Wednesday, October 3, 2012

Jinsi Ibilisi Anavyozuia Maombi Yako


Ndugu msomaji wa blog hii, kati ya makala au masomo ambayo nimeyaandika humu, hili ni somo na ushuhuda mmojawapo wenye nguvu sana ambao, kila mwana wa Mungu atakayeusoma, atapata msukumo wa rohoni usio wa kawaida. Haya ni mafunuo yenye nguvu mno ambayo, hakika yatakuinua kwa kiwango cha juu sana nawe utamshukuru Mungu. Nilipouona ushuhuda huu kwenye mtandao, moyo wangu ulianza kuwaka niweze kuutafsiri harakaharaka na kuuweka kwenye blog hii ili yamkini uweze kuwafikia wapendwa wengi iwezekanavyo.



Huu ni ushuhuda ulioandikwa na Mchungaji John Mulinde wa Uganda kutokana na kile alichosikia kutoka kwa mhusika mwenyewe. Mhusika huyo, mchungaji hajamtaja, lakini alikuwa ni kijana ambaye alimtumikia shetani tangu angali tumboni mwa mama yake. Baadaye, kwa neema ya Bwana kijana huyo aliokolewa, ndipo akaanza kueleza siri hizi za ufalme wa giza na ufalme wa nuru.


Mamilioni ya Wakristo duaniani tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali tuliyonayo. Lakini liko swali moja kubwa linalojirudiarudia ndani ya mioyo yetu karibu kila siku. Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa muda mrefu. Mbona Mungu hajibu...?” Tunabaki bila majibu, tunavunjika moyo, na tunaanza kudhani labda sisi ni wenye dhambi sana ndio maana hatujibiwi.


Ukiifahamu siri iliyomo kwenye ushuhuda huu, utatiwa nguvu sana za rohoni; maana maarifa ndiyo yanayotufanya tuwe na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani kwa kadiri ya kiwango cha maarifa au ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua sana, tunaweza sana; tukijua kidogo, tunaweza kidogo.


Karibu ujipatie maarifa ambayo Bwana wetu ameruhusu yatufikie. Nami na hakika utamfurahia Bwana kwa kukupigisha hatua nyingine ya imani. Utafanya vema kama ukiweza kuwapatia na wengine somo hili la muhimu sana kwa ajili ya mwili wa Kristo.


******************

Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni katika wakati huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho pale tunapoomba.

Kijana huyu alizaliwa baada ya wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa. Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na wachawi wa kawaida.

Alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA. Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje huko na kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling).  Na kijana huyu alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.

Siku moja, alipangiwa kwenda kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima. Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.

Siku moja, kijana huyu aliuacha tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho.

Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.

Roho yake ilikuwa inapaa hewani juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika.  

Ndiyo, alikamatwa na malaika! Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua."

Mchungaji alipofungua macho yake, alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye; maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.



Sasa, mambo haya ni magumu kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?" Kijana yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.

Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili. Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.    

Usiku mmoja, mimi (John Mulinde) nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa ombi.

Kulikuwako na wachungaji wengi pale kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini, wafundisheni watu namna ya kuomba.”  Watu ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni watu namna ya kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa."

Kisha alieleza jinsi ambavyo alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na mapepo haya yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza kuathiri matukio yanayoendelea duniani. 

Pale mapepo wachafu pamoja na maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara.  

Kijana huyo alisema kuwa, maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni.

Baadhi ya maombi huonekana kama moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani.

nyingine ya maombi nayo ni kama moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa, lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea. Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu anapoomba. 

Aina ya tatu ya maombi ni kama moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo na kuendelea hadi juu.

Mara nyingi watu wanapoanza kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba yanapenya kabisa ule mwamba.

Mara nyingi maajenti wa uovu hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!"

Mara nyingi Wakristo hushindwa na mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi. Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza kuwa, ngoja niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.  

Mbinu zingine za kuvuruga maombi nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu, bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao. 

