Thursday, November 9, 2017

Kubatizwa kwa Moto Uwakao - 8


 
Ni siku nyingi zimepita tangu niweke ushuhuda unaohusu Kubatizwa kwa Moto. (Miaka takribani mitatu). Mungu amekuwa mwema, na kwa neema yake tutaendelea sasa na ushuhuda huu wenye nguvu sana na wa muhimu kwa kanisa na maisha ya mtu mmojammoja. Karibu tuendelee na Bwana wetu Yesu kristo akubariki.

==== SIKU YA 17 ==== 
 
Shemasi Shin, Sung-Kyung:
Tangu jumapili, nilikuwa naomba kwa kunena kwa lugha kwa siku tatu. Ghafla, mwili wangu ulihisi moto na nikaanza kuomba kwa nguvu hata zaidi kwa kunena. Mwanga mkali uliniangazia na nikaanza kutoka machozi, huku nikifanya sala ya kutubu. Machozi na jasho vilifunika uso wangu ilhali orodha ndefu ya dhambi zangu nilizotenda ilinijia akilini mwangu.

Sikuwa nikitunza kwa utakatifu siku ya jumapili kwa ajili ya kumwabudu Mungu, licha ya nafasi yangu kama shemasi kanisani kwetu na mara nyingi nilimpa wakati mgumu sana mchungaji wangu. Alijitahidi sana kuniambia maneno ya kunitia moyo, na pia ya kunikemea. Lakini yaliingilia sikio moja na kutokea jingine. Kwa nje nilionekana kama ‘shemasi’ wa kweli lakini moyo wangu haukuwa na muunganiko na Mungu. Hii ilikuwa ndiyo sababu kuu ya mimi kutaka kuhudhuria maombi ya mkesha na nilikuwa nimedhamiria kubadilika.

Kim, Yong-Doo: *Toba ya Mchungaji Kim
Siku ambayo ningepokea kipawa changu cha rohoni iliahirishwa kwa sababu sikutii agizo la Bwana la kutunza siri yake. Niliitoa siri hii kwa rafiki yangu wa karibu na hili lilimkasirisha sana Yesu. Kibinadamu, halikuwa jambo kubwa sana. Ni kosa ambalo mtu yeyote anaweza akalifanya, lakini mawazo ya Mungu ni tofauti kabisa na yetu. Kadiri tunavyozidi kuzama ndani zaidi ya ulimwengu wa roho, Bwana anataka tuwe makini zaidi na zaidi kiroho. Hadi pale ambapo kitabu kingekamilika, alitaka tujitenge kabisa na ulimwengu wa nje. Kwa siku tatu niliomba toba usiku na mchana, lakini hasira ya Bwana ilionekana kama hata haikupungua. Yesu aliniamuru niache kuandika kitabu. Uwezekano wa kuondolewa kwa karama ya rohoni ya kupambanua roho, unabii na karama zote sita ndani ya binti yangu Joo-Eun, pamoja na washirika wengine ulifanya moyo wangu ujae huzuni. Ilikuwa ni kama laana.
Sikujua cha kufanya. Niliwaza, “Nitachungaje kanisa hili? Nimeshakataliwa na Mungu? Mawazo haya ya aibu yalinijaa moyoni. Lakini sikukaa chini na kukata tamaa. Nililia, nikatubu, nikasihi, nikapaza sauti, na kuomba kwa namna zote mbalimbali za kuomba ambazo niliweza kuzikumbuka, huku nikiendelea kulia kwa sauti. Nilipoendesha mahubiri ya jioni, sikuweza hata kuona mbele yangu kwa sababu macho yangu yalivimba. Mahubiri ya saa nne hadi tano ambayo kwa kawaida huwa nayatoa bila shida ilikuwa vigumu na sikuweza kutoa mahubiri usiku ule. Taa zilizimwa na huku tukiimba, sote tuliomba toba kwa ajili ya dhambi zetu.
 “Bwana, tafadhali nipe nafasi moja tena!” niliomba. Nilitumia kila aya ya biblia iliyohusiana nami ili niweze kuomba msamaha kikamilifu. Kila mshiriki wa timu ya maombi alilia na kuomba pamoja nami kwa nguvu zote. Oh, niliguswa sana na kutoka machozi na kuwa na shukrani kwa washirika wangu! Bwana alikuwa na rehema kwa washirika hawa walio vijana na maskini.
Bwana aliposikia sala zetu zenye mguso, aliamua kunipa nafasi nyingine tena. Bwana alisema waziwazi kuwa kuanzia wakati huu, kila kitu lazima kiwe siri hadi pale kitabu kitakapotoka. Mtu hata mmoja nje ya kikundi hiki asijue mambo haya. Hata kwa washirika wenyewe, si kila kitu Bwana alitaka waambiwe, lakini kiasi fulani tu ndicho washirikishwe. Kila mazungumzo yaliyohusu jambo hili lazima yaidhinishwe na mchungaji na yahusu kile kiasi kidogo cha taarifa ambazo washirika wanazijua.

