Sunday, October 9, 2022

Uumbaji wa kutoka chini

Mungu Baba aliye JUU YA YOTE aliumba kila kitu.

Neno lake linasema: Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, NI CHEMA SANA. (Mwanzo 1:31)

Iwe ni wanyama, ndege, mazao na binadamu – KILA KITU kikawa ni chema sana.

Kuna watu duniani humu wanaomchukia Mungu kuliko unavyoweza kufikiri.
Wamebadilisha mazao karibu yote unayoyajua.
Iwe ni pilipili, tangawizi, mahindi, matikiti, maparachichi, nk.
Yale yanayozalishwa sasa, ukiyatazama kwa macho ni makubwa, na yanazaa sana. Siku hizi utaona maparachichi makubwa kama boga dogo.
Kibiashara utawaza ni faida sana.
Lakini ukweli utabaki palepale – HAKUNA MWANADAMU ALIWAHI AU ATAWAHI KUTENGENEZA KITU KIKAMILIFU KAMA MUNGU BABA – HAKUNA!
Iwe ni zao, mnyama, dawa, au chochote.

Ukitembea popote utaona maua madogomadogo, mengine hayana hata mvuto wa maana – yapoyapo tu. LAKINI Bwana Yesu akasema: … nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. (Mat 6:29)

Kale kaua kabayakabaya unakokakanyaga kila siku bila kukatilia maanani kameundwa na Mungu Baba kwa ufundi wa hali ya juu (extremely sophisticated) kuliko vazi au pambo lolote lililotengenezwa na mwanadamu duniani!

Neno linasema:
Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, AMBAO MBEGU ZAKE ZIMO NDANI YAKE, juu ya nchi; ikawa hivyo. (Mwanzo 1:11)

Siku hizi kuna matunda na mazao ambayo hayana mbegu ndani yake. Yameshachezewa na mwanadamu. Hata yakiwa na mbegu, ni mbegu tasa. Huwezi kuipanda ikaota. Ukishavuna, inabidi ukanunue mbegu za kileo ili upande tena.

Wameshabadlisha pia wanyama.
Ndiyo maana kuku aitwaye “wa kisasa” anaotaga mayai lakini hayawezi kuangua vifaranga, nk.

Lakini kwa nje utavutiwa kwa sababu unataka pesa – miezi mitatu, umeshavuna na kuuza.

Swali ni kuwa, unadhani wataishia kubadili mimea na wanyama tu? Je, hawana mpango wa kumbadili hata mwanadamu?

Dunia inaongozwa na uongo mkubwamkubwa MWINGI.
Yesu ni KWELI na UZIMA.
Ibilisi – ambaye anaabudiwa na dunia – ni UONGO mtupu na MAUTI.
Yeye ndiye audanganyaye ulimwengu WOTE.
Anatumia umoja wa mataifa kutimiza malengo maovu ya kuharibu uumbaji wa Mungu Baba.
Heri ungeelewa ninasema nini!
Mpokee Yesu uwe salama.

Kama una maswali, uliza ujue zaidi.

NYAKATI HIZI NI MBAYA SANA

Japo injili ya mafanikio haijawahi kuwa na umuhimu wakati wowote, lakini huu HASA si wakati kabisa wa kuhubiri injili za mafanikio.

Dunia tayari inatekwa na waabudu shetani.

Ufunuo 9:15 inasema:
Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.

Theluthi ya wanadamu kwa leo duniani ni watu wangapi?
Tukiwa tunakaribia watu bilioni 8, theluthi ni watu karibu BILIONI TATU NA NUSU!
Hivi inawezekana watu bilioni 3.5 wakaondoshwa duniani?
Jibu ni NDIO, NDIO, NDIO!
Na tayari mchakato uko kazini hivi sasa usomapo maneno haya.

Tunaishi kwenye kurasa za mwisho za kitabu cha Ufunuo.

Nirudie kusema tena, dunia inatekwa na waabudu shetani.

Ibilisi anaitwa “audanganyaye ulimwengu wote” (Ufu 12:9).

Dunia inazidi kudanganywa kuwa inapewa kinga dhidi ya magonjwa. Wengi wameingia kwenye mtego wa yeye audanganyaye ulimwengu wote.

Wanadai kuwa eti tumekuwa wengi sana kiasi kwamba tunahatarisha dunia!
Yaani kwao ni bora kulinda mazingira kuliko kulinda uhai wa watu. Ni bora kwao wanadamu wapungue ili samaki, miti, fisi na nguruwe waongezeke kuliko kinyume chake.

Dunia inaenda kulazimishwa kumwabudu mungu wake kwa nguvu sana.

Dunia – sasa hivi inapelekwa kuwa kama ifuatavyo:
- serikali moja duniani kote
- kiongozi mkuu mmoja duniani kote
- jeshi moja duniani kote
- dini moja duniani kote
- sarafu moja duniani kote
…………
Heri watumishi wa Mungu wangeachana na kuhubiri mafanikio, wahubiri utakatifu na kutafuta Ufalme wa Mungu KWANZA na sio mafanikio kwanza.

Wakati umeshasonga sana.
Muda wowote Bwana Harusi ataondoa bibi harusi wake. Maneno haya tumeyasikia miaka mingi – lakini hakika, huu ndio muda wenyewe.
……….
Kama una maswali – na hasa kama wewe ni mtumishi unayechunga kanisa – karibu tujadiliane mambo haya kwa undani maana hapa naongea kwa juujuu tu.

Mambo yanayoendelea ni makubwa kuliko nilivyoandika hapa.

Lakini kwa wale wanaompenda Bwana Yesu – tuendelee kuchochea moto mioyoni mwetu. Hata hali iwe mbaya kiasi gani:

Danieli 11:23 inasema wazi:
Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.
………….
Giza linaifunika dunia lakini Yesu, aliye Jua la Haki, kwake hakuna giza.