Na kama watu waking’ang’ana kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza kustahimili pia. Wote wanakimbia.

Kama mtu atajitoa kuomba kwa bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha kuburudisha, na chenye nguvu.

Na nimegundua kuwa wakati huo, huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi. 

Na mara anapomaliza kuomba, lile tundu linabakia wazi.

Kijana huyu pia alisema kuwa, watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba, katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao. Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine. Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo vyote vya adui vinadhoofika.  

Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo. Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa na nguvu sana.

Na kama kuna sehemu ambako maombi ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika.

Na kama atatokea mtu wa kusema nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena kwenye sehemu kama hizo.

Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo?

Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi.

Sasa unaweza kupiga picha, sote tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake. Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri. Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."

Kwa kuwa mtu wa aina hii anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana.

Kama, kwa mfano, imeshajulikana kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha watu watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi, anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana, lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa haimfikii tena!

Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika! Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako. 

Kama udhaifu wa mtu ni kwenye masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si vizuri kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, " Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu."

Kila mara unapopata mpenyo katika maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana, nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia, usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali fulanifulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee, Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”

Mungu anaweza kufanya hivyo. Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika, “Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa njia hiyo anatuokoa na mambo yapi,  tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.

Yule kijana aliendelea kusema kuwa, unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya maombi yake. 

Kisha aliongea jambo ambalo kwa kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14).  Alisema kuwa watu wanapoomba, majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana. Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na amejivika silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika kikamilifu kwa silaha hizohizo.

Lakini, kama anayeomba hajali silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.

Malaika anapokuwa anakuja, mapepo wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.

Sasa, najua kuwa hili ni gumu kuamini; mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza, “Je, malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.

Kumbuka kile ambacho Biblia inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo 1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.

Katika Biblia, Yesu alisema, "Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na kumwacha adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?

Na hawaridhiki tu na kuiba jibu la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye. Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo, Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.

Nilimwuliza kijana huyo, “Una maana kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na malaika wa nuru  kwa mtu huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina.

Niliondoka kwenye kile chakula cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata kujaribu kuamini jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili. Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.

Alinipa mambo matatu:

Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba yetu.

Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu sisi.

Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia, anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na anasema, “Omba sasa!” Kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana, nitaanza Jumatatu!” 

Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa. Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili, linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali ni vya Bwana! Haleluya!  

Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu, kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.” Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!

Asante Yesu.


**********************


Ndugu msomaji wa blog hii, somo hili ambalo ni muhimu sana kwa kila mwanadamu na mwili wa Kristo, nimeliweka pia kama E-Book, hivyo unaweza kulipakua na kulisoma tena na tena; na pia kuwagawia wengine. Bofya HAPA.


Unaweza pia kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza (pamoja na shuhuda zingine) kwa kubofya HAPA.


Usikate tamaa. Simama imara katika imani. Unaweza kushinda. Bwana si dhalimu; anakupenda na amekuwa akijibu maombi yako siku zote. Je, Biblia si inasema kuwa KILA aombaye hupokea? (Mathayo 7:8). Na kwamba Mungu si mwanadamu hata aseme uongo (Hesabu 23:19).


Tumia mafunzo haya kusonga mbele katika wokovu na imani yako. Bwana Yesu akubariki sana.

42 comments:

  1. Mungu ambaye ni Baba wa Mbinguni asikuache katika Jina la Yesu. Ushuhuda huu umekuja kwenye majira yenyewe ambapo mwili wa Kristo unahitaji kuamka. Naitumia statement ya kwenye ushuhuda wa Victoria ya kuwa 'Muda unaisha haraka'
    Ni maombi yangu ujumbe huu uguse kila mwenye mwili ili isiwepo mahali mtu akatoa sababu kuwa hakufahamu hata akashindwa.
    Maombi ni vita, na vita nzuri na yenye ushindi ni ile inayokupa fursa ya kujua adui yako ana silaha za namna gani.
    Asante kwa Roho Mtakatifu anayetufanya tushinde na zaidi ya kushinda hata anafunua haya toka yalikositirika. Hakika huu ni mpango wa Mungu kuona Utukufu wa nyakati hizi kuwa juu.