* Kubadilishwa kwa mikono yangu
Wakati ninaomba kwa dakika 30 huku mikono yangu ikiwa imeinuliwa juu, mikono hii ilianza kusogea kwa mtiririko fulani. Kwanza kiganja changu cha kulia kilisogea kuelekea nje. Baada ya kuendelea kuomba kwa kunena kwa lugha, kiganja changu cha kushoto nacho vilevile kilisogea kuelekea nje.

Usogeaji huo ulikuwa wa polepole. Nikawaza, kama hii ndiyo ilikuwa ni kasi ya kuamshwa kiroho, basi sitafikisha saa moja. Kwa washirika wengine, hata baada ya sala fupi, Yesu alijidhihirisha kwao na walikuwa na uwezo wa kuona mapepo. Mimi ni mchungaji. Kwa hiyo alishughulika na mimi kwa ugumu zaidi. Ilinichukua wastani wa dakika 20-30 kabla ya kuona dalili yoyote ya badiliko na kwa kasi hii, nilikuwa nahofia nisipoteze utashi au dhamirio langu.
Niliomba kwa saa mbili hadi tatu na, kama kawaida, mikono yangu ilirudia kule kusogea. Ndipo ghafla, nilihisi shoti ya umeme ikipita bila huruma ndani ya kichwa changu. Nikawaza, “Tayari; hapa ninatambulishwa kwenye ulimwengu wa roho,” na nikajawa na shauku ya kutaka kujua.  Nikaongeza nguvu kuomba, wakati ule mtiririko wa umeme ukiendelea kutetemesha mwili wangu mfululizo.

* Kundi la mapepo lashambulia
Kama kawaida, nilikuwa naomba huku mikono yangu ikiwa imeinuliwa juu, kwa takribani saa nne. Ghafla, kiumbe chenye umbo la ajabuajabu kilikuja na kunyonga mkono wangu. Kikanichoma shingoni kwa kitu chenye ncha kali na upande wa kulia wa mgongoni nikahisi kama vile nakatwa kwa kisu kikali. Nikalia kwa mateso makubwa kisha nikaanguka kuelekea mbele, huku mwili wangu ukiwa umepooza. Nikahangaika, lakini wapi! Sikuweza. 

Lile pepo likanidhihaki likisema, “Unathubutu kufanya macho yako ya rohoni yafunguke? Ukipokea uwezo huo, unadhani sisi tutapona? Hata sasa tunaadhibiwa vikali kwa sababu ninyi mnaomba kupita kiasi! Hatuna nafasi kwa sababu unasifu muda wote, unatoa mahubiri na unaomba, lakini inaonekana kwamba siku yako imefika leo. Umewachukua wajinga wasiojua chochote na umewasaidia kupokea vipawa vya rohoni. Utalipa kwa kile ulichokifanya!” Halafu kundi hilo la mapepo likaingia ndani ya mwili wangu. 

