yao ya uchungaji
Niliendelea kuomba kwa muda mrefu, kisha Yesu alinitokea na kuniita kwa jina langu la utani, “Ufuta! Mpendwa wangu Ufuta. Unaweza sana kuwafukuza mapepo wachafu!” Nikajibu, “Yesu, nimekumbuka jambo ambalo baba yangu alipenda kukuuliza. Kuna wachungaji ambao wameacha uchungaji na kurudi kwenye kazi za kidunia. Kitu gani kitatokea kwa wachungaji hao?” Yesu akajibu japo hakuwa tayari sana kujibu hilo, “Wewe bado mdogo sana kukuelea jambo hili, lakini nisikilize vizuri na ukamwambie vilevile kama nitakavyokuambia.” Akaendelea kusema, “Wachungaji wanaoacha uchungaji kutokana na ugumu wake watahukumiwa vikali sana na Baba yangu wa Mbinguni. Baba wa Mbinguni atawakemea, ‘Kwa nini mliacha kuwa wachungaji? Niliwapa nguvu za kufanya kazi ya uchungaji, lakini kwa nini mlifanya uamuzi wa kuacha bila idhini yangu? Mmefanya kosa kubwa.’ Lazima mtubu! Kisha, kwenye maisha yake yaliyobakia duniani, ni lazima afuate kwa utii njia pamoja na Mimi. Kuna pia watu wanaoshindwa kutunza kitakatifu Siku ya Bwana, na wanafanya yoyote wayatakayo. Wale ambao hawajaokoka hufungua biashara zao. Haitakiwi kabisa kufanya biashara yoyote siku ya Jumapili. Wengi wanakiri wokovu kwa midomo yao tu, lakini wana makosa sana. Kama kweli wameokoka, maisha yao ni lazima yaonyeshe hivyo! Baba yetu wa Mbinguni anawatazama sana kila mmoja wenu. Kwa Baba, kila roho ina thamani sana; na roho inapoenda kuzimu kwa kuamua yenyewe, anaumia sana. Anatokwa na machozi mengi!”

* Wale wanaowafukuza wachungaji (Yakobo 3:16)
Kisha nikauliza, “Yesu, wakati mwingine kwenye TV naona makanisa yakigombana na mchungaji na kwa kweli inanifedhehesha sana. Kwa nini washirika na wachungaji wao wanagombana? Katika hali kama hiyo, Wewe unakuwa upande gani?” Yesu akasema, “Wewe bado mdogo, hata hivyo mara nyingi unauliza maswali hayo.” Nikajibu, “Bwana, mimi ni binti wa mchungaji. Ninasikitishwa sana kuona mchungaji akifukuzwa nje ya kanisa!” Yesu akajibu, “Mara nyingi mchungaji anafanya makosa na hilo ni tatizo. Cha muhimu zaidi, washirika wanapomchukia na kumfukuza mchungaji, wanakuwa wametenda dhambi kubwa sana. Hata kama mtu alitenda dhambi huko nyuma, kama wakitubu kwa kumaanisha na kumfuata Mungu, bado wanaweza kuingia Mbinguni. Wasirudie kutenda dhambi hiyo tena!” (Wafilipi 2:3)