    ReplyDelete
  2. Amina, amina sana Revocatus. Ni kweli kabisa tumo kwenye vita kali mno kiasi kwamba, naamini, asilimia tisini ya kushindwa kwetu inasababishwa si na utayari wa kuomba, bali na ukosefu wa maarifa. Maana hatuwezi kutenda nje ya imani. Na kabla mtu hajasikia kitu, hakuna imani - maana imani huja kwa kusikia. Lakini tunapoyasikia yale yanayoendelea katika ulimwengu wa roho, bila shaka tutaweza kushindana kwa nguvuzaidi, ujuzi zaidi, na mafanikio zaidi. Namwomba Roho Mtakatifu azidi kutufundisha zaidi na zaidi. Ubarikiwe sana na Bwana.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mtumishi James nashukuru sana kwa ushuhuda mzuri sana ambao umenipa mwanya wa kuwa na uelewa kiasi fulani. Binafsi mimi naomba nipate namba yako ili uweze kunisadia katika ufafanuzi wa mambo fulani.

      Delete
    2. Amina brother Masatu. Bwana aendelee kukupa nguvu. unaonaje ukiniandikia e-mail kupitia ijuekweli77@yahoo.co.uk maana huenda kwenye simu tusiweze kuzungumza kitu kikaeleweka. Maana naweza nisiwe na jibu la kila swali papo kwa hapo. lakini ukiniandikia chochote, ninapata muda wa kukitafakari, kukitafiti na hatimaye kuwa na jibu la uhakika zaidi. Bwana Yesu akubariki.

      Delete
  3. kama kuna ujumbe ulinifungua akili juu ya maombi basi hakuna kama ushuhuda huu na mimi natawafundisha wengi sana na kuwashuhudia juu ya ujumbe huu ili shetani asipenyeze lolote katika maombi,barikiwa sana mtumishi wa MUNGU James John

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amen brother Peter. Ubarikiwe nawe pia. Endelea kupiga majeshi kwa nguvu zaidi.

      Delete
  4. Leo hii nimegundua kua silaa za maombi kwangu hazipo, Kwani nikimaliza maombi najua nimemaliza part yangu kumbe sivyo muombajiwa mungu alivyo. Ushuhuda huu umenijenga pakubwa sana, JAMES JOHN ubarikiwe sana. Ninashaukuwa kusambaza ujumbe huu kwa watu wengi zaidi.

    ReplyDelete
    Replies
    1. I mean sivyo Muombaji wa Mungu alivyo

      Delete
    2. Amen ndugu yangu. Ubarikiwe nawe pia. Mungu akubariki unapousambaza ujumbe huu ili uweze kuwafikia wengine wengi nao wabarikiwe na kuinuliwa.

      Delete
  5. Namshukuru sana Roho mtakatifu kwa maarifa haya kwani nimepata nguvu mya na nimejuwa kuwa maombi ni vita halisi tena ni zaidi ya vita yoyote hapa duniani.Na ni muhimu sana ukaingia kwenye maombi haya ukiwa na silaha zote za Mungu.Na usujaribu kufanya maombi waka bado haujampokea Yesu kwani hauta kuwa na Nguvu ya Mungu ya kupambana katika ulimwengu wa Roho.Na kama umesh okoka ni Muhimu uka anza na toba kabla ya Maombi.ISAYA 59: 1-2 inasema maovu yetu uturarikisha na Mungu nakututenganisha na hata hataki kusikia Maombi yetu.Hivyo kuingia kwenye maombi bila toba na kurudisha uhusiano na Mungu lazima utashindwa.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amen. Amen. Ni kweli kabisa. Maisha ya kiroho ni vita kamili kabisa. Tunashindana na mashetani ambao ni wazoefu wa mambo haya kwa maelfu na maelfu ya miaka. Pia wao wanatujua na kutona wakati sisi hatuwaoni. Ni jambo lisilowezekana hata kidogo kuwashinda hawa kibinadamu. Ni Yesu pekee ndani yetu ambaye anaweza kutufanya tushinde. na ni kweli kwamba ili Yesu akae ndani yetu, ni lazima mioyo yetu iwe safi. Bila hivyo, kushindwa kwetu ni jambo la hakika. Ubarikiwe mpendwa.

