Sunday, November 4, 2012

Kuteswa kwa Ajili ya Kristo





Tunaweza kufikiri kuwa tunapita kwenye hali ngumu maishani mwetu. Lakini mara nyingi huwa tunanung’unika tu kwa sababu hatuna nguo, fedha au chakula.

Lakini wapo watakatifu wa Bwana ambao wamepitia mateso mengi kutokana na ushuhuda wao kwa Kristo, Bwana wetu. Ni kwa sababu walimwamini Kristo, matokeo yake wakajikuta kwenye mateso.

Hata leo wapo Wakristo wengi duniani ambao wanateseka kutokana na imani yao kwa Mwokozi. Lakini kwa neema ya Bwana, wameng’ang’ania imani hii.

Sijui wewe unapitia magumu gani. Je, umekata tamaa kwa sababu ya hali ngumu unayopitia? Je, unahisi kuwa Mungu amekuacha?

Mchungaji Richard Wurmbrand alikuwa ni mchungaji katika nchi ya Rumania wakati wa ukomunisti. Kwa kuwa ukomunisti ulikuwa unakataa kuwapo kwa Mungu, na shetani aliutumia kufanya kila liwezekanalo ili kuufuta Ukristo, mchungaji huyu pamoja na maelfu kwa maelfu ya Wakristo walijikuta wakikamatwa na kufungwa kwenye magereza; huku kila mmoja akijikuta kwenye chumba cha giza kilichoko chini sana ya ardhi; ambapo walibaki humo, si kwa siku kadhaa, bali kwa miaka mingi!


Lakini hata hivyo, watakatifu hawa, hawakumkana Kristo, na hawakuiacha imani.


Fuatana na Mchungaji Richard Wurmbrand upate kujua kuwa misalaba inabebeka na kwamba, nawe pia, unaweza kabisa kuvuka kipindi cha jaribu lako.

*******************

Mchungaji Richard anasema:
Hatukusikia katika jela hii sauti hata iliyo ndogo sana. Walinzi walikuwa na viatu vya nguo na kuta zilikuwa kimya kabisa. Sasa, katika ukimya huu mkubwa, tuliweza kubaini endapo Ukristo ni kitu cha kweli au sivyo.

Mimi nilikuwa ni mtu; mchungaji ambaye nilikuwa sijasoma Biblia yangu kwa miaka 14 – nimeshaisahau; nimesahau thiolojia yangu; lakini nimegusa uhalisia wa rohoni; nimegusa ulimwengu wa malaika. Na kwa unyenyekevu mkubwa, tungeweza kuyatamka maneno ya mitume katika waraka wa kwanza wa mtakatifu Yohana juu ya kile ambacho tulikiona kwa macho yetu; tulichosikia kwa masikio yetu; tulichogusa kwa vidole vyetu – hiki ndicho tunachowaambia.

Mara ya kwanza, tulipowekwa kwenye kifungo cha upweke (yaani unakuwa peke yako), ilikuwa ni kama kufa. Mara malaika wa mauti walipokupeleka kule, unakabakia peke yako na kumbukumbu za maisha yako yaliyopita. Ilikuwa ni wakati mgumu sana kwetu ambapo kila mmoja alianza kukumbuka dhambi zake za zamani na kukwepa kwake majukumu yake.

Tulikumbuka kila kitu tulichokosea. Sasa tulikuwa chini ya macho ya Mungu. Kama ilikuwa ni maneno mabaya tuliyoyasema kwa mtu, tulikumbuka; iwe ni matendo mabaya, tulikumbuka.

Humo gerezani, tulikuwa pamoja na mhubiri mmoja mkubwa kabisa wa Romania; ambaye ni kama Billy Graham wetu. Baada ya miaka hii ya mateso, alikuja kutuambia kuwa, katika miaka hiyo yote ya kifungo cha upweke, alikuwa na majuto makubwa juu ya jambo lifuatalo:

Siku moja alikuwa ametoka kuhubiri kwenye mkutano mmoja wa Injili ambapo alileta roho 400 kwa Kristo. Na alipomaliza mkutano, kijana mmoja alimkimbilia na kusema, “Mchungaji, naomba kuzungumza na wewe.” Na mchungaji yule alimgeukia na kusema, “Nimechoka sana sasa. Sitaweza. Tafadhali uje wakati mwingine.”