Nikaendelea kuuliza maswali. “Yesu, sote tunaomba kwa pamoja, lakini kwa nini unawachukua dada Baek na familia yake peke yao kutembelea Mbinguni na Kuzimu? Sisi ni familia ya mchungaji, si ndio? Familia yangu inaonekana kuwa na imani zaidi, lakini kwa nini wewe Bwana, unawapenda tu Haak-Sung, Yoo-Kyung na Dada Baek, Bong-Nyo?” Yesu alilipuka kwa kicheko kwa sababu ya swali langu na akajibu, “Mpendwa wangu Joo-Eun, hiyo si kweli. Wao wana maisha magumu sana. Haak-Sung na Yoo-Kyung wote wana matatizo ya kisaikolojia, si ndio? Pia, Dada Baek, Bong-Nyo amelala kitandani tu, akiwa na maumivu ya mgongo. Hawana chakula cha kutosha na wanaishi kwenye kichumba kidogo tu cha chini, lakini wanaomba bila kukoma! Hawajui ni lini watafukuzwa waishie mitaani, lakini bado wanamwomba Mungu kwa utii. Nawapenda, hasa kwa sababu licha ya matatizo waliyo nayo, bado wana bidii ya maombi! Wanahitaji ulinzi wangu! Wewe una ndugu wengi, lakini wao hawana hata baba au mume. Hii ndiyo sababu wanahitaji uangalizi maalumu!” (Kutoka 33:19)
“Yesu, mchungaji wetu anarekodi mambo yote haya kwenye kitabu. Kitabu kitakapokamilika, je, utatuondolea vipawa vyote vya kiroho ulivyotupa?” Bwana akasema, “Joo-Eun, kipawa cha unabii ni cha muhimu sana na ambacho huwa hakitolewi au kuondolewa kirahisi. Kipawa cha unabii kinaondolewa pale tu Baba yako wa Mbinguni anapoamuru iwe hivyo. Vinginevyo, kinaachwa kama kilivyo.”

Lee, Yoo-Kyung: * Mapepo yanaogopa imani yako
Leo, nilishambuliwa na pepo linalotisha sana ambalo lilijionyesha kwa sura nyingi tofauti. Baadaye nikamwambia Yesu, “Yesu, mapepo yanatisha kweli!” Akasema, “Yoo-Kyung, unaweza kuyashinda mapepo. Mapepo yanaogopa imani yako, kwa hiyo usiogope. Wakati wote malaika wapo hapa kukulinda.”

Sister Baek, Bong-Nyo: * Kujulikana kwa mapepo yasiyo na umbo maalumu yaliyomshambulia Mchungaji Kim
Nilikuwa naomba kwa nguvu kwa kunena kwa lugha, lakini sikuweza kuona chochote. Kila kitu kilikuwa giza kabisa. Nilijitahidi kuingia ndani kabisa ya ulimwengu wa roho, kwa hiyo niliomba kwa sauti zaidi. Niliona vitu vya umbo la duara, vikizunguka na kuzunguka. Nilidhani vinaweza kuwa ni aina ileile ya mapepo ambayo yalimshambulia kwa nguvu mchungaji wetu. Nilitaka kuyakomesha na menyewe. Kwa hiyo nikaongeza uzingativu zaidi. Yakakusanyika karibu yangu ili kuniharibia uzingativu wangu. Nikamwomba Yesu kwa bidii, naye akasema, “Yatazame kwa makini.” Yalionekana kama chapati ya dengu. Yalikuwa takribani 20 yakizunguka kwenye kanisa lote, huku yakiafuta fursa. Yesu akasema, “Yalikuwa ni mapepo haya ya hovyo ndiyo yaliyopindisha mkono wa Mchungaji Kim jana. Niliyachukua yote na kuyatupa kwenye shimo lenye moto la kuzimu, lakini yamerudi tena kushambulia watumishi wangu. Bong-Nyo, unatakiwa kuwa makini sana!”

Nilijulishwa kwamba mfalme wa mapepo alitoa amri ya siri, “Kuna mshirika kwenye Kanisa la Bwana mwenye kipawa cha macho ya rohoni, anayeitwa ‘Baek, Bong-Nyo’ na anaweza kututambua sisi ni nani. Fanyeni bidii kumshambulia mwanamke huyo!” Kama Bwana asingenifunulia mapepo haya, ingekuwa vigumu kuyaona hata kwa kutumia kipawa cha macho ya rohoni. Bwana aliniambia kwamba nikiomba kwa kuzama sana, nitaweza kuyaona mapepo hayo ambayo hayana umbo kamili.  Nikiomba kwa nguvu, mapepo hayo yatatambulikana na yatatoweka.