      Delete
  6. kweli kabisa ushuhuda huu umenibariki sana nimeona ni jinsi gani natakiwa kufuata utaratibu katika kuomba, haswa pale unapoamshwa na kuambiwa omba. Jambo lingine ni kukata tamaa kwa mambo unayoomba tunatakiwa kuendelea kuomba na kuzivaa silaha zote za kumpinga shetani na tuzifanyie kazi tusiende vitani bila silaha.

    Mungu akubariki sana

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amina mpendwa. Ubarikiwe sana na wewe pia.

      Delete
  7. Ningependa kujua ni jinsi gan mtu anaweza kuvaa silaa na kuzitumia kivip

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante mpendwa kwa swali lako muhimu. Biblia inasema kuhusiana na silaha za kiroho na uvaaji wake:

      Basi simameni, hali mmejifunga KWELI viunoni, na kuvaa DIRII YA HAKI kifuani, na kufungiwa miguu UTAYARI tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni CHAPEO YA WOKOVU, na UPANGA WA ROHO ambao ni neno la Mungu (Waefeso 6:14-17).

      Wakati Paulo anaishi (na hata nyakati za Bwana Yesu), Israeli ilikuwa ni koloni la Warumi. Katika nyakati zile, teknolojia ilikuwa chini kuliko leo. Kwa hiyo, hata vita haikuwa ikipiganwa kwa mabomu, bunduki na madege ya kivita kama leo. Ilikuwa ni vita vya ana kwa ana inayotumia silaha zilizokuwa zikitupwa kwa mkono, kwa mfano marungu, mikuki na pinde na mishale.

      Hivyo, hapa Paulo anatumia picha ya askari wa Kirumi jinsi alivyokuwa akionekana. Kwa kifupi, walikuwa wakivaa mabamba ya madini ya shaba mikononi, miguuni, kifuani na pia kofia (helmeti) kichwani ili kujikinga na silaha za adui kama vile mishale, mikuki, na panga.

      Kwa msingi huo, hata sisi tunahesabika kama askari kwa namna ya rohoni tukishindana na askari wengine (majeshi ya pepo wabaya). Ndipo sasa, Biblia inatuambia tuvae silaha kama ifuatavyo:

      Kiunoni - kweli. Kweli ni Neno la Mungu. Tunapokuwa na Neno hili mioyoni mwetu, katika ulimwengu wa roho tunaonekana tuna ulinzi kwenye miguu yetu. Silaha hii tunaivaa kwa kusoma Biblia, kusikiliza mahubiri kwa makini na kutafakari Neno la Mungu kwa undani.

      Kifuani – dirii. Dirii ni bamba la shaba. Lakini kiroho bamba hili ni haki. Maandiko yanasema: Hakuna mwenye haki hata mmoja ... wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. (Warumi 3:10,24).

      Hakuna mwanadamu anayeweza kwenda mbinguni kwa sababu ya kujitahidi kutenda matendo mema kama dini zingine zinavyojidanganya. Mtu anapoamua moyoni mwake tu kuamini kwamba: Naamini Yesu alikufa kwa ajili yangu na kubeba dhambi zangu, basi anasamehewa dhambi zake kwa kuwa Yesu alishazilipia adhabu yake. Kisha, kwa Yesu ni mwenye haki, mtu huyu anavikwa ile haki ya Yesu. Hivyo, Mungu anamhesabu kuwa ni mwenye haki kupitia mgongoni mwa Bwana Yesu. Huko sasa ndiko kuokoka. Kwa maana nyingine, unapoamua kupokea wokovu wa Yesu, unakuwa tayari umevaa dirii ya haki.