Nilikuwa napumua kwa shida. Mapepo yalisafiri kwa kusambaa ndani ya mwili wangu na kusababisha maumivu makali. Nilijaribu kujituliza kabisa, lakini bado maumivu yaliendelea tu. Mwili wangu wote ukawa na ganzi. Kila musuli, neva, kiungio na mfupa vilihisi maumivu makali sana.  Sikuweza hata kulia, licha ya kuwa nilikuwa kwenye maumivu makali kiasi hicho. Kila nilivyopiga kelele, ndivyo makovu yalivyozizima kwa maumivu. 

“Bwana, nisamehe. Niokoe. Tafadhali niokoe,” nililia. Washirika waliokuwa wanaomba walipatwa na mshtuko na mara moja walikimbilia madhabahuni. Wote waliogopa sana. Hawakujua wafanye nini. Kwa hiyo wakanitazama tu wakitarajia niwape ishara yoyote ya nini wafanye. Nikapiga kelele, “Enyi mapepo wachafu, kwa jina la Yesu wa Nazareti, tokeni kwangu!” Mapepo hayakuondoka. Nyakati nyingine nyingi, kila nilipotaja jina la Yesu, mapepo yalikimbia mara moja. Lakini safari hii, hata nilipopaza sauti sana wala hayakushituka.

Yakaanza kunikaba pumzi, huku yakishuka na kupanda kooni kwangu; na yakiendelea kunikatakata kwa shoka na kukamua mikono yangu. Mwishowe, yakanifanya nisiweze kabisa kuongea. Niliweza tu kupumua japo hata hilo lilikuwa jambo gumu na mwili mzima ukawa na maumivu. Nikakusanya nguvu zangu zote na kuwaambia washirika wangu wote wanizunguke na kuomba kwa nguvu zote. “Bwana! Bwana! Niokoe!” Nilijikuta tu maneno haya yananitoka bila kutarajia.

* Maombi yenye nguvu ya washirika
Washirika walipaza sauti zao. Nikawaomba washirika wenye kipawa cha macho ya rohoni kubainisha haraka ni aina gani ya mapepo yalikuwa ndani yangu, lakini wote kwa pamoja wakasema hawaoni chochote kabisa. Muda huu wote, kifundo cha mkono wangu wa kulia kilishapindishwa na kupooza.

Nikawahimiza washirika kumwita Yesu ili asaidie kubainisha ni mapepo gani. Tuliomba kwa muda mrefu na wale wenye kipawa cha macho ya rohoni wakaanza kusema kile walichokiona (Waefeso 1:18-19). Lile kundi la mapeo ndani yangu lilikuja kwenye Kanisa la Bwana likiwa na agizo maalumu kutoka wa pepo mkuu wa kuzimu. Kutokuonekana kwao na uwezo wao wa kujigeuza katika maumbo tofauti kulifanya iwe vigumu kuyaona bila kuomba kwa nguvu. Yesu alisema “Wanakondoo wangu wa thamani, kwa sababu ya maombi yenu mazito na ya kumaanisha pamoja na vilio kutoka kwa mchungaji wenu, nitawaruhusu muyaone mapepo hayo.”

Kulikuwa na takribani mapepo 30 na kumbe yalikuwa yakingoja kwa muda mrefu yapate fursa ya kushambulia. Pale mchungaji wa jirani pamoja na mke wake walipotutembelea, mapepo yalipata fursa na yakashambulia. Mfalme wa mapepo kuzimu alitoa amri ya moja kwa moja kwa sauti akisema, “Mtakapoingia kwenye Kanisa la Bwama, muwe makini sana kuliko mnavyokuwa kwenye makanisa mengine yoyote. Wapo washirika wengi wenye kipawa cha macho ya rohoni na wafuasi wangu wengi wa daraja ya chini wameshafukuzwa , kwa sababu sura zao halisi ziliweza kutambuliwa. Sasa, inabidi mngoje wakati sahihi wa kumshambulia Mchungaji Kim. Mpumbavu yule ndio chanzo cha matatizo haya. Tukiweza kumpiga akaanguka chini, kila kitu kingine kitafanyika kirahisi. Nendeni mkatekeleze hilo.”