Kwa hiyo, kijana yule aliondoka na mchungaji hakumuona tena.

Kisha wakomunisti waliingia madarakani. Siku moja jumapili, mchungaji alimaliza kuhubiri. Akiwa amechoka sana, usiku polisi wa siri wa kikomunisti walikuja kwake. Walimchukua na kumpeleka kwenye mahojiano kwa siku tano mfululizo – usiku na mchana! Na sasa, kutokana na hofu ya wakomunisti; hofu ya kuteswa, aliweza kufanya kile ambacho alikuwa hakuweza kufanya kwa ajili ya Kristo kutokana na upendo.

Kwa hiyo, aliteseka kwa mawazo kwamba, “Nitasema nini kwa Kristo nitakaposimama mbele zake? Maana ni kweli nilileta kwake roho 400. Lakini zingeweza kuwa 401.” – yaani kama asingemrudisha yule kijana.

Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kuwa, sote tulikuwa na maumivu makubwa mioyoni mwetu, tukiwaza kuwa hatukufanya vya kutosha kile tulichotakiwa kufanya kwa ajili ya Aliye Juu, ambaye alitoa uhai wake kwa ajili yetu msalabani. Na tulipokuwa kwenye kina cha majuto na maumivu haya, mara moja kuta za jela zilianza kung’aa kama almasi.

Nimeshaona mambo mengi mazuri maishani mwangu. Lakini sijawahi kuona uzuri uliokuwa kwenye vile vyumba vya giza kule gerezani, chini ya ardhi. Sijawahi kusikia muziki mzuri kama ule wa kwenye siku ambapo Mfalme wa wafalme, Yesu alipokuwa pamoja nasi. Tuliona welewa wake; macho yake ya upendo. Alifuta machozi kwenye macho yetu. Alizungumza nasi maneno ya upendo na maneno ya msamaha. Tulijua kuwa kila kitu ambacho kilikuwa kiovu kwenye maisha yetu, kimeshaisha; kimeshasahauliwa na Mungu.

Kisha zilikuja siku nzuri. Bibi harusi alikuwa kwenye mikono ya Bwana harusi. Tulikuwa pamoja na Kristo. Hatukujua tena kuwa tulikuwa gerezani. Wakati mwingine tulipelekwa kwenye kuhojiwa. Tulipigwa, tuliteswa. Lakini, kama ilivyokuwa kwa mtakatifu Stefano, wakati walipomtupia mawe, hakuwaona wauaji wake; hakuona yale mawe, lakini aliona mbingu zikifunguka na Yesu amesimama mkono wa kuume wa Baba. Kwa hiyo, na sisi hatukuwaona tena watesi wa kikomunisti. Hatukuona kuwa tuko gerezani. Tulikuwa tumezungukwa na malaika. Tulikuwa pamoja na Mungu. Tulikuwa hatuamini tena kuhusu Mungu, Kristo na malaika kwa sababu tu mistari ya Biblia inawataja – maana hata mistari yenyewe ya Biblia tulishaisahau – si kwa sababu vitabu vya thiolojia vinawataja, bali ni kwa sababu tulipitia uzoefu huo kwa namna iliyo halisi kabisa kiroho.

Na baada ya miaka mingi ya kifungo cha upweke, mambo yalibadilika. Tuliwekwa pamoja kwenye vyumba vikubwa. Wakati mwingine vilikuwa na watu 200 au 300. Amini usiamini, nyie mnaonisikia; mimi ni mchungaji. Na wajibu wangu ni kusema kweli yote. Lakini sitafanya hivyo kwa kuwa hamtaweza kustahimili kusikia kweli yote. Ninaongea mbele za uwepo wa Mungu. Katika gereza la Pitesht, wafungwa Wakristo waligombania misalaba kwa siku nne mfululizo. Misalaba ile iliwekwa sakafuni mara kwa mara. Na mamia ya wafungwa wengine walipigwa na kuteswa hata kuuawa, wakilazimishwa kujisaidia kwenye nyuso na miili za wale waliosulubiwa kwenye ile misalaba.