      Miguuni - utayari wa injili. Hii ni silaha ya kuwa tayari kuwahubiria wengine habari za wokovu, au kwa neno lililozoeleka, kuwashuhudia wengine kuhusu wokovu wa Yesu. Mtu anapofanya hivyo, katika ulimwengu wa roho anakuwa tayari amevaa silaha kwenye miguu yake kama ambavyo askari wa zamani walivaa mabamba ya shaba miguuni.

      Kichwani – chapeo. Wokovu pia unahesabika kama chapeo (helmeti) iliyo kichwani. Silaha hii nayo unaivaa kwa kupokea tu wokovu wa Yesu Kristo. Unapokubali kuokoka, mapepo na viumbe wa rohoni wanaona tayari kuna chapeo kichwani mwako.

      Mikononi – ngao na upanga. Kazi ya ngao ni kuzuia silaha za adui zisifie mwili wa askari. Imani ni ngao ambayo inabatilisha kazi ZOTE za shetani dhidi yetu, iwe ni magonjwa, hofu, uchawi, n.k. Tunavaa ngao hii kutokana na kusoma, kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu KWA BIDII, maana imani huja kwa kusikia Neno la Kristo.

      Neno la Kristo linapokaa kwa wingi ndani yetu na likachanganyika na imani inayozalishwa na Neno hilohilo, kinachotoka ndani yetu baada ya hapo ni upanga wa Roho. Kwa macho tunakuwa hatuoni lakini kwenye ulimwengu wa roho, neno la imani ni upanga kabisa. ndiyo maana tunasoma kuwa Bwana Yesu ana upanga kutoka kinywani mwake (Ufu 1:16).
      .........................
      Bwana Yesu akubariki.

      Delete
    2. Amina! Ubarikiwe sana James John hakika nimejifunza mengi kwenye ujumbe huu! na Mungu aendelee kukupa ufunuo zaidi! JINA LA BWANA LIHIMIDIWE!

      Delete
    3. Amen Sebastian. Bwana akubariki nawe pia.

      Delete
  8. SHALOM-NIMEUKUBALI USHUDA HUU NI WA KWELI , MUNGU AKUBARIKI
    Apostle Peter Minja -JESUS Power of Prayer Ministry

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mtumishi Apostle Peter, Bwana Yesu zidi kukubariki nawe pia na kukuinua katika huduma aliyokupa.

      Delete
  9. WAPENDWA WAKRISTO WENZANGU, MUNGU NI MWEMA HATA KUWATUMIA WATU MBALIMBALI WATUONYESHE YALIYOFICHIKA SIRINI, NI MUDA WETU NA WASAA WETU SASA KUYATUMIA ILI SIKU MOJA TUWE WASHINDI... BWANA AWABARIKI SANA WOOTE!

    ReplyDelete
    Replies
    1. amen mpendwa. Bwana aendelee kukuinua zaidi na zaidi katika njia yake ya uzima.

      Delete
  10. Hakika hakika hakika hakika ili neno limetoka kwa mungu limekuja wakati niko kwenye majaribu makubwa. Na hii si mara ya kwanza mungu kunipa majibu ya majaribu nayopata kwa kutumia blogs na inatokea tuu. Hakika Mwacheni Mungu aitwe Mungu. Thank u Jesus! Thank u Jesus. Nimefunguka sana daaah aisee

    ReplyDelete
    Replies
    1. sifa ni kwa Mungu wetu ambaye hatuachi ukiwa maadamutunazidi kumtazama na kumngojea kwa saburi. Yeye ni Mungu anayejibu maombi hakika!

      Delete
  11. Ndugu usikae kimya dah yaani yote uliyoyaandika yoooooote yananihusu mimi. Sasa nakuomba uende kwa bwana akupe mafunuo juu kuomba hadi kupata mpenyo. Please usikae kimya njoo tena najua kama Mungu alivyokuongoza ndivyo jinsi atakuongoza katika sehemu ya pili. Barikiwa na bwana.