* Malaika wakuu Mikaeli na Gabrieli
Malaika wawili wazuri sana walikuja ili wanisindikize hadi Mbinguni. Walikuwa ni Mikaeli na Gabrieli. Hawa hawawezi kulinganishwa na malaika wengine wowote.  “Mpendwa wetu Yesu ameamuru kwamba dada Baek, Bong-Nyo asindikizwe. Kwa hiyo, tumekuja wenyewe.” Niliguswa sana na jinsi ambavyo Bwana anamtendea kipekee mtu kama mimi asiye na chochote. Sikujua hata cha kufanya. Sikuweza kuficha furaha yangu na kwa shauku kubwa nikawafuata.

Kule Mbinguni, Yesu alinionyesha Bustani ya Edeni, ambayo ilikuwa nzuri sana. Katika mazungumzo yetu, Yesu aliniambia, “Bong-Nyo, ilikuwa kazi ngumu sana kuwatoa mapepo waliokuwa wameingia ndani ya Mchungaji Kim jana. Utakuwa umechoka sana. Mapepo waliokuwa ndani yake ni kama kupe wanaokung’ang’ania na hawataki kutoka. Wale mapepo wanaficha mwonekano wao na kujigeuza miili yao ili iweze kuvutika na kurudi kama mpira. Baada ya mkutano, Mchungaji Kim alikokota mwili wake wenye maumivu ili kumuendesha dada Shin Sung-Kyung hadi nyumbani. Hawa wanakondoo wadogo wana moyo wa kumlinda mchungaji wao. Mara nilipoona hili, niliguswa sana na nikaamua kuungana nao.” Akaendelea kusema, “Pepo la mwisho lililokuwa limeganda ndani ya Mchungaji Kim na lilikuwa limedhamiria kumtesa kwa muda mrefu kadiri liwezavyo. Ilibidi nitumie nguvu kulitoa. Kwa bahati mbaya, kwenye kanisa lako, miongoni mwa wanakondoo hao wachanga, ni wewe tu mwenye uwezo wa kuona hadi Kuzimu. Najua ni ngumu kwako, lakini nitafurahi kama utakuwa na subira. Hivi sasa, mchungaji wako, Kim Yong-Doo anatakiwa kuandika na kuweka kama kumbukumbu. Sehemu ya Kuzimu uliyoona sio kila kitu, bali ni kijisehemu tu. Ni shauku ya Baba yetu wa Mbinguni kwamba roho nyingi ziokolewe kupitia kazi hii. Inaumiza sana roho yangu kuendelea kukupeleka Kuzimu na ninajua moyo wao unaumia pia. Kuanzia sasa, nitakuonyesha kidogo tu, kwa hiyo tazama kwa makini na uripoti kwa Mchungaji Kim sawasawa na unavyoona.” Nikasema, “Yesu, kama ukisisitiza. Tafadhali, usinionyeshe mama yangu na kaka yangu mdogo. Sitaweza kuvumilia maumivu ninapowaona.” Yesu akajibu, “Hiyo haiwezekani. Ni lazima uone mambo ambayo haungependa kuyaona, ili kwamba uweze kuishuhudia kweli. Mara alipomaliza kuongea, Bwana akanishika mkono na kuniongoza hadi Kuzimu.

* Kurudi Kuzimu
Kuzimu kunatisha. Akili zetu haziwezi kupata picha jinsi sehemu ambako ufukara na huzuni vimefungiwa kulivyo kubaya. Ni sehemu iliyolaaniwa na ina mateso, miguno ya maumivu, na kupiga yowe tu. Bwana pamoja na mimi tulikuwa kwenye kibarabara chembamba. Upande mmoja kulionekana roho ambazo zilikuwa kwenye mateso kupita kiasi. Tulifika mahali ambapo kila upande wa barabara kulikuwa na shimo refu. Yesu akanitahadharisha, “Kuwa mwangalifu!” Ukiondoa tu macho yako barabarani kwa sekunde unaweza kutumbukia. Niliona mafuvu kila upande kwenye shimo yamerundikana kwa urefu wa kama vile hadi juu mbinguni.