Kisha ile misalaba ilisimamishwa, na wakomunisti wanasimama pembeni wanaanza kudhihaki wakisema, “Tazameni Kristo wenu jinsi alivyo mzuri. Ameleta manukato kutoka mbinguni.”

Kisha wanawapiga mateke wafungwa wengine kuwalazimisha kupiga magoti na kuwaabudu hawa waliosulubiwa huku wamejaa kinyesi na mkojo wa binadamu.

Mapadri na wachungaji wameshawekwa kwenye vyumba vyenye mamia ya wafungwa na kulazimishwa kuendesha misa kwa kutumia vinyesi na mkojo – na baadhi yao walifanya hivyo!

Nilipomuuliza padri mmoja wa kikatoliki, “Father, kwa nini hukuwa tayari kufa kuliko kushiriki kwenye dhihaka hii ya kishetani?”

Aliweka kichwa chake begani mwangu na kuniambia, “Kaka, usinihukumu. Mimi nimeteseka kuliko Kristo.”

Hebu shiriki mateso yetu. Kula, jioni hii, kijiko kidogo kimoja cha chumvi, kisha usinywe maji kwa saa moja. Ndipo utajua mateso ambayo Wakristo wafungwa walipitia kwenye makoo yao; ambapo walilishwa vijiko vikubwa vitatu au vinne vya chumvi, kisha walinyimwa maji ya kunywa kwa saa nyingi.

Kisha kilikuja kipindi kingine kibaya zaidi; kipindi cha “brain washing” – yaani akili yako kulazimishwa ifikiri mambo fulani tu au isifikiri mambo fulani. Mtu ambaye hajapitia “brain washing” hawezi kujua jinsi ilivyo mateso makubwa.

Kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 4 usiku – saa 17 kwa siku – tulilazimishwa kukaa huku umenyooka: hakuna ruhusa kuinama; hakuna mahali pa kuegemeza kichwa; kufunga macho lilikuwa ni kosa kubwa!

Kwa saa 17 kwa siku ulikuwa umekaa tu huku unasikia maneno yanayorudiwarudiwa: Ukomunisti ni mzuri; Ukomunisti ni mzuri; Ukomunisti ni mzuri; Ukomunisti ni mzuri; Ukomunisti ni mzuri; Ukristo ni ujinga; Ukristo ni ujinga; Ukristo ni ujinga; Ukristo ni ujinga; Ukristo ni ujinga; Hakuna tena mtu anayemwamini Kristo; Hakuna tena mtu anayemwamini Kristo; Hakuna tena mtu anayemwamini Kristo; Hakuna tena mtu anayemwamini Kristo; Hakuna tena mtu anayemwamini Kristo; Achana naye; Achana naye; Achana naye; Achana naye; Achana naye!

Kwa siku nyingi, wiki, miaka ... tulilazimika kusikiliza mambo haya!

******************

Ilipofika mwaka 1964, mchungaji Wurmbrand aliachiliwa kutoka gerezani na akaendelea na kazi ya kumhubiri Kristo licha ya vitisho alivyokuwa amepewa.

Mwaka 2001, Mchungaji Richard Wurmbrand alienda kuungana na Bwana mbinguni baada ya kumaliza kazi yake hapa duniani.

2 comments:

  1. Mateso yapo na wana wa Mungu wanakutana na shida nyingi duniani lakini afanyaye njia pasipokuwa na njia ndiye pekee mtetezi wetu.
    Mtumishi wa Mungu Wumbrand ni somo tosha kwa Wakristo kuwa hatukuitwa kwa furaha tu bali na machozi pia kwa ajili ya msalaba wa Kristo
    Amen

    ReplyDelete
    Replies
    1. I want to buy the book. Kuteswa kwa ajili ya Kristo My name is Michael Wurmbrand and I am the son of Pastor Richard Wurmbrand. Please contact me at hfr@helpforrefugees.com. God Bless!

      Delete