Mke wa mchungaji wa kanisa la jirani na sisi hana aina ya imani itakayoweza kuwafanya mapepo wamfuatilie, na wala yeye mwenyewe hawafuatifuati mapepo. Kwa kile ninachojua, yeye ni mwombaji jasiri anayeomba kwa bidii. Mapepo yalijaribu kwa nguvu kuficha sura zao na yakatafuta chombo cha kutumia. Yalipojua kuwa mke wa mchungaji anajiandaa kututembelea, yakamfuata ndani na yakatumia hitaji la kudumu la mwanadamu la kutaka huruma kama ndio chambo.

“Yesu, tuonyeshe haya ni mapepo gani. Yesu, tafadhali yafunue kwetu tuyatambue,” sote tuliomba. Ndipo mtu mmoja akapaza sauti, “Nayaona! Nayaona!” Kulikuwa na mapepo takribani 15 yaliyoonekana ya duara kama chapati za dengu. Yalikuwa na macho mengi na yalikuwa yanazunguka mwili wangu. Mengine yalikuwa mapepo ya maumbo na ukubwa mbalimbali. Kulikuwa na tandu mkubwa, kiwavi, pepo jeusi kama kivuli, pepo la kike, na simba. Kwa wasiwasi nikawaambia washirika wangu wanizunguke na kuomba kwa bidii kwa kunena kwa lugha, huku wakigusa sehemu zilizokuwa na maumivu.  Walianza kugusa mwili wangu na wakaanza kuomba.
Mtu mmoja akapaza sauti, “Mchungaji, mapepo yanajigeuza! Hayatawanyiki lakini yanaungana!”
Nikajibu, “Unasema kweli? Ombeni kwa nguvu na mamlaka na kuyatoa nje!”
Washirika wakapaza sauti kwa sauti moja, “Kwa jina la Yesu, tokeni kwenye mwili wa mchungaji wetu! Rudini kuzimu!” 
Joo-Eun akapaza sauti, “Mapepo haya machafu yamekaa ndani yako huku mikono yao ikiwa imefungana pamoja. Hapana! Hapana! Tufanyeje sasa?”
Nikasema kwa sauti, “Endeleeni kuomba. Kama mkiacha, tutakuwa kwenye matatizo makubwa.”

Wote wakaomba kwa nguvu. (Waefeso 6:10-11) “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”
Dada Baek akapiga kelele, “Mchungaji, mapepo yamejigeuza tena.”
Nikauliza, “Yamekuwa nini sasa?”
Akajibu, “Inatisha! Safari hii yamekuwa tandu mweusi. Anauma shingo yako kwa meno yake mawili makali; na kwa mwiba, amechoma ndani ya mwili wako. Tufanyeje? Tandu mwenyewe ameng’ang’ania mgongoni mwako!” Mara moja, nilihisi maumivu makali na nikaruka, na kusababisha maumivu makali hata zaidi. Kisha nikaangukia mbele.
 
Nikapiga kelele tena, “Bwana, tafadhali nisaidie!” Haikujalisha nimeita kwa sauti kiasi gani, hakuja. Nikawahimiza washirika, “Harakisheni na mmwite Yesu!”
Wakaita kwa pamoja, “Bwana, uko wapi? Tafadhali harakisha uje umsaidie mchungaji wetu!”
Baada ya kumsihi, Yesu akatokea mbele yetu.

Nilikuwa na hasira, maana nilihisi Yesu amechukua muda mrefu mno. Nikawaza, “Yesu alikuwa wapi hadi akachukua muda mrefu kiasi hiki?” Yesu akanijibu, “Nitakusaidia. Usiwe na wasiwasi.” Kwa macho yao ya rohoni, washirika walimwona Yesu akiingia ndani ya mwili wangu na kusema alikuwa anayafukuza mapepo yatoke. Mapepo yale yaliungana tena na kuwa kitu kama mipira inayovutika.

Yesu aliyavuta nje. Kila alipoyavuta upande mmoja, yaling’ang’ania upande wa pili na kunata huko bila kutoka. Ilihitaji muda mrefu kuyatoa mapepo yale yaliyonakuwa yananata. Naamini Yesu alikuwa anatumia muda mrefu kwa makusudi ili kutufundisha imani zetu. (Yakobo 4:7)
Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.