Mafuvu hayakuwa yamekufa, lakini yalikuwa yanasogea polepole na kupiga kelele. Ilikuwa kelele inayochoma masikioni mwangu. Mafuvu yale yalikuwa yanasongamana, wakati mengine yanaporomoka na kuangukia chini. Yalilalamika na kupaziana sauti, mengine yakisema, “Oh, nakosa pumzi! Mjinga wewe, sogea kule! Utasogea husogei?”

Nikauliza, “Tafadhali Bwana, inatia kinyaa sana. Kote kunatoa harufu ya uvundo. Nataka kuondoka hapa. Inawezekanaje yawepo mafuvu mengi kiasi hiki? Hawa walikuwa wanadamu wa aina gani?” Yesu akaniambia kuwa kulikuwa na watu wa aina tofauti pale, “Hapa wapo wezi wanaovunja nyumba ambao kwa bahati mbaya waliwasha moto kwenye nyumba hizo na wakaungua, wale waliokufa kwa moto wakiwa wamelala mahotelini, wale waliokuwa wakishawishi wanaume na wakafia kwenye moto, wale waliokuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa nguvu zao lakini wakaamua kuwa ombaomba, wale waliozama kwenye maji wakiwa kwenye matembezi, wale walioua wazazi wao, wale waliokuwa matembezi ya kuburudisha mwili na wakafa kwa ajali na wengine wengi toka maeneo mbalimbali ya maisha.”

Kulikuwa na mafuvu mengi sana sikuweza kuyahesabu. Upande mmoja, nikamsikia mtu mmoja akisema, “We mjinga, msongamano ni mkubwa sana hapa. Sehemu hii iliyojaa hivi inaniua!” Mafuvu ya upande wa chini yalikuwa yanasema “Nyie wajinga mlio juu, mnanivunja huku! Acheni kunivunja!” Yale mafuvu yaliyokuwa chini yalikuwa na vidonda vingi.

Kadiri tulivyoendelea kutembea, harufu ya maiti zilizooza iliendelea kuongezeka. “Bwana, hiyo ni harufu ya nini? Inanuka kama nyama zilizooza.” Bwana akaniambia, “Ndio, uko sahihi. Tazama kwa makini!” Nikaona majimaji yanayotoka kwenye miili inayooza. Ilikuwa kila mahali kama bahari. “Bwana, hakuna mafuvu wala mifupa hapa. Sioni mwili hata mmoja hapa, lakini kwa nini harufu ni mbaya kiasi hiki?” Yesu akasema, “Nyama na mifupa vilishaoza.”

* Mmea kama kakati
Tulipoendelea zaidi, tukafika kwenye eneo tambarare ambalo halina kitu. Lakini kulikuwa na mti mkubwa unaofanana na kakati (cactus), ambao haukuwa na miba inayoonekana. Mbele yake kulikuwa na kundi la vijidudu vidogo na pia kulikuwa kama na kitu kinatembea kwenye mti huo. Yesu aliniambia nikatazame kwa karibu, na kadiri nilivyousogelea mti huo, nilimwona mdogo wangu wa kiume pamoja na miili mingine isiyo na idadi iliyokuwa uchi. Yote ilikuwa imesongamana bila utaratibu huku ikiwa imegandamana kwenye mti huo. Kila mmoja alifunikwa na wadudu wale ambao walikuwa wanakula nyama za miili yao, huku watu wakipiga kelele kwa maumivu.