    ReplyDelete
    Replies
    1. amen. Bwana atafanya hivyo na kuzidi maana Yeye anajishughulisha na maisha yetu sekunde hadi sekunde. Tuendelee kumtazama Yeye peke yake.

      Delete
    2. Ndugu James bado nasubiri kwa hamu kubwa sana.kuusu swali hapo juu. Barikiwa sana

      Delete
  12. Mtumishi James. Naanza kupata maswali mengi sana baada kusoma mafunuo haya. Je mtu ambae tundu lake la mpenyo(kuomba) limezibwa na mapepo baada ya kumteka akili zake anatakiwa afanyaje? Au Aombaje? Je maombi yapi yenye Mpenyo ni yale yenye kuongozwa na roho mtakatifu yani kuna uwepo wa roho mtakatifu. Au yale maombi ya mdamrefu si chini ya saa moja kama Yesu alivyowauliza wakina petro hamkuweza kukesha nami japo saa moja!. Yenye kuzama kupitia roho mtakatifu. Je unapopata mpenyo katika moyo wakati unaomba ndo mbingu imekuwa wazi kule juu kwa ajili ya maombi?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom pendwa Joseph
      Samahani kwa kuchelewa kujibu maswali yako. Wakati mwingine mambo yanakuwa mengi sana lkn najitahidi kujibu kila swali hata kama ninachelewa kwa kiasi fulani.

      Kanuni moja ya muhimu sana kukumbuka katika maombi ni hii:
      Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, KWA KADIRI YA NGUVU ITENDAYO KAZI NDANI YETU. (Waefeso 3:20).

      Maisha ya mwamini ni jambo la tabia zaidi na sio vitendo vya dharura. Uhusiano wetu na Kristo wa siku hadi siku ndilo jambo la muhimu zaidi kuliko maombi tunayofanya kwa sababu ya dharura fulanifulani zinazotutokea, kama vile ugonjwa, nk.

      Tunapokuwa na maisha ya maombi kila siku, ndipo ILE NGUVU YA MUNGU NDANI YETU inaongezeka zaidi na zaidi. Na hiyo ndiyo anayoitumia kutenda yale tuyaombayo. Hatumii nguvu iliyo kwake mbinguni, hapana. Japo anaweza kufanya hivyo akiamua mwenyewe, kwa mfano anapomponya mgonjwa ambaye hata hamjui.

      Sasa nguvu hii inatokana na mambo yafuatayo (japo yanaweza kuwapo na mengine):
      1. Kujiepusha na dhambi na kuishi katika utakatifu.
      2. Kuwa mtu wa maombi kwa uda mrefu kadiri inavyowezekana – kwa mfano umetaja saa moja kama alivyowaambia akina Petro.
      3. Kusoma Biblia ili kujua haki zako na wajibu wako ndani ya Kristo. Yaani Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu (Wakolosai 3:16).
      4. Kujumuisha na kufunga.
      Maombi ni vita. Kama una jambo unataka Mungu akutendee, unaweza kumsihi na kumlilia – ni sawa. Lakini unapokabiliana na ibilisi, hapo hakuna kusihi. Ni kubomoa, kulazimisha, kung’oa, kuharibu kazi za shetani.

      Tunalifahamu vema andiko hili: Kwa maana KUSHINDANA kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. (Waefeso 6:12).

      Kwa nini tushindane?
      Kwanza: Tazama nimewapa AMRI YA KUKANYAGA nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. (Luka 10:19). Amri hapa maana yake mamlaka.

      Pili: maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata KUANGUSHA NGOME (2Kor 10:4)


      Silaha mojawapo kubwa kabisa ni Neno la Kristo: Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? (Yeremia 23:29).

      Ndiyo sababu ya kusema Neno hilo ni lazima lijae sana ndani yetu. Ukiomba kwa kutumia Neno, unakuwa unabomoa na kuangusha kabisa kazi zote za ibilisi.