Kwenye Biblia, Yesu alisema, mapepo hutetemeka mbele zake kwa woga na kutii. Lazima kulikuwa na sababu kwa nini Yesu alikuwa akichukua muda mrefu. Yesu alitaka kujaribu uimara wa kusanyiko letu na pia sisi tuone jinsi nguvu ya maombi ya pamoja inavyofukuza mapepo. Maombi yalianza saa sita usiku na kuendelea hadi saa moja asubuhi iliyofuata. Mwili wangu ulikuwa bado una maumivu na kusanyiko liliendelea na maombi.

Kusanyiko liliponizunguka na kuomba, tumbo langu lilinguruma na kujaa gesi. Mwili ulipata maumivu na tumbo langu lilikuwa kwenye maumivu makali sana kiasi kwamba sikuweza kustahimili tena. Kulikuwa na harufu isiyo nzuri kutoka kwangu ambayo iliwakera washirika. Nilijisikia aibu. Ilikuwa kana kwamba kuna kitu kilichooza ambacho kilikuwa kinanitoka.

Mtu mmoja akasema, “Tafadhali, hebu jizuie.” Aliposema hivyo, kila mtu alilipuka kwa kicheko. Nikasema, “Huu si wakati wa kucheka. Endeleeni kumwomba Mungu..” Kwa utii wakaendelea tena kuomba. “Joo-Eun, je, Bwana bado anaendelea kuondoa mapepo kwangu?” niliuliza. “Hebu harakisha kuangalia.” Mara moja, washirika watatu wakasema kuwa Yesu alikuwa akiyakamata mapepo moja baada ya jingine na kuyafunga. Mapepo mawili yaliyobakia yalikuwa mabishi. Lakini hatimaye Yesu aliyakamata na kuyafunga mapepo yote yaliyokuwa yamenitesa. Aliahidi kuwa atayatupa kwenye shimo lenye moto.

Baadaye Yesu alisema, “Safi! ‘Wanakondoo wadogo” wa Kanisa la Bwana ni watu wa kutilia maanani! Vilio na maombi yenu kwa ajili ya Mchungaji Kim, na pale mlipooingiwa na wasiwasi, na kuomba na kubakia naye wakati akipambana na mapepo kwa kweli mmenigusa sana. Hebu endeleeni kidogo tena. Nitafungua kipawa cha macho ya rohoni kwa Mchungaji Kim na ataweza kuona mambo ya Mbinguni na Kuzimu kwa undani. Kisha atarekodi mambo hayo kwenye kitabu na atawashirikisha ninyi pamoja na ulimwengu. Roho nyingi zilizopotea zitasoma kitabu hicho na kunirudia mimi.”

Niliporudi nyumbani na kujilaza chini ili kupumzika, vidonda kutokana na kung’atwa na kuparuliwa vilikuwa havivumiliki. Maumivu yalikuwa makali sana kiasi kwamba kupumua au kujilaza kulinifanya nipige kelele kwa maumivu. Mke wangu, Joseph, pamoja na Joo-Eun walianza kuomba kwa bidii.

Wakati Joo-Eun akiomba, alimsikia Yesu akisema, “Mapepo yalipoondoka, hayakuondoka kimyakimya. Badala yake, yaliacha athari za kitendo chao cha kukung’ata na kukuparua. Na athari hizo zitabakia na wewe kwa siku kadhaa zijazo. Kwa kuwa mke wako alipokea kipawa cha uponyaji, mwambie akuwekee mikono kwenye vidonda hivyo na akuombee.” 

Mara moja mke wangu aliniwekea mikono kwenye vidonda vyangu, lakini havikupona haraka kiasi cha kutosha. Nilijibiringisha ardhini kwa maumivu na kumwomba Bwana. “Bwana, mke wangu ana karama ya uponyaji, lakini kwa nini bado najisikia maumivu makali hivi?” Bwana akaeleza kuwa nguvu zake za uponyaji zilikuwa kidogo, lakini akanihakikishia kuwa nitapona hatua kwa hatua. Kwa kuwa sikuwa na subira, nilikimbilia kwa daktari ili anipe matibabu, lakini maumivu yalikuwa makali sana kiasi kwamba nikaachana na utaratibu huo wa tiba. Mke wangu akasema, “Katika miaka yetu 20 ya ndoa, sikuwahi kukuona ukiwa kwenye mateso na maumivu kiasi hiki.”