Pamoja na kelele zote zile za maumivu, niliweza kumsikia mdogo wangu waziwazi. “Dada! Mpendwa wangu dada Bong-Nyo, kwa nini umekuja hapa tena? Aagh! Kuna maumivu makali yasiyovumilika!” Kila mmoja alilia kwa maumivu wakati kila aina ya wadudu walipomuuma na kurarua ngozi yake, huku wakichimba kuingia kwenye miili yao. Sikuweza kuona hata sehemu ndogo ya ngozi kwa sababu walifunikwa kabisa na wadudu wale.

* Familia kwenye shimo lililojaa funza
Nilitazama kushoto na kuona shimo kubwa. Lilikuwa limejaa watu wasiohesabika. Wote walikuwa uchi na wamefunikwa na funza. Ilikuwa vigumu kutofautisha kati ya mwili na funza. (Marko 9:48). Nilidhani nitapoteza fahamu tena. Nilimwona mama yangu na kumwangalia machoni. Alikuwa akisubiri kutupwa kwenye shimo hilo. Mama yangu alipaza sauti, “Binti yangu, Bong-Nyo, nilisikia hukuwa unajisikia vizuri lakini kwa nini uko hapa tena?” Kisha akaanza kulia kwa sauti. 
“Mama, sitaki kuja kuzimu, lakini Bwana ameendelea kunileta huku. Nifanye nini sasa?” Mama yangu akaanza kuomba, “Bwana, kwa nini unaruhusu binti yangu anione nikiteseka Kuzimu, wakati unajua kuwa inaumiza sana?” Tulilia pamoja. “Mama, japokuwa nakuona ukiwa na maumivu makali kiasi hiki, siwezi kufanya chochote kinachoweza kukusaidia. Samahani mama!” nilisema. Mama yangu alinisihi, “Tafadhali, Bong-Nyo, usije ukarudi tena Kuzimu. Mimi nilishakufa na kuletwa hapa kuteseka, lakini wewe ni lazima uendelee kumfuata Bwana hadi mwisho. Usije kuishia hapa kama mimi, bali hakikisha unaenda Mbinguni.”

Nilimwomba Yesu asaidie, lakini hakuwa na cha kufanya. Nilipolia kwa sauti zaidi, mapepo yasiyo na huruma yalimtupa mama yangu kweye shimo lile. Mara moja, funza walimzingira, wakapanda kwenye mguu wake na kuchimba kwenye mifupa.   Alilia kwa maumivu makali na kurukaruka huku na huku, kama walivyokuwa wakifanya watu wengine. Mara kilio chake kilimezwa na vilio vya watu wengine.

Nilianza kumsikia mdogo wangu akiteseka upande wangu wa kulia. Alilia, “Dada, vijidudu vinakula mwili wangu hai.” Wadudu wale walimchoma mdogo wangu na sumu yao ilisambaa kwenye mwili wake wote, na kumfanya awe mweusi tii. Mdogo wangu alikufa kwa kujiua, lakini sikujua kuwa adhabu ya kufanya hivyo ilikuwa mbaya kiasi hiki. Nilimsihi Yesu lakini hapo tena akasema hakukuwa na nafasi hiyo tena. Nilimlilia hata Baba yangu wa Mbinguni, lakini naye pia alisema hapana. Baada ya muda kidogo, mwili wa mdogo wangu ukabakia mifupa myeusi tu, lakini bado alikuwa akilia, “Dada, harakisha uondoke mahali hapa. Usije kurudi tena mahali hapa. Unanielewa?”

Bwana alinielezea kuhusu baadhi ya watu hapo. “Kuna wanaume ambao waliishi na wanawake wawili na watatu, watu waliobadili wapenzi na kutembea na wengi, wale waliojiua wenyewe, wale walioenda kanisani lakini walikuwa wazinzi, wale waliokufa mlimani, wale waliouawa na mbwa, na wengine wengi waliokufa."