      Sasa, Mungu anaahidi kwamba: tukiomba mkate, atatupa mkate na sio jiwe au nyoka.


      Ni lini ataleta huo mkate baada ya sisi kuomba? HILI SASA HALINA JIBU MOJA KWA KILA MTU – na ni matokeo ya hiyo nguvu sasailiyo ndani ya mwombaji. Nguvu ikiwa kubwa, matokeo yataonekana haraka; ikiwa ndogo, matokeo yatachelewa.


      NYONGEZA:
      Kama unaweza kuomba zaidi usiku, itakuwa ni vizuri zaidi maana huo ndio wakati wa kuzimu kufanya kazi zao za uharibifu na kukaza zaidi vile vifungo wanavyotufunga navyo.

      Ubarikiwe na Bwana.
      Kama kuna sehemu haijaeleweka, tuendelee kujadiliana.

      Delete
  13. Kwa kweli ubarikiwe sana kaka Jamesi! Kweli nimeamini kumbe kuna muda unaweza kuomba sawa kwa muda mrefu rakini hujui unapambana na nini au ukadhani maombi yalifika kumbe ibilisi alishayazuia, Vile vile kumbe kuna maombi mengine tumeomba na kujisahau hadi ibilisi ameiba majibu Yetu hapo nimeamini.

    ReplyDelete
  14. Asante mtumishi nami sina swali lingine. Labla kule kwingine. Asante

    ReplyDelete
  15. Mungu akubariki sana mtumishi James kwa kutufungua macho ya Rohoni. Binafsi nimegundua siri kubwa katika mafundsho haya.

    ReplyDelete
  16. Mungu azidi kukubariki na kukutumia kutulisha neno lake kwa hekima. Nimebarikiwa saaaana na hili neno la maarifa nimelipata wakati muafaka. Kama mhubiri alivyosema kila jambo lina wakati wake. Na kweli hili nimelipata wakati muafaka. Barikiwa saaana mtumishi wa Mungu

    ReplyDelete
  17. Mungu azidi kukuinua na kukutumia somo zuru ushuda huu nli uprint nikawagea rafiki zangu uliwasaidia sana nami nimejifunza kitu kikubwa sana na mbinu za kuongeza kupambana ktk ulimwengu wa Roho.

    ReplyDelete
  18. Leo I hi nimefunga lakini nilikuwa nasikia NJaa sana .lakini shuhuda imeniinua zaidi
    Ubalikiwe mtumishi.

    ReplyDelete
  19. 1)amen amen leo nimewekwa huru kuna mambo nlikuwa siyaelewi.....kuna wakati nilikuwa namuona mtu ndotoni ambae alisema na mimi kama mwanafunzi wake na mapepo yalikuwa yanakasirika sana na nilifahamu yule ni roho wa mungu aliye mbinguni lakini nlikuwa najiuliza why afanyi kitu na mimi hizi roho zinanipiga vita USIKU NA MCHANA (nimeeka mabano sababu na maanisha ni vita kweli)
    2)Alafu kuna roho mmoja anapokuwa ananifuata usiku kupambana na mimi huwa anaangalia sana angani kana kwamba kuna kama maagizo anapokea sasa nafaahamu ni nini kilichokuwa kinaendelea sasa nabidi kubadilisha aina za maombi yangu barikiwa saana

    ReplyDelete
  20. nilikuwa vilevile naomba niruhusiwe ushuhuda huu kuu forward kwa mablog ya wakristo lakini nikiambatanisha reference au source injiliyakweli.blogspot.com

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom Petrus
      Nimekuwa sipati muda kirahisi kuja kwenye blog siku hizi. Muda mwingi natumika wenye facebook. Lakini unaweza kabisa kusambaza ujumbe wowote humu kiasi unachoweza.

      Delete
  21. Mungu akuinue na kukuweka mahali pa juu.
    Ubarikiwe mtu wa Mungu sasa nimejitambua

    ReplyDelete