Dada Baek, Bong-Nyo: * Nyumba zetu kule Mbinguni
Wakati nikiomba kwa ajili ya mchungaji wangu, Bwana alinionyesha nyumba ya mchungaji wangu kule Mbinguni. (Yohana 14:2-3). Nyumba ya Mchungaji Kim ilikuwa na urefu wa ghorofa 360 hadi 370 na ya mke wake toka 270 hadi 280. Nyumba ya Joseph ilikuwa na ghorofa nne na ghorofa ya tano ilikuwa karibu kukamilika. Nyumba ya Joo-Eun ilikuwa na ghorofa 12 na ya 13 ilikuwa inaendelea. Nikauliza, “Bwana, nyumba za Joseph na Joo-Eun zinaendelea kujengwa ghorofa moja baada ya nyingine, wakati za mchungaji na mke wake zinajengwa ghorofa kumi kwa mara moja. Kwa nini?”
 
“Si tu kwamba mchungaji anaandaa mahubiri na kuwabariki kanisa kwa hayo, lakini pia anawaombea ninyi kwa bidii. Maombi ya mchungaji yana nguvu zaidi ya maombi yenu. Utumishi wa mchungaji kwa kusanyiko lake ndio unaowezesha nyumba yake kujengwa kwa haraka. Pia, mke wa mchungaji, Kang Hyun-Ja, huandaa chakula kwa ajili ya kusanyiko usiku na mchana. Si hivyo tu, katikati ya wiki analisha na kuvika familia yako kila siku. Malipo yake Mbinguni yatakuwa makubwa sana. Joo-Eun ana tabia ya kuongea kwa kupaza sauti na kubishana. Jambo dogo tu linamfanya akasirike. Anaweza kuwa mwenye kiburi, kwa hiyo mnyenyekeshe. Joseph ni mkimya kiasi kwamba mara nyingi anaonekana mwenye hasira. Hata ninapomwona, uso wake hauonyeshi urafiki na ninamtaka abadilishe tabia hiyo. Mchungaji wako anapotaja kwenye mahubiri yake kile ambacho Joseph anatakiwa akiboreshe, yeye hafurahii mapendekezo hayo. Nataka Joseph akubali kwa imani na utii lawama hizi zenye kujenga. Ndipo nyumba yake itajengwa.”
Nyumba ya Haak-Sung ilikuwa na ghorofa kumi na nguzo za ghorofa ya kumi na moja tayari zilikuwa zinajengwa na nyumba ya Yoo-Kyung ilikuwa na ghorofa saba. Yesu aliniambia, kwa kuwa siri ya kanisa letu ilifunuliwa na mchungaji na mke wake, ghorofa 50 za mchungaji na ghorofa 30 za mke wake zilibomoka. 

Nilipoenda kwenye ibada ya jioni, mchungaji Kim alionekana mdhaifu, kana kwamba alikuwa anaomba na kulia kwa muda. Macho yake yalikuwa yamevimba na alikuwa akipata tabu kutazama. Nilimwomba Bwana. “Bwana, mchungaji wetu amepata mateso mengi toka kwa mapepo leo. Mtie nguvu.” Kwa upole Yesu alikuja akanifariji mimi, “Kila mmoja ana wanafamilia wengi wa kumfariji, lakini mpendwa wangu Baek Bong-Nyo, hauna mtu wala kitu. Nitakufariji wewe.” Akaendelea kusema, "Unanipenda kuliko chochote na hii ndiyo maana ninakuthamini sana!”