Huku tukiendelea na Yesu, niliona kitu kilichoonekana kama fyekeo kubwa – lilikuwa kubwa na la kutisha. Pepo moja kubwa sana lilishikilia fyekeo lile na likawa limejiandaa kuwakata watu. Yesu akasema, “Pepo hili ni la kumi kwa ukubwa huku Kuzimu.” Lilikuwa na vichwa vingi vimeota kwenye mwili wake wote. Lilianza kuwakata watu katika mstari na vilio vya kutisha vikasambaa kwenye anga  lote la kuzimu.

Mapepo yale maovu yalifurahia kuwatesa wengine. Yakaanza kumkatakata baba wa mchungaji wetu. Alipiga kelele, “Aaah! Tafadhali niokoeni. Samahani. Tafadhali acha! Nisamehe!” Ilikuwa inatisha. Kwa duniani, mtu angepoteza fahamu au kufa, lakini Kuzimu hakuna kupoteza fahamu wala kufa. Ni vilio vya kutisha tu. Hisia zako zote zinakuwa zinatenda kazi hapo.

Baba wa mchungaji alilia, “Ole wangu. Nilikufa kwa ugonjwa na nikadhani nikifa kila kitu kingeisha. Nilijua nitapumzika kwa amani bila ya kufanya kazi yoyote. Lakini sikutarajia mambo kama haya!” Alitikisa kichwa chake kwa uchungu. Baada ya kumkata mguu wake, lile pepo likasema, “Sasa nianze na mwili wako?” Likaendelea kumkatakata vipande vidogovidogo. Ilikuwa ni hali ya kutisha sana. Kila kitu kilikuwa kinaonekana waziwazi. Haikuwa ndoto. Pepo lile lilijua kuwa Yesu na mimi tulikuwa tunaangalia, lakini halikujali badala yake liliendelea tu kufanya kazi yake ya kikatili.

Pepo lile lilipasua kichwa chake vipande viwili kwa mikono yake na kutupa vipande hivyo kwenye sufuria kubwa la chuma, ambamo kulikuwa na mafuta yanayochemka. Watu waliyeyuka na kilichowabakia ni mifupa tu. Lakini bado vile vilio vya uchungu havikupungua. Mapepo yalikuwa yanakimbia huku na kule kwa msisimuko, huku yakicheka, kana kwamba ilikuwa ni namna fulani ya sherehe. “Ni safari nyingine tena tunaweza kujishibisha. Tuna vingi sana vya kula. Leo ilikuwa siku nzuri kwa sababu watu wengi sana wapya wamekuja Kuzimu. Ndio maana tunasherehekea na kuwakaanga,” yalisema.

Watu waliokuwa ndani ya sufuria walikuwa wakipiga kelele, “Wewe, ewe mjinga mwovu! Nitoe humu. Unaniunguza nikiwa hai. Nitoe humu sasa hivi! Siwezi kuona chochote. Kuna joto! Nakufa humu!” Pia walitukana matusi ambayo siwezi kuyataja humu.

Baada ya hapo, Yesu alinipeleka mahali ambako mabinti wawili wa Lutu (Mwanzo 19:31-38) walikuwa ndani ya shimo lenye moto, wakilia kwa uchungu. Yesu alihuzunika sana na kuumia kwa sababu ya maumivu makali kiasi kile akaamua kuondoka mara moja. Bwana akasema, “Bong-Nyo, moyo wangu unauma kwa sababu ya hawa mabinti wawili na ninajua maumivu uliyo nayo unapotazama familia yako ikiwa Kuzimu. Lakini, nataka ufikirie kwa kutulia juu ya yale uliyoyaona.” Yesu akaniambia kuwa kila mara aliponileta pale Kuzimu, moyo wake ulikuwa unaumia sana, lakini alikuwa anajizuia nisimtambue. Yesu akasema, “Hebu tuondoke sasa huku Kuzimu.” Akanirudisha tena kanisani.

No comments:

Post a Comment