Muda mfupi baadaye, malaika wawili wazuri walishuka kutoka Mbinguni. Walikuwa warefu na wazuri sana. Mmoja wao nilijua kuwa alikuwa Malaika Mkuu Mikaeli na mwingine alijitambulisha kwangu akisema, “Dada Baek, Bong-Nyo, mimi ni Gabrieli na ninasimama mbele za Mungu. Bwana ameniamuru kukusindikiza wewe. Kwa hiyo nimekuja.” Nikajibu, “Oh ndiyo, asante.” Wakaanza kunichukua tukaelekea juu angani. Ghafla, kundi kubwa la mapepo lilitokea na kutuzuia.

Nyuso za mapepo yale zilikuwa aina mbalimbali. Niliona kichwa cha dragoni, nyoka wakubwa, na roho mbalimbali za wanyama, wote wakiwa tayari kutuvamia. Walijikusanya pamoja na nguvu zingine za kipepo na mara nguvu yao iliongezeka sana. Lakini Gabrieli na Mikaeli hawakuingiwa na woga wowote hata kidogo. Badala yake, walikuwa wametulia. Walipoinua mikono yao, mapepo yalitoweka mara moja. (Ufunuo 12:7-9).

Baada ya mapepo kutoweka, tulifika Mbinguni, na Yesu akiwa amesimama kwa mbali, alinisalimia. Alisema kwa sauti, “Nakupenda, mpendwa wangu Baek Bong-Nyo. Nakupenda.” Yesu na mimi tulipaa kwenye mawingu, tukasafiri kote kwenye Mbingu. Kuna milima mingi Mbinguni, yote ikiwa ya dhahabu. Nilipoziangalia mbingu za Mbingu, wazo la kurudi nyumbani lilitoweka akilini mwangu.

Lee, Haak-Sung: * Yesu alia na Mchungaji Kim
Tuienda kwenye uinjilisti wa ushuhudiaji kuanzia saa 10 mchana hadi saa 1 jioni. Baada ya hapo, nilienda kanisani kuomba. Nilimwona mchungaji wetu akiomba na kulia akiwa amepiga magoti huku mikono yake ikiwa imeinuliwa juu. Nilimwona Yesu amesimama pembeni ya mchungaji. Yesu alivaa taji ya miba na alikuwa akilia huku akiwa ameelekeza macho yake chini kwa mchungaji. Kichwa chake kilikuwa kikitoka damu nyingi sana huku ikidondokea kwenye vazi lake. Alikuwa amelowa damu. Yesu alimkumbatia mchungaji Kim na aliendelea kuomba. Taa zote zilikuwa zimezimika kwenye madhabahu, lakini karibu na mimbari, nuru inayong’aa iliangaza kutoka kwa Yesu. Kwa nyuma, wimbo kuhusu mateso ya Yesu unaoitwa “Misumari mitatu” ulikuwa unaendelea kusikika.

Baadaye usiku ule, Yesu aliniambia, “Hata kama kuna baridi kiasi gani, ni vizuri kuomba ukiwa umevaa nguo nyepesi, ukiwa umepiga magoti na mikono yako ikiwa imeinuliwa juu wima. Ukijisikia baridi, nitakuletea moto, kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Ukivaa nguo nzito, utalala ukiwa unaomba. Unaelewa?”

Kim, Joo-Eun: * Kutubu kwa pamoja
Wakati ninaomba kwa kunena kwa lugha, dragoni la sura mbaya lenye vichwa vitatu lilinirukia. Likawa linakuja na kurudi nyuma ili kunitisha, lakini nikalitimua kwa kusema, “Kwa jina la Yesu Kristo, ewe pepo mchafu, ondoka! Ondoka kwangu!” Nikaendelea kunena kwa lugha. Yesu akatokea mbele yangu na alikuwa mkimya. Bila ya kusema neno, alisimama mbele yangu kwa muda mrefu huku akilia. Niliuliza maswali mengi, lakini yeye alilia tu. Leo, wakati wa ibada ya jioni, Mchungaji alikiri kwa machozi akisema, “Ninaumia sana, kwa sababu nimemsababishia Bwana uchungu mkubwa. Bwana, nimekutenda dhambi kubwa sana.” Sote tulijielekeza kwenye kuimba na kuomba toba kwa pamoja. Yesu, mchungaji na sisi sote, tulilia kwa pamoja. (1 Yoh 5:4).  

No comments:

Post a Comment